ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 17, 2012

Mapenzi ni mchakamchaka, fedha ni dereva wa moyo-4

MPENZI msomaji wa safu hii, leo nitahitimisha makala haya ambayo yalikuwa mahususi kuelezea jinsi baadhi ya akina dada ambavyo wanawatenda wenzi wao kwa sababu ya tamaa ya fedha na siyo kuwapa mapenzi ya dhati.Tuwe pamoja...
Usiku mmoja akiwa amelala, Shadrack alikurupushwa na mlio wa SMS, aliposoma kumbe ilitoka kwa Shania akimtaarifu kwamba siku iliyofuata ndiyo ndoa yake. Shadrack alichanganyikiwa, akaja kugundua kwamba kumbe muda wote Shania alikuwa na mchumba lakini akawa anamdanganya.
Kilichomuumiza zaidi Shadrack ni jinsi mrembo huyo alivyomuandikia maneno mafupi. Kwani Shania wala hakuonesha kuguswa, hata kuomba msamaha japo wa kinafiki kwa kumpotezea mwenzake muda, hakufanya hivyo. Aliandika: “Tomorrow is my wedding.”
Usiku mzima Shadrack hakulala, maneno: “Tomorrow is my wedding.” Yalirudia kichwani na kuzidi kumuumiza. Alijiona mwanaume bwege kuliko maelezo. Maisha yake ya kimapenzi aliyaona yamejaa mkosi. Kila siku wa kutendwa ni yeye, tena anayemtenda ni mwanamke huyohuyo.
Siku iliyofuata alifanya kazi zake kwa kujivuta, hakuwa mzuri kiutendaji. Alishindwa kutekeleza mambo muhimu kwa ajili ya maisha yake. Muda wote alimfikiria Shania, kuna wakati alitamani kwenda kufanya fujo harusini lakini mwisho aliamua kuyaacha yapite. Akapiga moyo konde.
Akasahau machungu taratibu na akamudu kutojionesha mbele za watu ana machungu moyoni kwa sababu hata alipokuwa na Shania, alishajua kwamba ni mtu anayejali zaidi fedha kuliko mapenzi na utu. Japo alijiona yeye ni fungu la kukosa, taratibu akaacha kujitoa kasoro na kujiamini yeye mwanaume sahihi, ila mwanamke wake ndiye alikuwa mapepe.
Shadrack alianza uhusiano na mwanamke mwingine. Mwanzoni ilimsumbua, kwani alihisi naye atamtenda kama yule wa mwanzo. Hata hivyo, akawa mwangalifu zaidi, baada ya muda, akabaini kwamba huyo ni mwanamke anayeweza kukidhi mahitaji yake ya kimaisha, kwa hiyo akafunga naye ndoa.
Maisha ya Shadrack yakawa vizuri, mambo yakamyookea zaidi. Wakati upande wa pili, Shania hali ikawa siyo ile aliyoitarajia. Kumbe mwanaume aliyemuoa, ni mume wa mtu na hata hali ya kimaisha aliyokuwa anaoneshwa kabla, ilikuwa ni kiini macho. Kimsingi, mwanaume huyo alimkaanga kwelikweli.
Wakati Shania anaolewa, alifuta namba za simu za Shadrack. Alionesha wazi kwamba hamtaki tena, kwa maana alimpata mtu wa kutimiza matarajio yake ya kimaisha. Miezi saba baada ya ndoa, hakukuwa na mawasiliano kati yao. Kumbe, Shania alikuwa kwenye mateso kwa takriban miezi mitano.
Mpaka wakati huo, Shania aliweza kufurahia ndoa kwa miezi miwili tu. Baada ya hapo ilikuwa ni mateso makubwa, kwani aliweza kubaini kwamba mume wake ni mume wa mwanamke mwingine. Shania akawa mtu wa vilio kila kukicha. Ikabidi aende mahamakani kudai talaka.
Akakumbuka mbachao. Shadrack ndiye mbachao wake. Namba za simu hana, akatafuta marafiki wa Shadrack, wakampa namba za simu, kuanzia hapo ikawa usumbufu. Alipiga simu na kumuomba amsamehe kwa aliyomtendea na kumweleza alikuwa tayari hata kuwa mke wake wa pili lakini Shadrack alimwambia nafasi ilijaa hivyo Shania akaishia kulia na kusaga.

www.globalpublishers.info

No comments: