ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 2, 2012

USISTADUU, UBRAZAMENI NA MAPENZI YA KICHINA -6



LEO ikiwa ni sehemu ya mwisho ya makala haya, nielekeze kuwa hatua muhimu zinaanza na wewe. Kama tabia mbaya ambazo nimekuwa nikizizungumza zipo ndani yako, tafadhali, jirekebishe haraka. Endapo wewe upo sawa na umebaini kuwa huyo unayemwita mwenzi wa maisha yako ana vitabia visivyofaa, muepuke haraka.
Ninaposema hatua muhimu zinaanza na wewe namaanisha katika pande kuu mbili. Mosi ndiyo hiyo ya wewe mwenyewe kujirekebisha pale unapoona unachemka. Pili ni kuachana na mwenzi ambaye anasumbuliwa na vitabia ambavyo nimevibainisha kinagaubaga tangu mwanzo wa makala haya.

UTAMJUAJE SISTADUU/BRAZAMENI
Nimeshakupa suluhu lakini kuna uwezekano ukawa hujafunguka inavyotakiwa. Hivyo basi, nakupa dondoo kadhaa ambazo nazichambua kwa kifupi ili kukuwezesha kutambua maana halisi ya kile ambacho nimekuwa nikikitambulisha tangu mwanzo mpaka kufikia hapa tunapokwenda kwenye tamati ya mada hii.
MTEGO WA FEDHA
Ipo wazi kuwa walengwa ni watu wanaobudu sana fedha kuliko utu. Unaweza kufanya kila linalohitajika kufanywa na wa jinsia yako kwa mpenzi wako lakini mwisho ukaishia kuumia. Utaonesha upendo na namna unavyojali lakini matokeo ya mwisho utaachwa solemba, huku ukilia kilio cha kusaga meno.
Anaweza kuwa nawe kwa sababu anavuta muda au anasubiri mambo yake yamnyookee akuache solemba. Inawezekana kweli akawa anakupenda lakini tabu ya mabrazameni na masistaduu mapenzi yao huwa nusunusu. Hata siku moja huwa hayakamiliki. Mifano ipo mingi ndiyo maana najenga hoja hii.
Yule brazameni ambaye alikuwa anajifanya anampenda mrembo wa umri wake, maisha yakawa matamu na kila mtu akadhani watafika mbali lakini baadaye yakatokea ya kutokea, kijana akaangukia kwa jimama anayejua kulea, matokeo yake bila huruma, akampiga teke mpenzi wake akiwa hajui la kufanya.
Siku zote unapowekeza upendo wako kwa brazameni au sistaduu, unapaswa kuwa mwangalifu, vinginevyo unaweza kujaa machozi mengi. Wewe kijana wa kiume, mpende na kumjali mwenzi wako lakini siku akipata mtu anayedhani ana fedha kuliko wewe, atamkimbilia na kukuacha na mateso ya moyo.
WANAPENDA KULELEWA
Hili ni jibu la yale ambayo nimeyaeleza kwenye kipengele kilicho hapo juu (Mtego wa Fedha). Unaweza kujiuliza ni kwa nini masistaduu na mabrazameni ni watumwa wa fedha. Jawabu ni kwamba wanapenda sana kulelewa ndiyo maana wanakuwa wepesi kushawishika na kukimbilia kwa wenye uwezo kifedha.
Asili yao ni watu magoigoi kwenye utafutaji. Hupenda kujilegeza, yaani wao ni lainilaini. Hali hiyo ndiyo huwafanya kuwa watumwa wa watu ambao hata hawawapendi. Kibinti kidogo kutembea na mzee mfano wa babu yake au kijana kujitumbukiza kwenye penzi la ajuza, anayemzidi umri hata mama yake mzazi.
Hii ikupe sababu ya kuona hatari iliyo mbele yako pale utakapojielekeza kwa mwenzi wako ambaye ana asili ya wale ambao nimewataja hapo. Fikiria kwamba wanataka muda wote wawe wamependeza hata kama hawana fedha, je, watakubaliana na maisha yako ya upendo wakati wanaona kuna sehemu ya fedha?
NIMALIZE KWA MFANO
Kuna ndugu yangu mmoja anaitwa Ponda, huyu ni mwanajeshi wa JWTZ, kutokana na sifa yake kitaaluma, aliwahi kuwa mwalimu Shule ya Sekondari Makongo. Huyu alikuwa na mke wake ambaye ni mtumishi wa Jeshi la Magereza. Tatizo la ndugu yangu huyo likawa ni kudanganywa na muonekano wa masistaduu.
Akiwa anafundisha, akadondokea kwa mwanafunzi wake ambaye ni sistaduu wa kutupwa. Baada ya kukolea kwa mwanafunzi huyo, akaanza kumletea visa mkewe (askari magereza). Zaidi akawa anamsimanga kuwa hajasoma na kwamba alikosea kumuoa. Mama ikamuuma, mwisho akaamua kuomba talaka.
Baada ya kuachana, Ponda akasubiri huyo sistaduu amalize kidato cha nne halafu akafunga naye ndoa. Unadhani maisha yalikuwa mazuri? Haikupita miezi mingi wakaacha kufuatia tabia ya mkewe huyo kuwa na tamaa ya fedha.

www.globalpublishers.info

No comments: