Aidha, suala hilo limepelekwa katika
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa
Mlalo (CCM), Brigedia Jenerali Mstaafu Hassan Ngwilizi, kwa ajili ya
kufanyiwa uchunguzi na kisha matokeo kurejeshwa bungeni.
Wakichangia hotuba ya makadirio ya mapato
na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini iliyowasilishwa bungeni juzi
na Waziri Sospiter Muhongo, walilamikia baadhi ya Bunge kuhongwa ili
kupitisha azimio la Maswi kuwajibika kwa kukiuka Sheria ya Manunuzi ya
Umma katika suala la manunuzi ya mafuta ya kuendesha mitambo ya
kuzalisha umeme wa dharura.
Spika Makinda alitangaza uamuzi huo jana
muda mfupi baada ya Bunge kupitisha bajeti hiyo, kufuatia Mbunge wa
Namtumbo (CCM) Vita Kawawa, kuwasilisha hoja ya kutaka Kamati hiyo
ivunjwe na suala la rushwa lipelekwe katika Kamati ya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge.
Kawawa alitumia kanuni ya 53 kifungu
kidogo cha pili na kanuni ya 55 kifungu F. “Nikuombe na kutoa hoja kwako
kwa kuwa tuhuma za suala hili ni nzito na linahusu Bunge na hivyo
kulidhalilisha kwa ujumla wake kwa kuwa tuhuma hizo ni nzito
kuzithibitisha. Naomba utumie mamlaka yako kuidhinisha,” alisema Kawawa.
Kawawa alimuomba Spika kwa mamlaka
aliyonayo akubali kuivunja Kamati ya Nishati na Madini na kamati
nyingine zilizowahi kutuhumiwa na rushwa.
Pia aliomba jambo hilo la rushwa
lililolalamikiwa sana katika hotuba hiyo, lijadiliwe na Kamati ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge, lifanyiwe uchunguzi ili ukweli wake
ukibainika na hatua ziweze kuchukuliwa.
Akijibu kuhusiana na hoja hiyo ambayo
iliungwa mkono karibu na Bunge zima, Spika alisema, “Naona hoja hiyo
imeungwa mkono na wabunge halafu iko wazi haina ubishi mwingine kwa
madhumuni sahihi na ametumia kifungu sahihi.”
“Sio tu hoja kwa siku zilivyokuwa
zinakwenda tabia ya waheshimiwa wabunge kwa maelezo haya imekuwa ni
kubwa nimeagiza kamati yangu ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge,
kutengeneza Code of Ethics (kanuni za maadili), na mtu yeyote
atakayetuhumiwa katika mazingira hayo (rushwa), lazima tuchukue hatua
tena kubwa.”
Spika Makinda alisema kamati hiyo
haitashughulikia tu mbunge anayehusika katika tuhuma hizo bali itakwenda
hadi kwa mtu anayehusika.
Alifafanua kuwa vimejitokeza vitendo vya mbunge kutoka jasho wakati akizungumza bungeni kumbe anafanya kazi ya mtu.
“Ni imani yangu kabisa serikali yetu na
nchi yetu inapita katika kipindi cha mpito na kama nyie wabunge
hamtakuwa imara kuweza kuisimamia Serikali kwa ukweli hatutaweza kwenda.
Matumaini ya wananchi yako wapi kama si Bunge?”alisema kisha kuongeza
kuwa:
“Kitendo hiki kwa kweli hakikubaliki ndani
ya Bunge, hatuwezi kuisimamia Serikali huku tunapokea pokea (rushwa).
Unaisimamiaje Serikali kwa mtindo huu? Kwa hiyo minaamini wabunge mkikaa
vizuri na kufanya kazi yetu vizuri, mabadiliko makubwa katika Serikali
yatatokea..Lakini wenzetu wanakwenda huko mara wajipendekeze mara
waombe hiki hatuwezi kwenda hivyo.”
Alisema kwa kutumia kanuni hiyo 53(3)
amelipeleka suala hilo katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya
Bunge, ili walifanyie uchunguzi na kuleta taarifa bungeni.
“Sasa hao mliokuwa mkitaka watajwe sasa
hiyo kamati itafanya kazi hiyo. La pili kwa kutumia kanuni 113(3) baada
ya kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Kawawa, naridhia ombi hilo,
nitaivunja na nyingine ambazo zimeonekana zikilalamikiwa katika hili,”
alisema.
Wajumbe wa kamati hiyo wanaongozwa na
Mwenyekiti Mbunge wa Bukene (CCM), Selemani Zedi na Makamu Mwenyekiti
wake ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Diana Chilolo.
Wajumbe wengine na majina ya majimbo yao
katika mabano ni John Mnyika (Ubungo-Chadema), Yussuf Haji Khamis
(Nungwi-CUF), Mariam Kisangi (Viti Maalum-CCM) na Catherine Magige (Viti
Maalum-CCM).
Wengine ni Abia Nyabakari (Viti
Maalum-CCM), Charles Mwijage (Muleba Kaskazini-CCM), Yusuph Nassir
(Korogwe Mjini), Christopher Ole Sendeka (Simanjiro-CCM), Dk Festus
Limbu ( Magu Mjini-CCM), Shaffin Sumar (Tabora Kaskazini-CCM), Lucy
Mayenga (Viti Maalum-CCM) na Josephine Chagula (Viti Maalum-CCM).
Wajumbe wengine ni Mwanamrisho Taratibu
Abama (Viti Maalum-Chadema), David Silinde (Mbozi Mgharibi-Chadema),
Suleiman Nchambi ( Kishapu- CCM), Kisyeri Chambiri (Babati Mjini-CCM),
Munde Abdallah (Viti Maalum-CCM), Sara Msafiri Ally, Vick Kamata, (Viti
Maalum-CCM) Mbarouk Salim Ali (Wete-CUF).
No comments:
Post a Comment