Siku sita tangu awadanganye wanachama wa Simba kuwa mchezaji Emmanuel Okwi amefanya majaribio na kufuzu Ulaya, mwenyekiti wa klabu hiyo Isamil Aden Rage amelia hadharani akitangaza kujitoa uongozi wa moja ya kamati za TFF -- shirikisho la soka.
Rage jana alitangaza kujivua nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF, akituhumu baadhi ya viongozi wa shirikisho hilo kutoitendea haki timu yake.
Mwenyekiti huyo wa Simba ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM) aliwaambia wanachama wa Simba katika mkutano Jumapili iliyopita kuwa Okwi alifanya majaribio na kufuzu katika klabu ya Red Bull Salzburg ya Austria.
Lakini akizungumza na Nipashe mapema wiki hii, Okwi alisema hakufanya majaribio yoyote Ulaya kutokana na kusumbuliwa na Malaria tangu awasili barani humo mpaka kurejea Uganda na kisha Simba.
Alipoulizwa kama haoni kuwa aliwadanganya wanachama wa Simba alipowaeleza jambo ambalo linakanushwa na mchezaji husika jana, Rage ambaye alidai pia kuwa mchezaji huyo atakuwa akilipwa euro 300,000 kwa mwezi na Redbull alisema:
"Okwi hakwenda kutalii kule... mimi ninasema kitu kilicho sahihi.
"Alifanya majaribio na kufuzu. Haya maneno mengine ni ya magazeti tu... sasa kama hajafanya majaribio alienda kufanya nini kule kwa kipindi cha wiki nzima."
Kwa mujibu wa taarifa za mtandao rasmi wa kompyuta wa Red Bull Salzburg, imesajili wachezaji wawili tu kati ya tarehe za Okwi kwenda Ulaya mpaka kurudi -- Valon Berisha kutoka Viking Stavanger na Havard Nielsen kutoka Valerenga Oslo. Zote za Norway.
Akizungumza na waandishi wa habari Bungeni mjini Dodoma jana, Rage alisema amejitoa katika kamati hiyo baada ya kuchukizwa na kitendo cha Yanga kumsajili beki wa APR ya Rwanda, Mbuyi Twite ambaye Simba ilishaingia naye mkataba, na kwa baraka za TFF.
Alisema TFF ina wajumbe wengi ambao ni wanazi wa Yanga na hivyo kushindwa kuitendea Simba haki.
“Kama serikali na mamlaka za kusimamia soka zitaonekana zinapendelea timu moja, basi wapenzi na wanachama wa Simba wanaweza kuamua kuangalia kwingineko ambako wanadhani watapata haki zao za msingi,” alisema Rage na kulazimika kukatisha kwa muda mkutano wake baada ya kumwaga machozi.
Rage hakufafanua Serikali inaingiaje katika suala la kuonewa kwa Simba huko anakodai, wala kama amepewa ridhaa na wanachama wa Msimbazi kuishutumu serikali yao kwa niaba yao.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesigwe, amesema kuwa wanasubiri muda ufike wamtangaze rasmi Mbuyi Twite atakayechezea timu hiyo msimu ujao wa ligi kuu ya Bara.
"Hiko kitu kipo (usajili wa Mbuyi), lakini siwezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa," alisema.
"Ngoja tusubiri wakati wake ufike na mchezaji ataonekana hapa kwa sababu hili sasa hivi limekuwa na mvutano kidogo."
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment