Thursday, September 13, 2012

Hukatazwi kujikweza ila mumeo ana ‘hela’?

NDUGU zangu, mapenzi si pesa! Nakumbuka nilishawahi kulizingumzia hilo kwenye makala zangu zilizopita. Wapo walio kwenye uhusiano wenye furaha licha ya kwamba hawana vipato kiviile.
Hata hivyo, pesa nayo ina umuhimu wake katika uhusiano lakini hata isipokuwepo penzi linaweza kuendelea. Kitu ninachotaka kukizungumzia leo ni kuhusiana na hii tabia ya baadhi ya wanawake kujifanya ni matawi ya juu wakati wao wenyewe, waume zao hawana kitu.
Katika maisha ya sasa, hukatazwi kuishi kimatawi ya juu hasa kama fedha unayo au mumeo ana uwezo wa kukufanya uwe na jeuri. Tatizo linakuja kwa wale ambao kwanza wametokea kwenye familia duni na kwa bahati mbaya wakaolewa na wale wenzangu na mimi wenye fedha ya kubadilishia mboga tu halafu kwa kuiga wenzao wakajifanya nao ni matawi ya juu.
Eti wanaanza kuwasumbua waume zao kuwafanyia yale ambayo yako nje ya uwezo wao. Mbaya zaidi wakishindwa kutekelezewa kutokana na pochi kutoruhusu, wanaanza kununa na kufikia hatua ya kugoma kutoa haki ya ndoa.

Unanuna na kutompatiliza kimapenzi mumeo unadhani huyo mwenzako anazo anakufanyia makusudi kutokukupatilizia? Wewe ni shahidi kwamba hata pesa ya chakula au ada ya shule huwa inawasumbua, sasa leo iweje ufikie hatua ya kutaka kuvaa kila fasheni inayotoka na kufanyiwa mambo mengi yaliyo nje ya uwezo?
Iweje leo ung’ang’anie kupelekwa ‘out’ kwa kuwa eti mashosti zako huwa wanapelekwa viwanja na waume zao?
Ifike wakati tuishi kutokana na vile tulivyojaaliwa na Mungu. Kama fedha ipo si vibaya mkajitanua huku mkikumbuka kwamba kuna kesho pia lakini kama mambo ya fedha yamewakalia kushoto, kubaliana na hali hiyo na kamwe isiwe sababu ya kupunguza mapenzi kwa mumeo.
Kinachoniuma ni kwamba, wapo baadhi ya wanawake kwa ulimbukeni wao wamefikia hatua ya kuwasaliti waume zao kwa tamaa ya kupata pesa zitakazowafanya nao waonekane ni wanawake mbele za watu. Hii ni hatari na kama kweli unafikia hatua ya kuisaliti ndoa yako kwa sababu tu unasaka maisha ya kifahari, elewa maisha yako yatakuwa si marefu.
Kumbuka kubadili nguo, kwenda viwanja vya sterehe kila wikiendi na anasa nyingine havitakuwa na thamani yoyote kwako kama utakuwa hujampata mtu mwenye mapenzi ya dhati kwako.
Kikubwa siku zote omba kwa Mungu akupe mume anayekupenda, kukuheshimu, kukuthamini na kukujali kwa shida na raha kisha amani mengine yatakuja tu.
Kumbuka wapo ambao wanapata kila aina ya starehe kutokana na kuwa na uwezo wa fedha au kuolewa na wanaume wenye ‘pesa chafu’ lakini maisha yao hayana furaha na amani kwa kuwa hawapati penzi la dhati.
Niseme tu kwamba, kujikweza au kutafuta kuishi maisha ya juu wakati pesa haipo siyo poa, ishi kulingana na kipato chenu na si kulazimisha kutaka kuishi kama wanavyoishi mashosti zako ambao hata wanakopata fedha zao hukujui.
 Ni hayo tu kwa leo, tukutane wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

1 comment:

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake