Sunday, August 12, 2012

Lema amwomba Slaa agombee Arusha Mjini


Godbless Lema
CHADEMA YACHANGISHA FEDHA KUNUNUA HELIKOPTA , VIJANA WAONGOZA JAHAZI 
Raymond Kaminyoge  
MBUNGE wa zamani wa Arusha Mjini, Godless Lema amesema anatamani Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa agombea ubunge wa jimbo hilo akieleza anaamini atatoa mchango mkubwa zaidi kwa chama kabla ya mwaka 2015.Lema  alitoa kauli hiyo juzi usiku jijini Dar es Salaam, wakati wa harambee ya kuchangia chama hicho kwenye kampeni yake ya Vuguvugu la Mabadiliko maarufu kama Movement for Change (M4C) mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema katika chama hicho kuna watu wengi wanaoweza kuwa wabunge wa jimbo hilo, lakini yeye binafsi angependa Dk Slaa awe mbunge wa Arusha Mjini kwa sababu Katibu Mkuu huyo wa Chadema  akiwa bungeni ni moto wa kuotea mbali.

Lema alisema: “Kuhusu ubunge wa Arusha sina hofu, atakuja Dk Slaa au mimi, ingawa sasa napenda aje Dk Slaa.”
Alisema angefurahi kama Dk Slaa angekuwa mbunge wa jimbo hilo hasa katika kipindi hiki cha kutafuta mabadiliko kumpokea  wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. 


Lema alisema hivi sasa anafurahia mchango mkubwa anaoutoa katika chama chake akiwa nje ya Bunge.
“ Nahisi kutoa mchango mkubwa katika chama nikiwa nje ya Bunge kuliko nilivyokuwa bungeni kwa sababu nimefanya shughuli nyingi zenye matokeo chanya katika taifa hili,” alisema Lema.

 Lema alienguliwa ubunge mwaka huu na Mahakama ya Kuu Kanda ya Arusha kwa kilichoelezwa kuwa alitumia lugha chafu katika kampeni za kuusaka ubunge huo mwaka 2010.

Kuchangia fedha za M4C
 Lema alieleza kuwa fedha zitakazopatikana katika harambee hiyo zitatumika kununulia helikopta, magari, pikipiki, baiskeli na matumizi mengine ya Chadema kwa ajili ya kufikisha ujumbe wa ukombozi kwa wananchi.

“Tusifanye siasa ili kutafuta vyeo bali  tulenge kuleta mabadiliko chanya katika jamii iliyonyanyasika kwa muda mrefu. Nchi yetu ilipata uhuru, lakini sasa tunahitaji mabadiliko yanayowakomboa wananchi kutoka kwenye umasikini,” alisema Lema.

Kauli ya Mbowe
Akizungumza katika harambee hiyo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuwa, propaganda za ukabila, udini na rangi zinazoenezwa na CCM ni dhaifu na zimeshindwa kuidhoofisha Chadema.

 Alisema kuwa wananchi wamezishtukia propaganda hizo na kwamba, wananchi wengi wamehamasika kutaka mabadiliko.
 Katika harambee hiyo zaidi ya Sh270 milioni zilipatikana, kati ya hizo Sh250 milioni zikiwa ni ahadi na Sh20 milioni zikiwa ni fedha taslimu.
Kati ya fedha hizo, Sh20 milioni zilichangwa na tawi la Chadema nchini Marekani likiwa na majimbo yake Washington DC, Maryland na Virginia.

 Watendaji wa Serikali
Kivutio kikubwa kilikuwa kwa baadhi ya watendaji wa Serikali kuchangia katika harambee hiyo na kutaka waitwe Wasamaria wema bila kutaja majina yao.

Mbowe alisema: “Kwa kuwa wananchi wametuamini, tumeacha njia ya maandamano na sasa tunataka kufika kila kata ya nchi hii ili kufikisha ujumbe wa mabadiliko kwa wananchi. "

Alisema kuwa wamekubaliana baada ya kumalizika kwa kikao cha Bunge wabunge wote wa Chadema watasambaa nchi nzima kueneza Vuguvugu la Mabadiliko.
 Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema kuwa mbali ya kufika kwenye kila kata chama hicho pia kimejipanga kufikisha ujumbe huo katika nchi zote ambako kuna Watanzania.

“ Hatuna mchezo sasa, tumejipanga kuchukua dola ifikapo 2015, hawa CCM sasa ni kama wanaweweseka hawajui wanalolifanya, tutawang’oa tu, ” alisema Mbowe.

  Alisema kuwa chama hicho kikifanikiwa kuchukua dola, kipaumbele kikubwa kitakuwa ni kuboresha elimu ambayo ni sekta muhimu kwa maendeleo ya taifa.

“ Kipaumbele namba moja, mbili hadi tatu kitakuwa ni elimu. Tutawekeza zaidi kwenye elimu ili kuwawezesha wananchi kuhimili changamoto za dunia ya sasa hasa katika usimamizi wa rasilimali zao,” alisisitiza Mbowe.
 Aliwahimiza watu wanaokichangia chama hicho kwa kuficha majina yao kuacha hofu akisema: “Jitokezeni hadharani, hamna sababu ya kuhofu kama kweli mnahitaji mabadiliko. Tumepuuzwa, tumenyanyaswa na tumedhalilishwa kiasi cha kutosha, sasa basi tuache woga.”

Alisema kuwa, CCM imeshindwa kuwasikiliza madaktari, walimu na wafanyakazi wengine lakini Chadema inaahidi kushughulikia matatizo ya makundi hayo.
  Akizungumzia umuhimu wa harambee hiyo, Mbowe alisema mabadiliko yana gharama zake na kwamba wadau ndiyo wanapaswa kuchangia chama hicho.
Mbowe aliomba kila mpenda mabadiliko kuchangia kwa kadri ya uwezo wake na kwamba fedha zake zitailetea mabadiliko nchi hii.

Vyeo
Akizungumzia suala la nafasi za uongozi ndani ya chama hicho, Mbowe alisema kuwa, huu si wakati wa kugawana vyeo wala kutangaza nafasi za kugombea bali kukiimarisha chama ili kiweze kuwa na nguvu zaidi.
Naye Mwenyekiti wa M4C, Mkoa wa Dar es Salaam, Alex Mayunga alisema harambee hiyo  ilikuwa na lengo la kukusanya Sh5 bilioni katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema katika hafla ya jana walipanga kupata Sh500 milioni, lakini hazikutimia kutokana na msongamano wa wananchi waliokuwa wakituma fedha kwa njia ya simu za mkononi.

“Tunadhani hadi kesho (leo) kiasi hicho kitatimia kwa sababu wananchi wengi wametuma fedha lakini bado hazijatufikia,” alisema Mayunga.
 Aliwataka wananchi kutuma fedha kwa kutumia njia ya simu za mkononi  kwa sababu hiyo ndiyo njia rahisi.

Mwananchi

1 comment:

  1. Akili kama hii ya Lema kumtaka Dr Slaa kugombea kiti cha ubunge Arusha mjini ni akili inayoonesha upeo mkubwa na kupevuka kisiasa, mimi binafsi toka kutenguliwa kwa ubunge wa Lema nilijua kabisa kwamba Lema ananafasi kubwa sana ya kuwa mbunge wa Arusha mjini hata uchaguzi ungerudiwa siku ileile. Napenda kumpongeza Lema nakuwambia kwamba nakubariana na yeye asirimia elfu moja kwamba akae pembeni kuendelea kukijenga chama na pamoja na kutafakari yeye binafsi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

    Mdau Washington DC.

    ReplyDelete

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake