BAADHI YA MAITI ZILIZOFUKULIWA NDANI YA MGODI
Watu wanane ambao ni wachimbaji wadogo
wa madini katika Mgodi wa Chimbila (MNACHO) wilayani Ruangwa, mkoani
Lindi wakekufa baada ya kufunikwa na kifusi wakichimba madini.Habari zinasema kuwa tukio hilo lilitokea juzi alasiri katika mgodi huo ulioko kwenye kijiji cha Ndagala.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, George Mwakajinga, alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa 9:00 alasiri wakati watu hao wakichimba madini aina ya vito maarufu kwa jina la Change Colour katika mgodi huo unaomilikiwa na mtu aliyetajwa kwa jina la Mama Kidesi.
Kamanda Mwakajanga alisema kuwa mgodi huo ulikuwa na wachimbaji tisa, lakini muda mfupi kabla ajali hiyo kutokea, mchimbaji mmoja alikwenda dukani kununua sigara.
Kwa mujibu wa Kamanda Mwakajinga, baada ya mchimbaji huyo kurejea kwenye mgodi aliwakuta wenzake wakiwa wamefunikwa na kifusi na ndipo akaanza kupaza sauti kwa majirani kwa ajili ya kuomba msaada.
Alisema kuwa wachimbaji saba walifariki hapo hapo baada ya kuangukiwa na kifusi hicho na mmoja aliokolewa, lakini alifariki dunia wakati akipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Lindi kwa ajili ya kupata matibabu.
Akizungumzia mazingira ya tukio hilo, Mwakajanga alieleza kuwa sababu iliyosababisha wachimbaji hao kufunikwa na kifusi ni kutokana na mwamba wa mgodi huo kupasuka baada ya kulika na ndipo wakafukiwa ndani ya shimo hilo na kupoteza maisha.
Alisema kuwa mgodi huo haukuwa na leseni yoyote iliyoruhusu shughuli za uchimbaji madini kuendelea sehemu hiyo baada ya serikali kuufunga mwaka jana.
Hata hivyo, alisema licha ya kufungwa, baadhi ya wachimbaji waliendelea na shughuli za uchimbaji kinyemela.
Alieleza kuwa kufuatia tukio la juzi, serikali iliamua kuufunga mgodi huo na kuwekewa ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi ili kupisha uchunguzi kufanyika kuhusiana na tukio hilo sambamba na kumtafuta mmiliki wa mgodi huo ambaye hajulikani aliko.
“Mgodi umefungwa toka jana (juzi), ulinzi mkali umewekwa katika eneo hilo ili shughuli za uchunguzi zifanyike,” Kamanda Mwakajanga aliiambia NIPASHE kwa njia ya simu.
Kamanda Mwakajanga alisema kuwa baadhi ya maiti zimeanza kutambuliwa na ndugu, jamaa na marafiki na kufafanua kuwa kwa maiti ambazo hazijatambuliwa zimehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Lindi.
Alisema, majina ya marehemu hao hayakuweza kutambulika mapema kutokana na mgodi huo kutokuwa na kibali cha uchimbaji madini na kwamba wachimbaji hao walikuwa wanachimba kienyeji.
chanzo NIPASHE
No comments:
Post a Comment