ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 3, 2012

FAHAMU NAFASI YA UONGO KATIKA MAPENZI!-2

KAMA unahitaji kuwa mpya ni vyema ukaweka ubongo wako huru kujifunza vitu vipya kila siku. Kwa kufanya hivyo, utajipa nafasi ya kupanua mawazo yako na kuwa wa tofauti zaidi.
Inawezekana kwa uelewa wako kuna mambo ambayo unayafahamu kuhusu mapenzi, lakini kwa kujenga utamaduni wa kujifunza, utaongeza kitu kingine kipya kila siku.
Naendelea kuchambua nafasi ya uongo katika mapenzi. Bila shaka mnakumbuka wiki iliyopita nilipoanza kwa kuelezea uongo unaokubalika na ule usiokubalika; leo tunakwenda moja kwa moja kuona aina za uongo unaokubalika.
Kumbuka yapo mengi sana ambayo ukiongopa hayana madhara katika uhusiano wako, lakini nimekuandalia yale ya muhimu zaidi. Karibu darasani.

WAPENZI WALIOPITA
Nani amewahi kuwa mkweli kwa mpenzi wake mpya kuhusu idadi ya mapatna aliowahi kutoka nao kimapenzi? Hebu anza na wewe mwenyewe? Jiulize, tangu umeanza mapenzi umetoka faragha na wanaume/wanawake wangapi? Je, upo tayari kumtajia mpenzi wako?
Umewahi kufanya hivyo? Rafiki zangu, kati ya mambo ambayo yanaudhi sana katika mapenzi, ni pale mpenzi anapogundua kwamba mwenzi wake ametoka na wapenzi wengi kabla yake.
Wengi wanatamani sana kusikia kwamba wao ni wa pili au tatu, vinginevyo akutane na mwanamke ambaye bado hajaanza kabisa mambo ya mapenzi. Rafiki zangu, tuwe wakweli, kumwambia mpenzi wako kwamba umeshatoka kimapenzi na wanaume hamsini, ni sawa na kumtangazia kwamba wewe ni malaya.
Hata kama ni kweli umetoka na idadi hiyo, akikuuliza ipunguze, mwambie yeye ni mwanaume wako wa nne! Wa kwanza alikutoa usichana ukiwa mwanafunzi, baada ya hapo ukaachana kabisa na mambo ya mapenzi.
Mwingine ulikutana naye chuo, ukamuacha baada ya kugundua kwamba alikuwa akipenda kukutumia tu, wa tatu ulifuma meseji ya mapenzi kwenye simu yake ukaamua kumuacha, yeye ni wa nne!
Mwanaume huyo atajisikia fahari sana kuwa na mwanamke mwenye namba ndogo ya wanaume aliotembea nao, ingawa moyoni mwako unaujua ukweli, lakini inabidi udanganye ili kulinda penzi lako. Tunakwenda sawa jamani?
UWEZO DUNI FARAGHA
Ukiwa na mpenzi wako, si ajabu sana katika mazungumzo yenu ya kawaida, akakuuliza kuhusu uwezo wako wa kucheza ‘kwata’ muwapo faragha. Kwa bahati mbaya kuna rafiki wenye matatizo ya hapa na pale faragha.
Baadhi ya wanawake husumbuliwa na tatizo la maumivu wakati wa tendo, kuchelewa kufika mshindo na hivyo kuachwa njiani au kupoteza hamu ya tendo.
Wanaume wao husumbuliwa na tatizo la kufika mshindo mapema, kushindwa kurudia tendo na kuchoka mapema wakati mwenzake akiwa bado angali anamuhitaji.
Kimsingi matatizo makubwa hapa husababishwa na utayari wa kisaikolojia, maandalizi duni n.k. Unapozungumza na mwenzako kuhusu hili, hutakiwi kumpa taarifa za kweli. Zipo athari kadha wa kadha za kuwa mkweli juu ya matatizo uliyonayo katika eneo hili.
Kubwa zaidi, unajiongezea tatizo, maana utakuwa unaingia uwanjani ukiwa unajua kabisa kwamba mpinzani wako anajua udhaifu wako hivyo ni rahisi kukushinda!
Matatizo ya aina hii hutibiwa zaidi na mtu mwenyewe, kugundua udhaifu wake na kuufanyia kazi. Kama umegundua kwamba unapata maumivu wakati wa tendo, ni wazi kwamba maandalizi si ya kutosha, dawa yake hapo ni kutumia muda mwingi katika maandalizi kabla ya kuanza kazi yenyewe.
Kueleza tatizo lako moja kwa moja, kutamfanya mwenzako awe na mawazo, akiamini kwamba ama hutaendana na kasi yake, hatakufurahisha au utamuacha njiani. Kwa mtazamo huo ni rahisi sana kufikiria kuachana na wewe ili akatafute anayeendana naye.
Unachotakiwa kufanya ni kuonesha kwamba unaridhishwa na mambo yake faragha, lakini wakati unawasilisha kutoridhika kwako iwe kama vile lengo lako ni kuboresha pale alipoishia.
Kwamba yupo vizuri, lakini unataka afanye vizuri zaidi kwa kutoa mawazo yako juu ya mambo ya kufanya. Mnaona mambo haya marafiki?
Nafasi yangu kwa leo imeishia hapa, wiki ijayo tutaingia katika sehemu ya mwisho, HAKIKISHA HUKOSI!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na Who is your Valentine vilivyopo mitaani.

No comments: