ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 1, 2012

BAHANUZI AITWA KIKOSI CHA STARS

KOCHA Kim Poulsen leo amemuita kwa mara ya kwanza mfungaji bora wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Said Bahanuzi wa Yanga, katika kikosi chake cha wachezaji 21 wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kitakachocheza mechi ya kirafiki ugenini Agosti 15 dhidi ya timu ambayo bado haijatajwa.

Pamoja na mshambuliaji huyo aliyejiunga na Yanga katika kipindi hiki cha usajili akitokea Mtibwa Sugar ya Manungu, Kim pia amemrejesha kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2010 kiungo Athuman Idd 'Chuji' aliyeng'aa katika michuano iliyomalizika Jumamosi ya Kombe la Kagame ambayo klabu ya Yanga ilitwaa ubingwa wa pili mfululizo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kim pia amemrejesha kikosini kiungo 'fundi' wa Simba, Haruna Moshi 'Boban' ambaye aliachwa na kocha aliyepita, Jan Poulsen, kufuatia kukacha kwenda kuchezea timu ya vijana kwa nia ya kuangalia uwezo wake.
Kocha huyo Mdenmark pia amemjumuisha katika kikosi chake kiungo wa Azam, Ramadhani Chombo 'Redondo' wakati makipa ni Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ali (Azam) na Deogratius Munishi 'Dida' wa Azam, ambaye aliisaidia timu yake kufika fainali ya Kombe la Kagame, ambapo ililala 2-0 dhidi ya Yanga.
Hata hivyo, Kim amemfumbia macho beki wa kati Nadir Haroub 'Cannavaro', licha ya mlinzi huyo kutengeneza ukuta mgumu pamoja na Kelvin Yondani na kuisaidia timu yao ya Yanga kutwaa ubingwa wa pili mfululizo wa Kombe la Kagame.
Wachezaji walioitwa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager wanatakiwa kuripoti kambi kwenye hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam, Agosti 8 mwaka huu saa 1 jioni tayari kwa mazoezi yatakayoanza siku inayofuata.
Makipa walioitwa kwenye kikosi hicho ni Deogratias Munishi (Azam), nahodha Juma Kaseja (Simba) na Mwadini Ali (Azam). Mabeki ni nahodha msaidizi Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Yanga) na Shomari Kapombe (Simba).
Viungo ni Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Moshi (Simba), Mrisho Ngassa (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba), Ramadhan Chombo (Azam), Ramadhan Singano (Simba), Salum Abubakar (Azam) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar).
Wachezaji wanaounda safu ya ushambuliaji ni John Bocco (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Said Bahanuzi (Yanga), Simon Msuva (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC).
 STORI NA DISMAS TEN 0718489260

No comments: