ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, August 12, 2012

FAMILIA YA MAREHEMU PATRICK MAFISANGO YATELEKEZWA, YATUPIWA VYOMBO NJE



Orly Ilemba, akiwa nje ya nyumba aliyokuwa akiishi na marehemu kaka yake, Patrick Mafisango baada ya mwenye nyumba kutoa nje vyombo vya ndani kutokana na deni la pango.

Baadhi ya vyombo vya ndani vya aliyekuwa kiungo mahiri wa Simba, marehemu Patrick Mafisango vikiwa nje ya nyumba aliyokuwa akiishi katika eneo la Keko Bora jijini Dar es Salaam, baada ya mwenye nyumba kuvitoa nje kutokana na deni la pango.


Na Andrew Chale

FAMILIA ya aliyekuwa kiungo mahiri wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba, marehemu Patrick Mutesa Mafisango iko katika wakati mgumu baada ya kutimuliwa katika nyumba waliyokuwa wakiishi, Keko Bora jijini Dar es Salaam.

Familia hiyo, ilitolewa nje vifaa katika nyumba hiyo na mmiliki wake, kutokana na kudaiwa kodi ya pango aliyokuwa akiudai  kwa muda mrefu uongozi wa Simba.

Akizungumza kwa masikitiko makubwa jana, mdogo wa marehemu Mafisango, Orly Ilemba, alisema, mwenye nyumba huyo, Chingweni Mtoro, aliwafuata asubuhi na kutaka chumba chake kabla yakutoa vitu hivyo nje ya chumba na kuweka kufuli jipya.
“Nipo nje tokea asubuhi, hatujafanya lolote, zaidi nalinda vitu vya marehemu, viongozi wa Simba kila nikijaribu kuwapigia simu hawapokei mpaka sasa sina la kufanya,” alisema Ilemba.

Alifafanua kuwa, viongozi hao wa Simba walijua mwisho wa kukaa humo, lakini wameshindwa kushughulikia suala hilo mapema mpaka wanakutwa na aibu hiyo.

“Lakini mwenye nyumba huyu, alisema mkataba huo ulitakiwa kufika mwisho Agosti 8, kamawalivyokubaliana na viongozi wa Simba, lakini mpaka jana viongozi hao hawakuweza kumalizana naye ndio maana kaamua kufikia hatua hii,” alisema kwa masikitiko.

Mdogo huyo wa marehemu Mafisango, yupo nchini kwa ajili ya kusubiria rambirambi, ambazo klabu ya Simba iliahidi kuzitoa.

Juhudi za kuupata uongozi wa klabu ya Simba, kujua wana taarifa na wanachukua hatua gani, zilishindwa kuzaa matunda kwani wahusika, hawakupatikana.

Mafisango kati ya nyota mahiri waliochangia kwa kiasi kikubwa timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita iliyofikia tamati Mei 6, alifariki dunia Mei 17, 2012 kwa ajali ya gari, eneo la Keko, jijini Dar es Salaam.

Juhudi za kuupata uongozi wa Simba kuzungumzia hali hiyo ilishindikana baada ya baada ya simu msemaji wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga kutopatikana kwa siku ya jana.

No comments: