MDAU wa michezo na aliewahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Villa Squad Fc ya Magomeni jijini Dar es Salaam, Ally Kindoile amejitosa kuwania nafasi ya Katibu Msaidizi wa Chama cha Soka Mkoa wa Kilimanjaro (KRFA), unaotarajiwa kufanyika mkoani humo Agosti 28 mwaka huu.
Akizungumza na Blog ya VIJIMAMBO kwa njia ya simu jana, Kindoile ambaye pia aliwahi kukaimu kwa muda nafasi Mwenyekiti wa Villa kabla ya kushuka daraja, alisema kuwa, amechukua uamuzi wa kuwania nafasi hiyo, ili kuinua soka la Mkoa wa Kilimanjaro na pia kurudisha sifa na heshima iliyokuwepo miaka ya nyuma kwenye mchezo huo.
Kindoile, alibainisha mipango yake mikubwa kuwa ni pamoja na kupandisha timu ligi kuu na kunyakua mataji mbalimbali ikiwamo Taifa Cup.
“Naomba wadau wa michezo mkoani hapa, kwa pamoja kushirikiana kwa hali na nguvu ili kuleta maendeleo ya soka, kwa kuwa pamoja tukishirikiana tunayo nafasi ya kurudisha hali na morali kwa vijana na wanamichezo ndani ya Kilimanjaro na siku za usoni tupate timu yetu itakayoshiriki ligi kuu Tanzania Bara,” alisema Kindoile.
Licha ya kuwa mdau wa michezo, aliwahi kuchezea timu mbalimbali zikiwemo Simba B na Idrisa Fc, kwa sasa ni mdau mkubwa wa timu ya Kilimanjaro Rangers ya mkoani Kilimanjaro na amekuwa kwenye mstari wa mbele katika kusaidia vijana kwenye soka, huku kwa vipindi tofauti alifanikiwa kuipandisha timu ya Villa Ligi Kuu kwa vipindi viwili ikiwemo msimu 2010-2012.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake