Friday, September 14, 2012

Tatizo si ndoa, ila ndoa na nani? - 2

JAMBO kubwa la kujifunza katika mada hii ni kuhusu umuhimu wa kumtambua mwenzi sahihi kabla ya kuingia kwenye ndoa. Rafiki zangu, ni imani yangu kwamba mtazamo wako utabadilika kwa kiasi kikubwa kupitia mada hii.
Huwezi kuteswa tena na mapenzi na uamuzi wako katika masuala ya uhusiano na mapenzi yatakuwa yenye nguvu na yaliyopimwa na mtu mwenye uwezo mzuri wa kufikiria.

Wiki iliyopita kuna mambo tuliyoanza kujifunza pamoja. Kama leo ndiyo kwanza unafungua ukurasa huu, nitakukumbusha; tuliona kuhusu mwenzi ambaye unatarajia kuwa naye kwenye ndoa kama ndiye yule uliyemtarajia kabla ya kukutana naye.
Je, ni kweli ni yule uliyekuwa ukimuota? Ana sifa zile ulizokuwa ukitarajia? Maana unaweza kukurupukia ndoa ili na wewe uonekane tu umeolewa au umeoa, lakini akawa si chaguo lako la ndani.
Matokeo yake ni kwamba, ndoa itakuwa iliyojaa migogoro kila kukicha. Hakutakuwa na amani na ni mwanzo wa mmoja wao kuwa msaliti. Hii ni kwa sababu mnakuwa mmeingia kwenye muunganiko usiyo sahihi. Muunganiko usiotarajiwa.
Kuna lingine tuliona; kasoro. Kila binadamu ana kasoro zake. Ukiwa makini kumchunguza mtu yeyote ambaye uko naye karibu ni rahisi sana kuona kasoro zake. Jambo kubwa na la msingi kwako kujiuliza ni kama kweli utaweza kuvumilia kasoro zake.
Naamini sasa nimekusogeza karibu kabisa na utakuwa tayari kuendelea na somo letu. Tuendelee kujifunza.

MWENYE MAPENZI HASA
 Sifa nyingine muhimu ya kumwangalia mwenzi anayefaa kuwa naye kwenye ndoa ni pamoja na yule mwenye mapenzi ya kweli hasa. Mapenzi ya kweli huonekana haraka sana. Penzi la dhati halijifichi. Hujitokeza hadharani, wakati mwingine bila hiyari.
Mwenye sifa hii ni msikivu (kwa wanaume na wanawake), muelewa na anayetoa kipaumbele kwa mwenzake. Kama anakupenda kwa dhati ni lazima akupe kipaumbele katika mambo yake.
Si msiri na hutoa nafasi kwa mwenzake kutoa mawazo yake katika mambo yanayomhusu. Hatua hii hutokana na namna anavyomuona mwenzake kama sehemu ya maisha yake. 

ISHARA ZA MPENZI ASIYEFAA
Unaweza kuwa na mpenzi na mkapanga mipango mbalimbali ya baadaye ikiwemo ndoa lakini akawa na kasoro kubwa zilizojificha. Wakati mwingine kasoro hizo unaweza kuziona lakini usijue kama ni kubwa na zinazoweza kuwa tatizo kubwa katika maisha yenu ya ndoa.
Mara nyingi kasoro za mwingine zinaweza kufichwa na mapenzi ya dhati yaliyopo ndani ya mtendwa. Mathalani wewe una mpenzi wako, kwa vile ndani yako kuna mapenzi ya dhati, mwenzako anaweza kuwa anakosea tena makosa makubwa sana, lakini ukajikuta unavumilia, kudharau au kupuuzia!
Zipo dalili nyingi za mpenzi asiyefaa, lakini hapa angalia zile za muhimu zaidi;
Usaliti; katika makosa makubwa kabisa kwenye uhusiano ni pamoja na kusaliti. Kama mwenzi wako anakusaliti na una ushahidi wa kutosha (kama umemfumania) ni dalili mbaya kwenye ndoa.
Kiburi/dharau; hii nayo ni dalili mbaya. Mwenzi mwenye dharau na kiburi hawezi kuwa sahihi, maana huko ndani ya nyumba kutakuwa ni majibizano yasiyo na maana. Mwenzi sahihi anapaswa kuwa msikivu, mwenye kupima kila kinachotoka kwenye ulimi wake.
Kipigo; tabia hii zaidi ipo kwa wanaume. Kosa dogo tu anamwangushia mwenzake kipigo. Kupigana si mapenzi marafiki zangu. Kama bado mpo kwenye uchumba tu, kosa dogo kipigo, vipi mkiingia kwenye ndoa? Tafakari jambo hili utaona ni kasoro kubwa sana.
Mbinafsi; hili ni tatizo lingine. Kama mnahitaji kuwa katika muunganiko wa ndoa, ubinafsi ni sumu kabisa. Mwenzi mwenye  tabia ya lake linakuwa lake mwenyewe na lako lenu hafai kwenye ndoa. 
Asiyejitoa; hili nalo ni tatizo. Unaweza kuwa na tatizo kubwa kabisa na kwa kulitazama unaamini kabisa kwamba mwenzako anaweza kukusaidia, lakini hataki tu. Mathalani unaumwa, anaweza kushindwa hata kufika kukujulia hali tu. Hata kama unampenda kwa kiwango gani, huyu hafai kabisa kuwa nawe kwenye ndoa.

Wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani. 

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake