Wanafunzi waendelea kurandaranda
Mahakama kuamua kesho
Mahakama kuamua kesho
Mahakama hiyo ilitoa taarifa hiyo jana jioni baada ya kukamilisha kusikiliza madai ya upande wa Jamhuri na Chama cha Walimu Tanzania (CWT).
Mgomo huo uliotangazwa na CWT Julai 30, mwaka huu umepelekea walimu katika shule za msingi na sekondari nchini kutofika kazini kabisa huku shule nyingi zikibakiwa na walimu wakuu na wakuu wwa shule pekee.
Kutokana na hali hiyo, wanafunzi katika shule hizo jana walishuhudia wakicheza kwenye mazingira ya shule hizo.
Shule za Wilaya ya Temeke zabakiwa na walimu wakuu tu. Katika Shule ya Msingi Serengeti, iliyopo wilayani Temeke, NIPASHE ilitembelea na kukuta mwalimu mkuu pekee.
Mwalimu huyo ambaye aliomba jina lake lisitajwe, alisema serikali haiwezi kukwepa madai ya walimu hivyo inachotakiwa ni kutimiza baadhi ya mambo yaliyoombwa na walimu.
Katika Shule ya Msingi Muungano, walimu wawili waliripoti kazini na kujiorodhesha katika kitabu cha mahudhurio kisha wakaondoka na kumuacha mwalimu mkuu pekee.
Walimu sita wa Shule ya Msingi ya Mbalala walioripoti kazini walisema licha ya kufika kazini, lakini hawatakuwa tayari kuingia madarasani kufundisha.
Walimu hao ambao walikataa kutaja majina yao, walisema watakuwa tayari kuingia madarasani kufundisha, baada ya serikali kutoa tamko kuhusu madai yao kama imekubali kuyapatia ufumbuzi.
Katika Shule ya Sekondari ya Benjamini William Mkapa jijini Dar es Salaam, ambako Rais wa (CWT), Gratian Mukoba, anafundisha, walimu katika shule hiyo walikuwa wamejikusanya nje ya madarasa wakijadiliana.
Walimu hao walipoulizwa kwanini hawakuingia madarasani kufundisha, walidai kuwa taarifa zote zinapatikana kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki.
WANAFUNZI WAANDAMANA
Wanafunzi wa shule za msingi za kata ya Wazo na Kunduchi, jana waliandamana kwenda ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam wakidai kuwa wanakwenda kudai haki yao ya kufundishwa.
Wanafunzi hao waliandamana huku wakirusha mawe. Walilalamika kuwa walimu walikuwa wanafika shuleni na kujiandikisha katika vitabu vya mahudhurio kisha kuondoka bila kufundisha.
CWT: MGOMO UKO PALE PALE
RAIS wa CWT, Gratian Mukoba, amesisitiza kuwa mgomo utaendelea licha ya vitisho kadhaa vilivyoanza kutolewa na serikali.
Akizungumza na NIPASHE jana, alisema walimu wasiogope vitisho vya serikali kwani CWT imefuata taratibu zote zinazotakiwa katika mgomo.
Mukoba pia alikanusha taarifa zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa alikwenda kazini juzi.
“Nimeshawasiliana na mwanasheria wangu kuvifikisha mahakamani vyombo vya habari vilivyoripoti kuwa nilikwenda shuleni ninakofundisha na kusaini daftari la mahudhurio, taarifa zisizo za kweli,” alisema.
Kuhusu kwanini walimu waliingia kwenye mgomo wakati suala la mgogoro kati ya CWT na serikali upo mahakamani, alisema taarifa za mahakamani walizipata baada ya mgomo kuanza.
KAWAMBWA AENDELEZA VITISHO
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukru Kawambwa, amesisitiza kuwa serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria walimu wanaotishia wenzao waliokataa kugoma.
Akizungumza katika mahojiano na redio ya Clouds FM, alisema baadhi ya walimu na viongozi wa CWT wamekuwa wakiwatisha walimu wasiogoma na kwamba wakibainika serikali itawachukulia hatua kali.
Aidha, aliwataka wazazi na wanafunzi wasijiingize katika vurugu kufuatia mgomo kwani serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha mgogoro unapatiwa ufumbuzi haraka ili usiathiri elimu.
POLISI DAR WAONYA
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linafanya uchunguzi kuwasaka watu wachache wanaotishia walimu na kuwafukuza darasani ili wasiendelee kufundisha kutokana na mgomo wa walimu.
Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Suleiman Kova, alisema jana kuwa jeshi hilo limepata taarifa za kuwepo na kundi la baadhi ya walimu ambao wanawatishia wenzao waliokataa kugoma ili wakibainika wachukuliwe hatua za kisheria.
CWT Dar: mgomo wetu siyo batili
Nayo CWT Mkoa wa Dar es Salaam imesema mgomo wa walimu ni halali kwa kuwa ulifuata taratibu zote za kisheria hivyo madai yanayotolewa na serikali kwamba ni batili hayana ukweli.
Mwenyekiti wa CWT wa mkoa huo, Zubeda Aziz, alisema mgomo huo siyo batili kwa kuwa ulifuata sheria .
Alisema walimu 12,447 wa shule ya msingi na sekondari walipiga kura ya kuitishwa kwa mgomo ambapoi kati yao 11,542 waliunga mkono.
MGOMO DAR WAFANIKIWA ASILIMIA 90
Alisema mgomo katika Mkoa wa Dar es Salaam umefanikiwa kwa asilimia 90 kwa walimu kulala nyumbani bila ya kwenda kazini japokuwa zipo shule tatu ambazo hazijashiriki kwenye mgomo huu.
Alizitaja shule ambazo walimu wake hawajashiriki kuwa ni Shule ya Msingi Bunge, Vingunguti na Shule ye Sekondari ya Mnazi Mmoja.
Aziza aliwataka walimu kupuuza uvumi ulioenezwa kuwa viongozi wa chama hicho wamewasaliti wanachama wao kwa kwenda kazini.
ILALA, KINONDONI WAGAWANYIKA
Baadhi ya walimu katika shule za msingi na sekondari katika Manispaa za Kinondoni na Ilala wamegawanyika kuhusiana na mgomo huo ambapo wameonekana wakiendelea kufundishani kama kawaida huku wengine wakiwa wamesaini katika vitabu vya mahudhurio na kurudi majumbani.
Katika Shule ya Msingi Mchikichini, walimu walionekana wakifundisha huku wanafunzi wakithibitisha kufundishwa vipindi vya asubuhi.
Mwanafunzi Maliki Yunus wa Mchikichini alisema walifundishwa masomo kadhaa, likiwemo Jiografia na Hisabati.
Katika Shule za Msingi Boma na Mkoani, walimu tangu juzi walikuwa wakifika shuleni na kusaini vitabu vya mahudhurio na kuondoka.
“Walimu wangu wamefika kazini kama kawaida na kusaini kitabu cha mahudhurio kisha wakaondoka,” alisema Betty Msenga, Mwalimu Mkuu wa Boma.
Naye Mwalimu Mkuu Mhule ya Msingi Mkoani, Jane Mganwa, alisema walimu walifika kazini na kufundisha.
Kwa upande wa Shule za Manispaa ya Kinondoni wanafunzi walidai walimu walifika kazini asubuhi na kuondoka.
“Walimu walikuja asubuhi, lakini hawajatufundisha na baadae waliondoka,” alisema Mariamu wa Shule ya Msingi Msisiri.
Katika shule za msingi za Turiani, Lions, na Ally Hassan Mwinyi, wanafunzi walionekana wakicheza nje huku walimu wao wakiwa katika vikao.
CWT MWANZA WALAANI POLISI
CWT mkoani Mwanza kimelaani kitendo cha Jeshi la Polisi kujiingiza katika mgogoro huo kwa kuwakamata baadhi ya walimu wanaoshiriki mgomo huo.
Katibu wa CWT mkoani hapa, Issac Chaushi, alisema jana kuwa amepokea taarifa za walimu kadhaa kubughudhiwa na kukamatwa na polisi kwa kushiriki mgomo.
“Nimepata taarifa kwamba kuna walimu wamekamatwa na polisi, ila kwa sababu za kiusalama sitaweza kuwataja kwa sasa, lakini napenda kutumia fursa hii kulaani kitendo hicho kwa sababu mgomo wetu ni halali na hakuna chombo chochote ambacho kinapaswa kuingilia,” alisema Chaushi.
Aliongeza kwamba kitendo cha kutumia polisi kuwakamata walimu wanaodai haki zao kwa mujibu wa sheria, ni matumizi mabaya ya dola, ambapo askari hao wana kazi nyingi za kukabiliana na uhalifu.
Mgomo huo umeonekana kuathiri mahudhurio sio tu ya walimu bali pia wanafunzi katika shule mbalimbali za msingi jijini Mwanza.
Katika shule za msingi Nyanza, Kitangiri, Kirumba A, na B,Azimio, Shamaliwa, Nyamanoro, Nyakato na Gedeli mahudhurio ya wanafunzi kushuka.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyamagana A ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema karibu nusu ya wanafunzi hawakuhudhuria shuleni jana.
Katika shule ya msingi Nyanza walimu ambao hawakutaka majina yao yatajwe gazetini walisema CWT kilipaswa kufanya hamasa kubwa zaidi shule hadi shule ili kuwezesha walimu wote kugoma.
MAHAKAMA KUTOA UAMUZI KESHO
Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Sophia Wambura, jana alisema kuwa uamuzi wa ama kusitisha mgomo huo au la utatolewa kesho baada ya kumaliza kusikiliza maombi ya upande wa Jamhuri na CWT.
Upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Obadia Kameya na Pius Mboya uliwasilisha maombi kutaka mgomo usitishwe kwa muda na Mahakama itoe masharti kwa Rais wa CWT na Katibu Mkuu wa CWT kutozungumzia suala hilo kwa vyombo vya habari hadi uamuzi utakapotolewa.
Kameya na Mboya walidai mgomo uliotangazwa na CWT ni batili kwani chama hicho kilitakiwa kutoa notisi ya siku 60 badala ya masaa 24.
Kwa upande, wakili wa CWT, Gabriel Mnyelle, alidai kwamba mgomo ni halali sababu ipo sheria inayoruhusu kufanya hivyo endapo malalamiko yanashindwa kufikia mwafaka ndani ya siku 30.
Mnyelle alidai kuwa serikali iache tabia ya kukimbilia mahakamani na badala yake iwe inakubaliana na wafanyakazi wake kufikia mwafaka katika madai wanayokuwa wanayataka.
Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe, Hellen Mwango, Jimmy Mfuru, Isaya Kisimbilu, Neema Nyagonde, Samson Fridolin, Mrema Juma, Leonce Zimbandu, Happy Kaiza, Jacqueline Yeuda, Dar na Happy Severine, George Ramadhan, Mwanza.
Viongozi wanne wa CWT watiwa mbaroni
Viongozi wanne wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) katika baadhi ya wilaya mkoani Mbeya wamekamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuhamasisha walimu wenzao kushiriki katika mgomo wa walimu ulioanza juzi nchini, huku watu tisa wakishikiliwa na Jeshi hilo kwa tuhuma za kushiriki vurugu ubwa zilizotokea jana katika mji mdogo wa Tunduma wilayani Momba.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Athuman Diwani, alisema jana kuwa viongozi wa CWT waliokamatwa walikuwa wakishirikiana na watu wengine kupita kwenye shule mbalimbali mkoani Mbeya kuwashinikiza walimu wanaoendelea kufundisha ili washiriki kwenye mgomo wa walimu.
Aliwataja viongozi hao kuwa ni Katibu CWT Wilaya ya Kyela, Patro Mangula (52); Katibu wa CWT Wilaya ya Rungwe, Akson Kibona na wajumbe wawili wa wa CWT Wilaya ya Ileje ambao ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Mbebe, Emmanuel Kyejo (45) na Mwalimu wa Shule ya Msingi Mkumbukwa, Anyakingwe Lwingwa (54).
Alisema watuhumiwa wote baada ya kamatwa walifikishwa mahakani kwa ajili ya kujibu tuhuma zinazowakabili.
Kuhusu vurugu zilizosababisha kuvunjwa kwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya mji mdogo wa Tunduma, Kamanda Diwani alisema kuwa baada ya upelelezi kufanywa na Jeshi la Polisi, watu tisa wametiwa mbaroni kuhusiana na vurugu hizo
Watuhumiwa hao ni Meck Mbilinyi (52), Akida Kondo (25), Charles Lupia (29), Athuman Mgala (39), Stella Gilbert (20), Atilio Mnyamwanga (28), Nicodemus Mnyamwanga (17), Mashaka Kyusa (27) na James Kabuje (29), wote wakazi wa mji mdogo wa Tunduma.
Alisema pia Jeshi la Polisi limefanikiwa kuokoa baadhi ya mali zilizoibwa katika ofisi za Mamlaka ya Mji huo ambazo alizitaja kuwa ni mabati 168, printa moja, mita mbili za maji, bendera moja ya Taifa na mashine moja ya kurufu.
Wakati huo huo, mgomo uliendelea jana na baadhi ya walimu kutofika kabisa shuleni huku wale wanaofika wakisaini kitabu cha mahudhurio na urejea majumbani.
Wanafunzi katika shule mbalimbali walikuwa wakicheza nje ya shule huku wengine wakirandaranda mitaani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Athuman Diwani, alisema jana kuwa viongozi wa CWT waliokamatwa walikuwa wakishirikiana na watu wengine kupita kwenye shule mbalimbali mkoani Mbeya kuwashinikiza walimu wanaoendelea kufundisha ili washiriki kwenye mgomo wa walimu.
Aliwataja viongozi hao kuwa ni Katibu CWT Wilaya ya Kyela, Patro Mangula (52); Katibu wa CWT Wilaya ya Rungwe, Akson Kibona na wajumbe wawili wa wa CWT Wilaya ya Ileje ambao ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Mbebe, Emmanuel Kyejo (45) na Mwalimu wa Shule ya Msingi Mkumbukwa, Anyakingwe Lwingwa (54).
Alisema watuhumiwa wote baada ya kamatwa walifikishwa mahakani kwa ajili ya kujibu tuhuma zinazowakabili.
Kuhusu vurugu zilizosababisha kuvunjwa kwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya mji mdogo wa Tunduma, Kamanda Diwani alisema kuwa baada ya upelelezi kufanywa na Jeshi la Polisi, watu tisa wametiwa mbaroni kuhusiana na vurugu hizo
Watuhumiwa hao ni Meck Mbilinyi (52), Akida Kondo (25), Charles Lupia (29), Athuman Mgala (39), Stella Gilbert (20), Atilio Mnyamwanga (28), Nicodemus Mnyamwanga (17), Mashaka Kyusa (27) na James Kabuje (29), wote wakazi wa mji mdogo wa Tunduma.
Alisema pia Jeshi la Polisi limefanikiwa kuokoa baadhi ya mali zilizoibwa katika ofisi za Mamlaka ya Mji huo ambazo alizitaja kuwa ni mabati 168, printa moja, mita mbili za maji, bendera moja ya Taifa na mashine moja ya kurufu.
Wakati huo huo, mgomo uliendelea jana na baadhi ya walimu kutofika kabisa shuleni huku wale wanaofika wakisaini kitabu cha mahudhurio na urejea majumbani.
Wanafunzi katika shule mbalimbali walikuwa wakicheza nje ya shule huku wengine wakirandaranda mitaani.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment