Miili mitatu ya wanajeshi wa Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waliokuwa katika misheni ya kulinda amani
katika jimbo la Darfur nchini Sudani, imeshawasili nchini.
Miili hiyo kutoka nchini humo iliwasili jana majira ya saa 4 asubuhi
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini
Dar es Salaam.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, mhariri mkuu wa jarida la Ulinzi,
linalochapishwa na JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, alisema kuwa baada
ya kuwasili miili hiyo itapelekwa katika kambi ya jeshi Lugalo kwa
ajili ya maandalizi ya kuiaga kwenda vijijini kwao leo kulingana na
taratibu zitakavyowekwa.
Kanali Mgawe aliyataja majina ya marehemu hao kuwa ni Sajinitaji Julius
Chacha Marasi, kutoka Shule ya Mafunzo ya Infantilia (SMI) iliyopo
Arusha; Koplo Yusuph Said Chingwile kutoka kikosi cha Lugalo na Praiveti
Anthony Danieli Paulo kutoka kikosi cha Lugalo.
Kwa mujibu wa Mgawe, wanajeshi hao na wenzao wanane wakiwa katika
shughuli za kulinda amani katika jimbo la Darfur, nchini Sudani, wakiwa
wamepanda gari linalojulikana kwa jina la Armould Personel Carrier
(APC), maalumu kwa shughuli za kijeshi, ghafla wakakumbwa na mto mkubwa
wa msimu uliokuwa umefurika ghafla.
“Kulikuwa na APC mbili, moja ikapita, wakati hii ya pili iko kwenye
uwanda huo, ghafla mto ukafurika na kulipindua gari lao lililokuwa na
wanajeshi nane na kisha kuzolewa. Kulikuwa na mvua inanyesha…kulingana
na baadhi ya maeneo katika jimbo hilo, barabara zinazotumika ndio mito
ya msimu inapita, ambapo ghafla wakashangaa mto umefurika na kuwazoa,”
alifafanua.
Alisema kuwa baada ya kutokea ajali hiyo, maiti mbili zilipatikana siku
hiyo hiyo zikiwa zimetupwa umbali wa meta 200, na moja ilipatikana baada
ya siku tatu ikiwa imeharibibika vibaya.
CHANZO NIPASHE
No comments:
Post a Comment