Thursday, August 9, 2012

`Wanaotetea Muungano wa mkataba wana ajenda ya siri'


Mwanasiasa mkongwe Zanzibar, Mgaza Othman Mgaza, amesema viongozi wanaotetea Muungano wa mkataba kuzingatiwa katika mabadiliko ya Katiba mpya, wana ajenda ya siri ya kutaka kuuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Mgaza aliyasema hayo jana katika mahojiano maalum na NIPASHE nyumbani kwake Kisauni Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Alisema iwapo marekebisho ya Katiba yatazingatia hoja hiyo, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utavunjika na kubakia historia yake.

"Nashaanga sana kuona viongozi wanatetea Muungano wa mkataba wakati mfumo huo kama itakubalika, Muungano utakufa na kubakia historia yake," alisisitiza.

Alisema wananchi wa Zanzibar lazima watumie busara na hekima kabla ya kuamua kuunga mkono hoja za kuvunja Muungano huo.

“Muungano kama unavunjika kila upande raia wake watalazimika kuondoka, jambo ambalo litaleta athari kubwa kwa wananchi wa pande mbili," alisema.

Alisema kitendo cha Zanzibar kuwa na bendera yake na kiti Umoja wa Mataifa chini ya muundo wa Muungano wa mkataba, sawa na kuuvunja Muungano wenyewe.

Mgaza alisema kama kuna viongozi wa chama na serikali Zanzibar wanaafiki mfumo wa Muungano wa mkataba, hakuna sababu ya Muungano wa Tanganyika kuendelea kuwepo nchini.

Alisema kitendo cha Zanzibar kuwa na kiti chake Umoja wa Mataifa na bendera, sawa na kuvunja Muungano wenyewe.



Mgaza ambaye aliwahi kuwa mgombea mwenza wa Jamhuri ya Muungano kupitia cha cha TLP 2010, alisema wananchi lazima wawe makini na kampeni zinazoendelea kufanyika za kutaka Zanzibar kujitenga katika Muungano.

“Wazanzibari  lazima tutumie busara na hekima kabla ya kuamua kuvunja Muungano, sisi ndiyo tutaumia na nje ya Muungano suala la Upemba na Unguja litaibuka tu,” alisema.

Aidha, alisema Wazanzibari wengi wamenufaika na ardhi Tanzania bara pamoja na kutumia soko la biashara la watu milioni 40 na kupata mafanikio makubwa katika sekta ya biashara.

Kadhalika, alisema vijana wengi Zanzibar wamekuwa wakinufaika na ajira kupitia Vikosi vya Ulinzi na Usalama mbali na masomo ya elimu ya juu kila mwaka.

Mgaza alisema kwamba pamoja na wananchi wa Pemba kuwa ni watu wanaonufaika kwa kiwango kikubwa na fursa za Muungano, bahati mbaya ndiyo wamekuwa mstari wa mbele kupinga Muungano.

“Ajabu  watu ambao wananufaika na Muungano ndiyo wanaokuwa mstari wa mbele kuupinga," alisema.

Aliongeza kuwa kampeni za kuvunja Muungano zinazoendelea na baadhi ya viongozi katika Chama na Serikali Zanzibar kunatokana na kuweka maslahi binafsi mbele badala ya maslahi ya Taifa.

Pia alisema mfumo wa serikali mbili ndiyo mwafaka katika kulinda Muungano isipokuwa Rais wa Zanzibar awe Makamu wa Pili Rais katika itifaki ya Tanzania.



 
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

  1. Hapa Bwana Mgaza kama yuko makini na serikali yake anayoitetea ya Muungano wangefanay utafiti kwa nini wanaonufaika na Muungano hawautaki?
    Na jee Wazanzibari 3000 walioajiriwa kwenye Vyombo vya ulinzi vya Muungano ndio wawateke nyara Wazanzibari uhuru wao kwa viel wao watakosa kazi wakati Wazanziabri watawatumia wao kuunda Jeshi la Polsii na Vyombo vyengine vya Ulinzi kuimarisha Ulinzi visiwani Zanzibar.
    Hakuna sababu ya kuwasikiliza wanasiasa wa Zanzibar ndio waliowadumaza wananchi wao na kufanya Muungano ndio uonekana umewadumaza wakati uongozi mbovu wa SMZ ndio uliowadumaza , njia pekee ni kukubali Demokrasia ifuate Mkondo wake visiwani tusikubali kutumia Mwamvuli wa Serikali ya Muungano kulinda viongozi wabovu Zanzibar tunapolinda viongozi wabovu ndio tunauvunja Muungano kwani viongozi wabovu ndio tatizo la Zanzibar. Pia tukubali Wananch iwa Zanzibar waulizwe kwenye Sanduku la Kura kama wanautaka Muungano au hawautaki hapo ndio tutaweza kujadiliana na kwua na Muungano wa kweli , tuwe na Muunagno wa wananchi sio wa wanasiasa.

    ReplyDelete

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake