ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 19, 2012

Unataka kumjua anayekuibia mumeo? Mbinu hizi zitakufaa!


 
MPENZI msomaji wangu, mapenzi usipoyajulia yanaweza kukufanya ukawa chizi. Nasema hivyo kutokana na kile ambacho nimepanga kukiandika leo kupitia safu yetu hii.
Rafiki yangu mmoja wa kike ambaye tumekuwa tukishirikiana katika mambo mengi, juzi alinipa kisa ambacho kilinigusa sana hadi nikapanga leo niwaandikie mada hii ili nanyi muweze kujifunza kitu.
Aliniambia kuwa, wikiendi iliyopita alikuwa amejisikia kummisi sana mpenzi wake ambaye ilikuwa wafunge ndoa miezi kadhaa ijayo. Alisema:
“Nikiwa nyumbani nilimpigia simu, lengo nijue kama yuko nyumbani ili niende tukaliwazane. Wakati naongea naye kwenye simu, kwa nyuma nikasikia sauti ya demu akimuuliza; ‘mpenzi wangu ni nani huyo anakupigia simu’.
“Sauti ile ilinishtua sana na kwa kweli nilichanganyikia. Sikutaka kuwa na papara, nikadhamiria kuhakikisha namnasa mwanamke anayeniharibia uhusiano wangu.
“Kuanzia siku hiyo nikaanza kumfuatilia hadi nikawanasa pamoja. Leo hii naongea na wewe, yule mchumba wangu nimeshaachana naye kwani NIMETHIBITISHA si muaminifu.”
Rafiki yangu huyo ndiye aliyenipa baadhi ya mbinu alizotumia mpaka akamnasa mwizi wake na leo nimeona nikuletee mbinu hizo ili ikiwezekana na wewe uzitumie kumbaini mtu ambaye anakumegea penzi lako.

1. Ikague simu yake
Katika mazingira ya kawaida, haishauriwi kuikaguakagua simu ya mumeo kwani kufanya hivyo ni kuonesha jinsi usivyomuamini lakini unapohisi unaibiwa na hujui ni nani mwizi wako, unaweza kuanza kuikagua simu ya mpenzi wako kwa siri sana.
Angalia simu zilizoingia na kutoka, meseji zilizotumwa na kuingia. Kama kuna mtu ambaye ana uhusiano naye, utagundua lakini tambua kwamba ni zoezi la muda mrefu na fanya hivyo bila mpenzi wako kugundua. Tumia muda anaokwenda kuoga, chooni na anapoisahau simu nyumbani, ipo siku utabaini siri nzito.

2. Ingia kwenye Facebook yake
Kama mumeo ni mtu wa facebook na unajua password yake, ingia mara kwa mara kwenye ukurasa wake. Kama ulikuwa hujui mtandao huo wa kijamii sasa hivi unatumiwa na wengi katika kuzisaliti ndoa zao.
Waume za watu wanatumia njia hiyo kuwasiliana na vimada baada ya kubaini wakitumia simu ni rahisi kukamatwa. Kwa maana hiyo, tumia mbinu ya ushawishi kupata password yake na huko unaweza kumbaini mtu anayekuharibia.

3. Mfanyie ‘sapraizi’ kazini
Kama mumeo anafanya kazi, elewa kwamba wengi hutumia muda wa ‘lunch’ kuwa na wapenzi wao wa pembeni. Unaweza kumuibukia siku mojamoja kazini kwake au kwenda sehemu ambayo hupendelea kula chakula cha mchana.
Kwa mfano siku ya kwanza umemkuta yuko na demu, ukaondoka kisha siku nyingine ukawakuta tena pamoja, ukaondoka na siku nyingine tena ukawaona katika mazingira hayo, akili yako itakupa jibu.
Hata hivyo, katika njia hii uwe makini kwani inawezekana huyo msichana ni mfanyakazi mwenzake ambaye hupendelea kwenda naye lunch tu na hakuna kingine cha zaidi.

4. Chunguza nguo zake unapozifua
Wakati unafua nguo zake, tumia muda mwingi kuzichunguza. Angalia kwenye waleti yake, unaweza kukutana na risiti zinazoonesha amenunua vitu vya kike ambavyo wewe hujaviona.
Pia unaweza kukutana na vikaratasi vyenye namba za simu ambazo ukizipiga ni za mwanamke na ukimwambia wewe ni mke wa fulani, anakupa majibu ya kiwiziwizi. Pia kwenye nguo zake unaweza kubaini ‘lipstick’ nyekundu wakati wewe hutumii hiyo.

5. Muazime gari lake
Kama mpenzi wako analo gari, mshitukize kisha muombe gari lake uende sehemu. Kwa kumshitukiza atakuwa hajapata nafasi ya kulisafisha hivyo ukiwa nalo lichunguze kila sehemu.
Unaweza kukutana na risiti, namba za simu au nguo na vitu vya kike ambavyo huvijui. Wapo ambao waliwahi kufanya hivyo na wamefanikiwa kubaini usaliti wanaofanyiwa.

6. Mshitukize baa
Yawezekana mumeo ni mnywaji wa pombe na umekuwa ukimpa uhuru wa kufanya hivyo bila kumfuatilia. Kama umebaini unasalitiwa na humjui anayekuibia penzi lako, siku moja muulize anakunywa pombe wapi, kwa kuwa amezoea huna tabia ya kumfuatilia, atakujibu.
Siku hiyo mfuate, mwanamke utakayemkuta naye mnoti kisha ondoka bila mpenzi wako kujua. Siku nyingine, mbabatize tena akiwa baa na kama utamkuta na msichana yuleyule, basi mwekee alama na kwa uchunguzi ambao utaendelea nao, kuna siku utajua ukweli.

7. Mfuatilie
Hili nalo halishauriwi kulifanya kwani mpenzi wako akijua unamfuatilia, anaweza kukuacha kwani atajua humuamini na wengi hawapendi kuendelea kuishi na watu ambao hawawaamini. Ila sasa, ukishahisi unasalitiwa huna budi kufanya hivyo.
Tumia watu kufuatilia nyendo zake kila anapokwenda na haitachukua siku nyingi utajua huyo mpenzi wako anakusaliti na mtu gani.
Kwa kifupi ni kwamba, unastahili kuwa na mtu muaminifu, anayekujali na kukupenda kwa dhati. Unapohisi mumeo si muaminifu, usikimbilie kuomba talaka au kuja juu kama moto wa kifuu bila kuwa na ushahidi. Tumia mbinu hizo hapo juu kutafuta ushahidi wa kile unachokihisi na mwishowe utafanya uamuzi sahihi.
Tukutane wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

2 comments:

Anonymous said...

shukran sana kwa kutupa hizi mbini mimi nina wasi wasi na mpenzi wangu na katika mbinu ulizotupa nimeshazifuatilia mbili kuchunguza nguo zake na simu yake na kazini kumpa surprise ila ya kwenye baa naona kila nikimuliza anafetua tu kwamba huwa anakunywa sehemu kibao hata home si anakunywa any way shukran na nitakiyeni mema jamani kwa sababu huyu jamaa naona ananidatisha akili zangu

Anonymous said...

Kisa cha kujisumbua kumfuatilia? ukiona umefikia hapo jua huyo si mwenzako tena unapoteza muda wako.