Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na Naibu Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza anayeshughulikia masuali ya Jumuiya ya Madola bwana Mark Simmonds, katika ofisi za Wizara hiyo mjini London.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na maveterani wa Uingereza walipokutana mjini London jana tarehe 14/09/2012.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwa katika picha ya pamoja na maofisa wa ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza pamoja na baadhi ya maofisa wa SMZ mjini London.
LONDON 14/09/2012.
Na, Mwandishi Maalum, London
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema Zanzibar yenye muundo mpya wa serikali ya umoja wa kitaifa inafanya kazi zake vizuri na inakaribisha wawekezaji kutoka sehemu mbali mbali duniani kwa lengo la kukuza na kuendeleza uchumi wa nchi.
Amesema viongozi wa serikali hiyo kutoka vyama vya CCM na CUF wamekuwa wakishirikiana vyema na wananchi katika jitihada za kuendeleza umoja wa kitaifa ambao ulitokewa kwa kipindi kirefu.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo mjini London Uingereza, alipokuwa akijibu masuali mbali mbali kutoka kwa mabalozi wa nchi za Afrika pamoja na maveterani wa Uingereza, waliokutana kuzungumzia masuala mbali mbali yanayohusu maendeleo ya Zanzibar.
Katika masuala yao ya msingi, mabalozi na maveterani hao walitaka kujua juu ya mustakbali wa Zanzibar pamoja na maendeleo ya serikali ya umoja wa kitaifa iliyoundwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema licha ya changamoto ndogo ndogo zilizopo kutoka kwa baadhi ya viongozi na watendaji wa ngazi za chini, Serikali ya Umoja wa kitaifa imepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kurejesha umoja wa Wazanzibari pamoja na kuweka mazingira bora ya kuvutia wawekezaji.
Kabla ya mkutano huo wa mabalozi, Maalim Seif amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza anayeshughulikia masuali ya Jumuiya ya Madola bwana Mark Simmonds, katika ofisi za Wizara hiyo mjini London.
Katika hatua nyengine Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amekutana na baadhi ya viongozi wa Umoja wa Wazanzibari Wanaoishi Uingereza Zanzibar Walfare Association (ZAWA) na kubadilishana mawazo juu ya mambo mbali mbali yanayoihusu zanzibar ikiwa ni pamoja na kuimarisha idara ya Diaspora, ili iweze kuwa karibu zaidi na wazanzibari wanaoishi nchi za nje.
Viongozi wa jumuiya hiyo wametaja mafanikio mbali mbali yaliyopatikana ikiwa ni pamoja na kuanzisha asasi za kijamii nchii Uingereza ambazo zitawaunganisha wazanzibari wanaoishi nchini humo.
Jumuiya hiyo pia imeelezea nia yake ya kuleta maendeleo Zanzibar kupitia jitihada mbali mbali ikiwa ni pamoja na kujjipanga katika kusaidia vifaa na vitendea kazi zikiwemo kompyuta.
Kwa upande wake Maalim Seif aliwasisitiza Wazanzibari wanaoishi nchini Uingereza na kuwataka kuendeleza umoja na mshikamano wanapokuwa nje ya nchi, sambamba na kufikiria namna wanavyoweza kuisaidia nchi yao kimaendeleo.
Maalim Seif aliwasili nchini Uingereza tarehe 12 Septemba 2012, baada ya kumaliza ziara yake nchini Marekani, ambapo mara tu baada ya kuwasili alitembelea ofisi za ubalozi wa Tanzania mjini London kwa lengo la kusalimiana na wafanyakazi wa ubalozi huo.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake