ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, September 30, 2012

Kocha Yanga: Nawafahamu vizuri Simba, msihofu


Kocha mpya wa Yanga, Mholanzi Ernstus Wilhelmus Johannes Brandts akisaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo huku akishuhudiwa na Makamu Mwenyekiti wa Timu hiyo, Celemnt Sanga. Wilhelmus aliyewahi kuicheza timu ya taifa ya Uholanzi mwaka 1977 - 1985 amekuja kuziba nafasi ya kocha Tom Saintfiet aliyetimuliwa hivi karibuni

KOCHA mpya wa Yanga, Ernest Brandt amewataka mashabiki wa Yanga kutokuwa na wasiwasi na ujio wake hasa kwa mchezo wa watani Simba kwani anaifahamu vizuri soka ya timu hiyo.
Brandt aliyewasili juzi usiku kwa ndege ya Shirika la Ndege la Uholanzi, alilakiwa na viongozi mbalimbali wa Yanga na jana katika mkutano wake wa utambulisho, aliwatuliza mashabiki wa timu hiyo akiwaahidi ushindi.

Simba na Yanga zitakutana Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Taifa kuanzia saa 1:00 usiku katika mechi ya mzunguko wa tano wa Ligi Kuu.

Brandts alisema hayo mara baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja kuifunidsha timu hiyo mbele ya Waandishi wa Habari, Makao Makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam jana.
"Naifahamu Simba vizuri, nimeshaiona ikicheza, najua ni wapinzani wakubwa wa Yanga ina wachezaji wazuri. Naamini mchezo utakuwa mgumu, siwezi kuahidi ila tutajitaidi kuhakikisha tunashinda," alisema Brandts.
Brandts  ambaye amemaliza mkataba wake wa kuinoa timu ya APR ya Rwanda, anachukua nafasi ya Kocha raia wa Ubelgiji, Thomas Saintfiet aliyetimuliwa wiki moja iliyopita.
 Brandts akizungumzia hatua ya yeye kumwaga wino Jangwani wiki moja tu Saintfiet kutimuliwa, alisema: "Kocha kufukuzwa kwenya timu ni jambo la kawaida. Ukweli ni kwamba, hili siyo jambo jipya na hainishangazi hata kidogo."
Aliongeza: "Nashukuru uongozi wa Yanga kwa kuniamini na kunipa mkataba. Siwezi kutoa ahadi kubwa, lakini jambo la muhimu nitahakikisha wachezaji wangu wanafanya vizuri na kushinda mechi."
Alisema anajipanga kuipa klabu mafanikio mazuri kadri atakavyoweza lakini hilo pia likitegemea zaidi na ushirikiano kutoka kwa viongozi.
"Nilikuwa Uholanzi, nikapigiwa simu na viongozi wa Yanga kama niko tayari kuja kuifundisha timu yao. Kweli nilikuwa na ofa nyingi ila nilivutiwa na falsafa na  sera za klabu ya Yanga.
"Kama kocha, nataka kushinda kila mechi, nataka wachezaji wacheze soka la kuvutia, nataka kila mchezaji acheze  vizuri, na timu icheze vizuri, kwa sababu hakuna bora zaidi ya timu,î alisema.
Akizungumzia suala la nidhamu ndani ya klabu hiyo alisema: ìNidhamu ni muhimu kila sehemu kwenye michezo. Ukitaka kuamka saa moja kamili, fanya hivyo bila kupitiliza. KUjenga timu yenye nidhamu ni jambo muhimu, hata mimi wakati nacheza nilikuwa hivyo.
"Ni muhimu kujivunia timu unayochezea (Yanga). Nidhamu siyo tu unapokuwa kambini hata nje ya kambi. Nataka kuona nidhamu ndani na nje ya uwanja, mchezaji anapojituma juhudi zake zitaonekana na atapata mkataba mzuri zaidi hata kucheza nje ya nchi hata Ulaya,
 ìKesho kuna mechi na kuna mechi Jumatano, dhidi ya Simba itakuwa ngumu sana. Tutafanya kila tunaloweza kushinda. Yanga ni timu nzuri, nitajaribu kuiboresha najiona mwenye bahati kusaini mkataba na timu hii,î alisema.
Brandts alikuja mwaka jana na mwaka huu kwa ajili ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, akiwa na APR ya Rwanda na mara zote, Yanga iliibuka bingwa. Mwaka jana ikifundishwa na Mganda, Sam Timbe na mwaka huu ikifundishwa na Mbelgiji, Saintfiet.
Mwaka jana, APR ilitolewa mapema katika kundi lake Morogoro, lakini mwaka huu ilifika nusu fainali na kutolewa na Yanga. Ataiongoza Yanga leo katika mechi yake ya kwanza dhidi ya African Lyon.  
Mtaalamu huyo, alizaliwa Februari 3, mwaka 1956 mjini Nieuw-Dijk, Gelderland, mbali na PSV Eindhoven, alichezea pia Roda JC Kerkrade, MVV Maastricht na De Graafschap.
Brandts aliichezea mechi 28 timu ya taifa ya Uholanzi na kuifungia mabao matano na pia alicheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1978.
Brandts atakutana na wachezaji wake wa zamani wawili wanaocheza Yanga, beki Mbuyu Twite anayeanza msimu wa kwanza katika klabu hiyo na kiungo Haruna Niyonzima anayeingia msimu wa pili.

No comments: