Viongozi waliofikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali saa 4 za asubuhi huku mahakama hiyo ikiwa tupu haina watu baada ya Jeshi la Polisi kuwaondoa wafuasi wa viongozi hao na kutaka warudi nyumbani.
Washitakiwa wengine ni Sheikh Mselem Ali Mselem (52)mkaazi wa Kwamtipura, Sheikh Azzan Khalid Hamdan(43), mkaazi wa Mfenesini, Sheikh Mussa Juma Issa (37),mkaazi wa Makadara, Sheikh Suleiman Juma Suleiman mkaazi wa Makadara, Sheikh Khamis Ali Suleiman (59), mkaazi wa Mwanakwerekwe, na Sheikh Hassan Bakari Suleiman (39) mkaazi wa Tomondo wote
kutoka Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Kesi ya washitakiwa hao iliendeshwa na mawakili saba, watatu wakiwa wa Serikali na wanne kutoka upande wa washitakiwa, ambapo kesi hiyo ilichukuwa muda wa saa tatu hadi kumalizika kwake huku ulinzi nje ya mahakama ukiwa umeimarishwa zaidi.
Mawakili kutoka serikalini waliongozwa na Maulid Ame Mohammed, Ramadhan Ali Abdallah na Khamis Jaffar Mfaume.
Huku upande wa mawakili wa washitakiwa walikuwa Rajab Abdallah Suleiman, Suleiman Salum na Abdallah Juma Mohammed ambaye alikuja kumuwakilisha Salim Taufik ambaye alitoa dharura ya kufiwa ambapo yupo safarini nchini Nairobi.
Akiwasomea mashataka hayo Wakili wa Serikali, Mohammed Ame alidai kuwa washitakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 45 (1) (a) na (b) cha sheria namba 6 mwaka 2004 sheria ya Zanzibar.
Alidai mahakamani hapo mnamo Agosti 17 mwaka huu, majira ya saa 11 za jioni eneo la Magogoni Msumbiji katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja wakiwa wahadhiri kutoka Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar washitakiwa hao walitoa matamshi ya lugha ya uchochezi yanayoashiria uvunjifu wa amani na kusababisha fujo, maafa mbali mbali na mtafaruku kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Washitakiwa hao ambao walisomewa shitaka lao kwa pamoja mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Ame Msaraka Pinja walipotakiwa kujibu tuhuma yao hiyo mmoja mmoja ambapo wote walikana kutenda kosa hilo.
Awali wakili wa washitakiwa hao, Abdallah Juma alimuomba hakimu kuwapatia hati ya mashtaka pamoja na kuwapa dhamana wateja wake kwa masharti nafuu.
Kwa upande wa Wakili wa Serikali alidai kuwa upelelezi wa kosa hilo bado haujakamilika na kuiomba mahakama kutoa muda zaidi wa kukamilisha taratibu pamoja na kuiomba kupanga tarehe nyengine ya kesi hiyo kwa kutajwa.
Hata hivyo, Juma aliiomba mahakama hiyo kutoa dhamana kwa washitakiwa hao kulingana na mazingira ya kesi yenyewe ambapo kwa upande wa Hakimu alisema kuwa baada ya kupitia hoja za pande zote mbili mahakama imeona ni vyema isikurupuke kutoa dhamana na kupanga tarehe nyingine ambayo ndio itakayoweza kukaa na kutoa maamuzi juu ya
suala la dhamana.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi keshokutwa kwa kutolewa maamuzi ya dhamana iwapo washitakiwa watapewa dhamana.
Baada ya washitakiwa kusomewa shitaka lao kulitokea mvutano kwa pande mbili za mawakili ambapo upande wa wakili wa washtakiwa ulitoa malalamiko ya kutokuwepo kwa kibali kinachomruhusu hakimu kuendesha kesi hiyo kisheria kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP), jambo ambalo
lilipatiwa jibu lake na kesi hiyo kuendelea kama kawaida.
1 comment:
mbona hujaweka wahusika tuwaone walivyo kamatwa
Post a Comment