Kigogo mmoja wa Mamlaka ya Mapato
(TRA) Mkoa wa Tanga, anadaiwa kula njama na kufanikiwa kupata Sh.
milioni 2 kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete.
Kigogo huyo aliyetajwa kwa jina
moja la Masingisa anadaiwa kufanya njama hizo akishirikiana na uongozi
wa Serikali ya kijiji cha Chongoleani kumuingiza mkenge Rais wakati
alipokwenda kufanya ziara kijijini hapo.
Hayo yalibainika baada ya wananchi
wa kijiji hicho kulalamikia kitendo hicho walichodai kuwa ni cha utovu
wa nidhamu kwa watumishi wa serikali ambao walitakiwa kuonyesha mfano
katika kukemea vitendo vya kihuni kama hivyo.
Wakielezea sakata hilo, wananchi
hao walidai kuwa kigogo huyo kwa kushirikiana na uongozi wa serikali ya
kijiji walimpeleka Rais kwenye shamba lake ambalo ameanzisha ufugaji
samaki na kumdanganya kuwa ni kikundi cha wanakijiji jambo ambalo si
kweli.
Omar Mustaph alieleza kuwa
wanakijiji hao walidai kuwa Rais alipofanya ziara mkoani Tanga, waliomba
atembelee kikundi chao cha ufugaji wa samaki na kwamba uongozi wa
kijiji uliwahakikishia kuwa ombi lao la kutembelewa na Rais
limekubaliwa.
Mustaph alidai kuwa baada ya Rais
kufika wakiwa wamejiandaa kumpokea, walishangaa kuona uongozi wa kijiji
kumpeleka Rais katika shamba la kigogo huyo badala ya lile ya kikundi
chao.
“Unajua tuliona kama miujiza,
tukajiuliza vipi!?. Rais apelekwe katika kikundi kingine badala ya kile
cha kijiji?...tulikosa jibu” alisema Mustaph.
Alidai kuwa Rais alichangia Sh. 2
milion katika kikundi hicho fedha ambazo ziliwastahili wanakijiji hicho
kuimarisha mradi wao wa ufugaji wa samaki unaosuasua.
Walisema kuwa baada ya Rais
kuondoka waliufuata uongozi wa kijiji kuuliza kulikoni Rais kutembelea
kikundi kingine badala ya cha kwao na kudai kuwa walipata majibu ya
vitisho ya kuwa wasijaribu kuchokonoa mambo ya wakubwa.
Akijibu madai hayo kwa njia ya simu
ya kiganjani, mtumishi huyo wa TRA aliyejitambulisha kwa jina moja la
Masingisa alikiri kupokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Rais Kikwete
na alipoulizwa kwanini alipelekwa katika kikundi chake badala ya kile
cha wanakijiji alidai kuwa yeye pia anastahili kupata fedha hizo na ni
haki yake ya msingi.
Alipotakiwa kufafanua madai ya
kumtapeli Rais, Masingisa alieleza kuwa kikundi hicho kipo kisheria na
kina usajili wake na uongozi na kwamba yeye ni mtunza hazina na kuna
mwenyekiti na katibu wake ambao alimshauri mwandishi kuzungumza nao pia.
“Wewe bwana sikiliza, kwanza Rais
Kikwete kaja kwangu akijua anakuja kwa Masingisa na wala si kwenye
kikundi cha wanakijiji kama inavyodaiwa…usihoji kajaje huu ni urafiki
wetu,” alisema afisa huyo.
Aidha alidai kuwa si ajabu kwa Rais
huyo wa nchi kutembelea mradi huo kwa kuwa wao ni marafiki wa karibu
na kwamba alikuja kama kwa jamaa yake.
“Wewe andika tu! Lakini ukiandika
vibaya nitakushitaki, mimi niko nyuma ya wakubwa na wala sina hofu na
madai hayo wala kuandika kwako, hata hii kazi niliyonayo aliniwezesha
yeye kuipata…wee! andika tu hakuna tatizo,” alisema Masingisa.
Naye Katibu wa kikundi hicho
kinachojulikana kwa jina la Kigomen fish farm, Omar Kombo, alieleza kuwa
Rais hakupelekwa kwenye kikundi cha wanakijiji kwa kuwa hakukuwa na
maandalizi ya kutosha kumpeleka mkubwa wa nchi.
“Ni kweli Rais hakupelekwa, lakini
ni kutokana na mazingira hayakuwa mazuri huwezi kumpeleka kiongozi
sehemu isiyovutia bwana, hiyo ndiyo sababu kubwa,” alisema Kombo
alipozungumza kwa njia ya simu ya kiganjani.

No comments:
Post a Comment