ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 25, 2012

Twite ruksa kukipiga Yanga 2013

Wakati uongozi wa klabu ya Simba ukiwekea pingamizi kwa Shirikisho la soka kutaka mchezaji Mbuyi Twite asiidhinishwe kukipiga Yanga, TFF jana imetangaza kutua kwa Hati ya Uhamisho wake wa kimataifa kutoka klabu ya FC Lupopo ikithibitisha imemuuza kwa mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati.

Afisa habari wa Shirikisho la soka (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa ITC ya mchezaji huyo pamoja na mshambuliaji Didier Kavumbagu kutoka klabu ya Atletico ya Burundi zimetua nchini na wachezaji hao sasa ruksa kuichezea klabu hiyo.



"Tumepokea ITC 11 kati ya 14 zilizombwa na klabu mbalimbali za ligi kuu hapa nchini na kati ya hizo pia ipo ya Mbuyi Twite iliyoombwa na Yanga... hizo ITC zimetufikia hapa TFF," alisema Wambura.

Kutua kwa ITC ya Mbuyi Twite kunamaliza mkanaganyiko wa usajili wa mchezaji huyo ambaye awali aliripotiwa kusajiliwa na mabingwa wa soka nchini Simba kupitia kwa Mwenyekiti wake, Ismail Aden Rage.

Rage ambaye kudanganya kwake na kupanda jukwaani na bastola katika mikutano ya kampeni kumeonekana kuwa miongoni mwa sababu za kubatilishwa ushindi wa aliyekuwa Mbunge wa CCM wa Igunga Dk. Peter Kafumu, alilia siku alipozungumza na waandishi wa habari Dodoma kupinga kitendo cha Yanga kutangaza kumnyaku Twite.

Simba imeiandikia barua TFF kulalamikia juu ya usajili wa mchezaji huyo pamoja na beki Kelvin Yondani.

Lakini kutua kwa ITC hiyo ya Twite kunapelekea mchezaji huyo kuwa huru kuitumikia klabu ya Yanga kwenye msimu ujao wa ligi kuu ya Bara.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kuwa malalamiko ya uongozi wa klabu ya Simba ya kuwataka wajumbe wa kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi ya Wachezaji akiwemo mwenyekiti wake, Alex Mgongolwa, Iman Madega na Lloyd Nchunga kutokuwemo wakati wa kupitia malalamiko ya usajili wa Twite na Yondani kwa kuwa ni wanachama wa Yanga hayana msingi.

Osiah alisema kuwa kamati hiyo inafanya kazi kwa kufuata kanuni na sheria na sio mapenzi binafsi ya timu ya wajumbe wa kamati hiyo.

Osiah, alisema kuwa katika kamati hiyo pia wamo mwenyekiti wa klabu ya Simba, Isamail Aden Rage na Omar Gumbo ambaye ni mwanachama wa klabu hiyo.

"Kama Simba wanataka hivyo, basi hata Rage na Gumbo hawastahili kuwemo kwenye kupitia usajili kwa sababu ni wana simba... haya mamabo hatuyapeleki kwa mapenzi ya timu hii kamati inafuata kanuni na sheria zilizopo," alisema Osiah.
CHANZO: NIPASHE

No comments: