
Mkurugenzi Mtendaji, William Mhando aliyesimamishwa kazi Julai 15 mwaka huu.
BODI ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa siku mbili mfululizo limeshindwa kutangaza hatma ya Mkurugenzi Mtendaji, William Mhando aliyesimamishwa kazi Julai 15 mwaka huu.
Taarifa za ndani zilieleza kwamba Bodi ya shirika hilo, ilikwishatoa uamuzi kuhusu hatua zilizochukuliwa dhidi ya Mhando na kwamba katika mkutano huo ungetangazwa uamuzi uliochukuliwa na bodi.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud kuitisha mkutano na waandishi wa habari juzi saa 11.00 jioni.
Hata hivyo licha ya waandishi kukaa katika ofisi hizo kwa saa nne, Badra aliwatangazia kwamba mkutano huo sasa ungefanyika jana saa 4.00 asubuhi katika ofisi hizo kwa sababu sahihi muhimu katika taarifa hiyo ilikuwa imekosekana.
Jana saa 4.00 waandishi hao wakafika katika ofisi hizo kwa ajili ya mkutano huo, lakini walipofika mapokezi walielekezwa kwenda katika ofisi za Wizara ya Nishati na Madini.
“Nimeelekezwa kwamba niwaeleze waandishi wa habari kwamba mkutano wao umehamishiwa wizarani, hivyo mnatakiwa kwenda huko,” alisema mmoja wa wafanyakazi wa mapokezi.
Baada ya kupata ujumbe huo kutoka kwa Badra, waandishi walianza safari ya kwenda wizarani.
Hata hivyo walipofika wizarani, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara ya Nishati na Madini, Fadhil Kilewo alisema hana taarifa na kuwapo kwa mkutano na waandishi wa habari wizarani hapo.
“Mimi ndiye huitisha mikutano na waandishi wa habari, lakini kwa leo sina taarifa zozote za Tanesco ama wizara kuwa na mkutano, hivyo hakuna mkutano,” alisema Kilewo akiwa amezungukwa na waandishi.
Bodi ya wakurugenzi wa Tanesco ilimsimamisha kazi Mhando kwa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Mbali na Mhando, pia iliwasimamisha kazi wafanyakazi wengine watatu ambao ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji , Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Ununuzi, Harun Mattambo.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment