Thursday, September 13, 2012

Rage bingwa wa kudanganya

Kauli  kwamba Simba itajadili kujitoa kwenye Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara na kwenda kushiriki katika Ligi Kuu ya Zanzibar iliyotolewa na mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage juzi na kwamba ameitisha mkutano mkuu wa dharura jana, zimethibitisha kwamba kiongozi huyo anakurupuka katika anayoyasema na pia anawadanganya wanachama wa klabu hiyo.

Rage alitoa madai hayo wakati akielezea kutoridhishwa na maamuzi ya Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambaye naye ni mjumbe, ya kumuidhinisha beki wa zamani wa Simba, Kelvin Yondani kuichezea Yanga.



Katiba ya Simba inaeleza kuwa ili kuwepo na Mkutano Mkuu wa dharura ni theluthi mbili ya wanachama wa klabu hiyo wawe wamejiorodhesha majina yao kwenda kwa mwenyekiti na itakapothibitishwa uhalali wao mkutano huo utaitishwa ndani ya siku 45 na si ghafla kama alivyosema Rage juzi kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

Kauli aliyoitoa kwamba Simba inataka kufanya mkutano huo kwa nia ya kujadili kushiriki ama kutoshiriki ligi ya Bara na pengine kuhamia katika ligi kuu ya Zanzibar hilo ni jambo jingine lililodhihirisha kauli za kukurupuka za kiongozi huyo ambazo hazistahili kutolewa na kiongozi wa klabu ambaye ni lazima ajadiliane na wenzake kabla ya kutoa taarifa kwa kuwa Simba si mali yake binafsi.

Kutoshiriki ligi kuu ya Bara kunamanisha kwamba Simba itahitaji kulipa fidia ya mabilioni ya fedha kwa kukiuka mkataba wa udhamini binafsi kutoka Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yao ya Kilimanjaro Premium Lager, ambayo imezidhamini Simba na Yanga kwa mkataba wa zaidi ya Sh. bilioni 5 kwa miaka mitano.

Timu haiwezi kuhama ligi kama mpangaji anavyohama kutoka nyumba moja kwenda nyingine.
Simba italazimika kuonyesha kuwa ina  maskani yake yake visiwani Zanzibar kwenye maeneo kama Bububu, Rahaleo, Pemba, Mkunazini na kwingineko, na wala siyo kwenye makao yao ya sasa yaliyopo Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Baada ya kukamilisha hilo, Simba italazimika kusaka usajili ili kuhalalisha uwepo wake kisheria Zanzibar na katika Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) ambako kabla ya yote, itaangaliwa kama hakuna klabu ya soka yenye jina linalofanana na lao (Simba).

Super Falcon, kwa mfano, ikichukizwa na mwenendo wa Ligi Kuu ya Zanzibar, haiwezi kuhamia kirahisi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara bali italazimika kusaka usajili na baadaye kuanzia ligi za chini za TFF. 
Wakivuka kigingi cha usajili, Simba watalazimika kuanza kucheza ligi za chini hadi ije kufuzu kucheza Ligi Kuu ya Zanzibar, ambako udhamini wa pombe (kama kinywaji cha Kilimanjaro Premium Lager) haukubaliki.

Wachezaji wa Simba waliosajiliwa kwa fedha nyingi na wanaolipwa mishahara minono nao watadai fidia kwa kuwa hawakujiunga na timu hiyo ili kucheza ligi za chini.

Rage pia alizungumza na vyombo vya habari akiwa mkoani Dodoma na kusema anataka Yanga irejeshe fedha walizozitoa katika kumsajili Mbuyu Twite (Dola za Marekani 39,000) bila ya kuishirikisha Kamati ya Utendaji ya klabu yake ambayo yenyewe ilisisitiza kwamba haikuwa na nia ya kurudishiwa fedha bali walihitaji huduma ya mchezaji huyo.

Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM) aliwahi kutangaza kwamba ataileta klabu ya Birmingham City ya Uingereza lakini ziara ya timu hiyo iliyeyuka na baadaye alitamka kuingia mkataba na kampuni moja ya Uturuki kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa kisasa wa klabu hiyo ambao bado utekelezaji wake uko shakani.

Inakumbukwa kwamba Rage alisema ujenzi wa uwanja huo utagharimu Sh. bilioni 74,  lakini bila ya kusema fedha nyingi kiasi hicho zitapatikana wapi. Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam ulijengwa kwa Sh. bilioni 56 zilizopatikana kwa kiasi kikubwa kutokana na msaada wa serikali ya China. 

Rage aliudanganya mkutano mkuu wa wanachama wa Simba Agosti 5 mwaka huu kwamba mshambuliaji wao Emmanuel Okwi amefuzu kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Salzburg nchini Austria na kwamba Simba inatarajia kupata dola 600,000 (sawa na Sh. milioni 930), jambo ambalo halikuwa kweli baada ya Okwi kuiambia NIPASHE siku chache baadaye kwamba hakuwahi hata kujaribiwa na klabu hiyo kwavile alifika huko (Austria) akiwa anaumwa.

Mwenyekiti huyo pia alidai kwamba Yondani aliidhinishwa kuichezea Yanga baada ya wajumbe kupiga kura, jambo ambalo limekanushwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, Alex Mgongolwa, ambaye alisema hakuna kitu kama hicho katika kanuni na kwamba maamuzi yaliyofanywa yalizingatia kanuni, ibara ya 44(3) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na pia ibara ya 18(3) ya kanuni za uhamisho wa wachezaji za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Inakumbukwa kwamba Rage aliwahi kusema kwamba amemsajili mshambuliaji Kenneth Asamoah kutoka katika klabu ya Asante Kotoko ya Ghana na kwamba Yanga waliojidanganya kwamba wamemsajili Mghana huyo kutoka katika klabu ya FK Jagodina ya Serbia wamepotea "chaka".
Hata hivyo, baada ya Asamoah kutua Dar es Salaam na kuvishwa jezi ya Yanga yenye jina la Rage, mwenyekiti huyo wa Simba alisema alikuwa akitania tu watani zao.

Alisema pia wanaanzisha Simba TV lakini cha kushangaza televisheni yenyewe ilipangwa kuwa ndani ya televisheni nyingine na licha ya kuzindua vipindi vyao, hadi leo imekuwa kimya.

Wakati anachaguliwa kuiongoza Simba Mei 10, 2010, Rage alisema kwamba anataka kuona wachezaji wanaweka kambi kwenye jengo la klabu yao, wanakuwa na gym yao ya mazoezi, na kuahidi kufanya ukarabati wa jengo ndani ya siku 100 lakini kufikia sasa miaka miwili na miezi minne imepita (zaidi ya siku 850) jambo hilo halijatekelezwa na badala yake jengo la kwanza la klabu hiyo linaendelea kuchakaa wakati lingeweza kuwa ni kitega uchumi kikubwa. Kikubwa alichofanya ni kupaka rangi na kushughulikia tatizo la umeme. 

Wakati tunaenda mitamboni jana jioni, Kamati ya Utendaji ya Simba ilikuwa imekutana kwenye hoteli ya Movenpick jijini Dar es Salaam kujadili ajenda ya kujitoa ama kushiriki Ligi Kuu ya Bara.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake