ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 7, 2012

Dar yafunga uandikishaji vitambulisho


Wakati zoezi la usajili na utambuzi  kwa ajili ya vitambulisho vya Taifa jijini Dar es Salaam limefungwa jana jioni, idadi kubwa ya wananchi wamelijitokeza kwa wingi katika baadhi ya vituo vya usajili huku wakiomba kuongezewa muda wa kujiandikisha.

NIPASHE ilishuhudia misururu vituoni ambapo katika wilaya Ilal,a Mtaa wa Tabata watu walionekana kuwa wengi huku Mwenyekiti wa mtaa huo, Hassan Chambusa, akisema watu waliojitokeza mwishoni ni vijana na watu wa makamo.

Eneo jingine katika Wilaya ya Ilala lililokuwa na watu wengi ni Mtaa wa Mchikichini.

Katika Wilaya ya Temeke kituo kilichopo Kata ya Mtoni watu walionekana kuwa wengi huku maeneo mengine yakikosa watu ikiwamo kituo kilichopo Kata ya Temeke-Mtaa wa Matumbi.

Mwenyekiti wa  Mtaa wa Matumbi ambaye pia ni mwekiti wa Umoja wa Wenyeviti Serikali za Mitaa wilaya ya Temeke (Uwesemite), Othman Omari, aliliambia NIPASHE kuwa kuna haja kwa serikali kusimamia sheria na ratiba wanazozipanga katika shughuli yoyote ili kuwajengea wananchi tabia ya kuwajibika kwa muda mwafaka katika mambo ya msingi na si kuongeza muda kila wakati.

“Serikali isimamie katika sheria pale inapopanga shughuli yoyote isiongeze muda ili kuongeza mwamko kwa Watanzania katika mikoa mingine kufuata muda uliopangwa katika kutekeleza zoezi hili. Kwa mfano, zoezi hili litaendelea kwa mikoa mingine je, katika mikoa hiyo wananchi wakidai kuongezewa muda baada ya muda uliopangwa kuisha watalalamika?” alihoji Omari.



Wakati huo huo katika Wilaya ya Kinondoni kituo cha serikali ya mtaa wa Makumbusho-Kata ya Kijitonyama kilichopo sokoni kilionekana kuwa na  idadi ndogo ya watu. Pia watu walipungua katika kituo cha kata ya Mbweni na Wazo.

Afisa habari wa Nida, Edward Nyange, alisema zoezi hilo limemalizika mkoani Dar es Salaam na kwamba wananchi watakaokosa usajili na utambuzi huo wasubirie tamko la uongozi juu ya kuongezwa ama kutoongezwa muda.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: