ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 4, 2012

Mwakyembe adai Sh317.7 bilioni zinatosha bajeti yake


Waziri wa Uchukuzi,Dk Harrison Mwakyembe
Boniface Meena,Dodoma
WAZIRI wa Uchukuzi,Dk Harrison Mwakyembe amesema Sh 317.7 bilioni alizoliomba Bunge kwa ajili ya bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2012/13 zinamtosha hata kama kuna watu wanasema kiasi hicho ni kidogo.

Alisema ili wizara yake iweze kutekeleza majukumu na malengo yake katika mwaka huu wa fedha kiasi hicho kinatosha kuitoa sekta ya uchukuzi ICU.

Dk Mwakyembe alisema hayo juzi wakati akijibu hoja za wabunge waliochangia hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2012/13.

"Bajeti hii mimi inanitosha kwani sekta ya uchukuzi ilikuwa ICU,"alisema Dk Mwakyembe.

Alisema kati ya fedha hizo Sh 64.9 bilioni zitakuwa ni za matumizi ya kawaida na Sh252.7bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

"Fedha za matumizi ya kawaida zinajumuisha Sh37.0 bilioni za mishahara ya watumishi na Sh27.8 , fedha za matumizi mengineyo,"alisema Dk Mwakyembe.

Alisema fedha za miradi ya maendeleo zinajumuisha Sh189.7 bilioni ambazo ni fedha za ndani na Sh52.9 bilioni fedha za nje.

Wakati Dk Mwakyembe akiomba kiasi hicho cha fedha, Kamati ya Bunge ya Miundombinu imesema, wizara hiyo imetengewa fedha kidogo ikilinganishwa na mahitaji halisi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba aliliambia bunge kuwa wizara ya uchukuzi ni miongoni mwa wizara chache zinazoweza kuchochea ukuaji wa uchumi kwa haraka kwa kuwa fedha inayowekezwa katika wizara hiyo inakwenda kuzalisha fedha zitakazotumika kuboresha sekta nyingine.

"Pamoja na ukweli huu, wizara hii imetengewa fedha kidogo ikilinganishwa na mahitaji halisi kwani mwaka wa fedha 2011/12 ilitengewa jumla ya Sh167.9 bilioni baada ya Bunge kushinikiza fedha za maendeleo ziongezwe katika sekta ya reli na bandari,"alisema Serukamba.

Alisema Serikali iliahidi kuongeza Sh95 bilioni na hivyo fedha za maendeleo kufikia jumla ya Sh262.9 bilioni lakini hadi kufikia Mei mwaka huu fedha za maendeleo zilizotolewa ni jumla ya Sh96.7 bilioni sawa na asilimia 57.6 ya fedha ambayo bunge liliomba kutaka iongezwe.

No comments: