MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali maombi ya Shirika
la Umeme Tanzania (Tanesco) kutaka isitishe utekelezaji wa malipo ya
Sh96 bilioni kwa Kampuni ya Kufua Umeme ya Dowans kutokana na kuvunja
mkataba wa kibiashara kinyume na sheria.
Kufuatia uamuzi huo,
Tanesco sasa inatakiwa kuilipa Dowans kiasi hicho cha fedha ambacho kwa
ujumla kinaliongezea shirika hilo mzigo wa madeni.
Tanesco
kupitia mawakili wake Rex Attorneys iliwasilisha mahakamani hapo maombi
mawili; kibali cha kukata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama hiyo
iliyotolewa Septemba 28, 2011 na kuomba kusimamishwa kwa utekelezwaji wa
hukumu hiyo.
Katika hukumu ya awali iliyotolewa na Jaji Emilian
Mushi, mahakama hiyo ilikubali maombi ya Tuzo kwa Dowans iliyotolewa na
Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC),
Novemba 15, 2010.
ICC iliamuru Tanesco kuilipa Dowans fidia ya Dola
za Marekani billion 65,812,630.03, kutokana na kuvunja mkataba wa
kibiashara kinyume cha sheria. Mahakama Kuu Tanzania ilikubaliana na
tuzo hiyo na kuipa kampuni hiyo nguvu ya kisheria.
Hata hivyo,
Tanesco haikuridhika na hukumu hiyo, badala yake ikawasilisha mahakamani
hapo taarifa ya kusudio la kukata rufaa kuipinga.
Jana, kwa
mara nyingine mahakama hiyo iliendelea kubariki Dowans kupewa tuzo hiyo
na kutupilia mbali maombi ya Tanesco, ikiwamo pingamizi la utekelezaji
wake.
Katika uamuzi wake aliousoma jana asubuhi, Jaji Dk Fauz Twaib
alikubaliana na hoja za Wakili wa Dowans, Kennedy Fungamtama kwamba
mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusimamisha utekelezaji wa malipo
hayo baada ya hukumu ya ICC.
Awali, wakili Fungamtama katika
hoja zake, alidai kuwa maombi hayo yamefunguliwa chini ya Kanuni ya 11
(2) na ya 47 ya Mahakama ya Rufani ya Tanzania ya mwaka 2009.
Alidai
kuwa kanuni hiyo ya 47 inatumika kwa maombi ambayo Mahakama ya Rufani
na Mahakama Kuu nchini zina mamlaka ya kisheria lakini, katika maombi
hayo ya Tanesco kusimamisha utekelezaji wa malipo hayo, mahakama kuu
haina mamlaka hayo.
Kwa mujibu wa Fungamtama, kanuni ya 11(2)
(b) ya kanuni za Mahakama ya Rufani za 2009, zinaihusu Mahakama ya
Rufani tu na kwa maana hiyo, ni Mahakama ya Rufaa pekee ndiyo inaweza
kusimamisha utekelezwaji wa malipo.
Hata hivyo, wakili wa Tanesco
aliyejitambulisha kwa jina la Mwandambo akijibu hoja za Wakili
Fungamtama alidai kuwa, kanuni hizo zinaipa nguvu mahakama hiyo
kusimamisha utekelezaji wa malipo iliyotolewa katika mahakama hiyo
ambazo zinakatikwa rufaa katika Mahakama ya Rufaa.
Lakini, Jaji
Dk Twaib alikubaliana na hoja za wakili Fungamtama kwamba kifungu cha
kanuni ambacho Tanesco ilikitumia katika maombi hayo, hakiipi mamlaka
Mahakama Kuu kusimamisha utekelezaji wa hukumu zake.
Jaji Dk Twaib
alisema kuwa, namna na masharti ya kusimamisha utekelezaji wa hukumu
yalivyoainishwa katika kifungu (d) cha kanuni hizo za Mahakama ya
Rufani.
Alisema kama Wakili Fungamtama alivyoeleza kwa usahihi,
kanuni hizo zinaihusu Mahakama ya Rufaa tu kama ilivyoainishwa vizuri
katika Kanuni ya 3 ya Kanuni za Mahakama ya Rufaa za mwaka 2009.
“Mheshimiwa
Jaji Mkuu anatambua msimamo wa kisheria uliowekwa katika maamuzi
mbalimbali kwa misingi kwamba, mchakato wa rufaa unapokuwa umeanza kwa
kuwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa, mahakama hii inakoma
kuwa na mamlaka ya kusimamisha utekelezaji wa hukumu,”, alisema Jaji.
Jaji Dk Twaib alisema mahakama hiyo inaweza kuwa na mamlaka hayo kabla kuwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa.
“Mara
tu taarifa ya kusudio la kukata rufaa inapokuwa imewasilishwa (kama
ilivyo katika kesi hii), Mahakama Kuu inakoma kuwa mamlaka,” alisisitiza
Jaji Dk Twaib na kuongeza:
“Kwa misingi iliyoelezwa mahakama
hii haina mamlaka ya kisheria kushughulikia maombi ya kusimamisha
utekelezaji yaliyowasilishwa na muombaji (Tanesco)”, alihitimisha uamuzi
wake Jaji Dk. Twaib.
Sakata lenyewe Mwaka juzi jopo la majaji
watatu wa ICC lilitoa uamuzi wa kuitaka Tanesco kuilipa Dowans Tuzo ya
Sh96 bilioni, kutokana na madai ya kuvunja mkataba wa kibiashara kinyume
cha sharia. Hata hivyo, uamuzi huo umekuwa ukipingwa na baadhi ya watu
wakisema Dowans ilirithi mkataba haramu wa Richmond hivyo, mkataba huo
haukuwa halali.
Tanesco nayo kwa upande wake, katika maombi yake
ilidai kuwa kama mchakato wa utekelezaji wa hukumu hiyo utaendelea,
itaathiri uwezo wake wa kuzalisha na kusambaza umeme nchini na hivyo
kusababisha tatizo kubwa la ukosefu wa umeme nchini na hivyo kuathiri
uchumi wa nchi kwa jumla.
Pia lilidai kuwa iwapo maombi yao
hayatakubaliwa itapata hasara kubwa na hivyo kuathiri kwa kiwango
kikubwa utendaji wake na hata kuleta wasiwasi wa kusimama kwa shughuli
zake za kila siku. Mawakili hao walisihi mahakama hiyo kuzingatia
maombi hayo kwa madai kuwa hasara itakayotokana na tatizo la ukosefu wa
umeme itakuwa ni kubwa na isiyoweza kufidiwa kwa namna yoyote ile.
Walidai
kuwa ingawa taarifa ya kusudio la kukata rufaa siyo kigezo cha kuzuia
utekelezaji huo, lakini kwa hoja za kesi yake ni nzito kiasi cha kutosha
kuifanya mahakama kutumia uwezo wake wa kisheria kuzingatia maombi
yao. “Mahakama ina uwezo wa kuamuru kusimama kwa utekelezaji huo kwa
namna itakavyoona inafaa.”, walisisitiza mawakili hao wa Tanesco katika
maombi hayo.
CHANZO GAZETI LA MWANANCHI
No comments:
Post a Comment