Thursday, August 9, 2012

Maiti 136 wa ajali ya Skagit zapatikana Z’bar

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema idadi ya maiti waliopatikana katika ajali ya boti ya Mv Skagit imefikia 136 tangu kutokea kwa ajali hiyo Julai 18, mwaka huu.
Takwimu hizo zilitangazwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alipokuwa akizungumza na uongozi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) uliofika ofisini kwake Vuga na kutoa mkono wa pole kufuatia ajali hiyo jana. 


Malozi Seif alisema kwamba hadi sasa maiti zilizopatikana 136 ziliopolewa, watu waliookolewa ni hai 146, na watu wanane hawajapatikana kwa mujibu wa idadi ya abiriwa 290 walikuwemo kabla ya boti kupinduka na kuzama katika mkondo wa Pungume Zanzibar.
Balozi Seif alisemakufuatia ajali hiyo,  Baraza la Usalama la Taifa Tanzania  limeshaamua  kuagiza meli na boti zote zinazoagizwa au kununuliwa ni lazima zipate ridhaa ya kukubalika kitaalamu kutoka kwa mamlaka zinazosimamia usafiri wa majini.
Alisema kwamba Mamlaka ya Usafirishaji Baharini Zanzibar (ZMA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Nchi kavu na Majini Tanzania bara (Sumatra), pia  zimetakiwa kuzingatia ukaguzi wa meli pamoja na viwango vya ubora kabla ya meli au boti kuruhusiwa kutoa huduma hiyo.
Alisema ajali hiyo imeacha msiba mkubwa katika taifa na serikali inaendelea na kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kuhakikisha wananchi wa pande mbili za muungano wanakuwa na usafiri wa uhakika katika mwambao wa bahari ya Tanzania.
Balozi Seif alipokea mchango wa maafa wa Shilingi milioni 10 kutoka kwa uongozi wa BoT.
Mchango huo ulikabidhiwa na Mkurugenzi wa BoT Zanzibar, Joseph Mhando, kwa niamba ya Gavana wa BoT.
Mhando alisema uongozi wa BoT umefarajika na hatua mbali mbali za uokozi zilizofanywa na serikali kupitia vikosi vya ulinzi na usalama baada tu ya kutokea kwa hajali hiyo.
“Tunastahiki kuipongeza serikali kupitia washirika wake hasa vikosi vya ulinzi na uokozi kwa kuendesha zoezi zima la uokozi katika  mazingira magumu,” alisema Mhando.
Wakati huo huo, Tume ya kuchunguza ajali hiyo imeanza kuwahoji watu mbalimbali wakiwemo walionusulika katika ajali hiyo mjini Zanzibar.
Tume hiyo yenye wajumbe 10, inaongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu, Abulhakim Issa Ameir, iliundwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kutafuta ukweli kuhusiana na sababu zilizosababisha ajali hiyo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake