
Kuna mengi tulijifunza wiki iliyopita, lakini kikubwa tulianza kuangalia namna bora zaidi ya kuishi na staa. Jambo la kwanza tuliona kuhusu wivu. Kimsingi hupaswi kuwa na wivu sana unapokuwa katika uhusiano na staa. Sasa tuendelee na vipengele vingine.
MJULIE
Msome taratibu mpenzi wako, chunguza vitu anavyopenda, ukivijua hatakusumbua! Fahamu aina ya mavazi anayopendelea, chakula na hata burudani.
Kwa mfano umetoka naye, inawezekana hajavutiwa na wewe kwa asilimia mia moja na mavazi yako, lakini atatumia muda mwingi kuwasifia wengine jinsi walivyopendeza. Jifunzie hapo na uchukue hatua.
ISHI KAMA YEYE
Kwakuwa tayari umeshaingia katika uhusiano na staa, lazima na wewe ujitahidi kwenda sawa na mazingira. Ishi kistaa kwa kila kitu kuanzia mavazi, uzungumzaji wako, muonekano n.k
Mara nyingi mastaa ni watu wanaojulikana na kuheshimiwa sana, ili kuepuka aibu, huwa hawapendi sana kuchangia vitu ambavyo hawana uhakika navyo.
Ni watu wa kiasi kwa kila kitu, hawazoeleki haraka n.k, sasa na wewe lazima ufuate utaratibu huu ili uweze kwenda sawa na mpenzi wako.
MASTAA WANAWEZA KUWA WAPENZI?
Hili ni swali ambalo linawaumiza wengi vichwa. Jibu ni jepesi sana, lakini lenye viambatanisho mbele yake. Ndiyo! Staa anaweza kuwa na uhusiano na staa mwenzake lakini kuwepo na mambo makubwa manne; mapenzi ya dhati, kuheshimiana, kuchukuliana na kila mmoja kuthamini uwepo wa mwenzake.
Kama mkipendana kwa dhati, huwezi kujisikia, kudharau, kiburi, jeuri na tabia nyingine mbaya. Kama unampenda lazima utakuwa na hofu ya kuachwa. Penzi la dhati limebebwa pia na heshima.
Lazima umchukulie mpenzi wako kulingana na udhaifu wake, lakini kubwa zaidi ni kule kuthamini uwepo wa mwenzako. Ni kweli mastaa wanafahamiana na wengi na wanapenda sana kuishi maisha fulani ya ‘Kizungu’, lakini ni vyema ukajua kuwa wakati ukifanya jambo fulani, yupo ambaye anakupenda, anakuona!
VIPI KWA STAA NA ASIYE STAA?
Kama nilivyosema mwanzoni, baadhi ya mastaa wanaathiriwa na ustaa wao, kujiamini kupiliza, kutothamini penzi n.k, ni mambo yanayoweza kuharibu uhusiano na kuweka historia ya kuwa na wenzi wengi.
Hata hivyo, kama penzi la kweli lipo miongoni mwao, basi penzi linaweza kudumu. Pamoja na yote hayo, yapo mambo ambayo staa anatakiwa kuyafuata ili aweze kuishi na mpenzi wake ambaye si maarufu. Hebu tuone...
ONESHA MAPENZI ZAIDI
Inawezekana mwenzi wako naye amekuwa na wewe kwasababu tu anakupenda, lakini hana imani kama penzi lenu litadumu akihofia ustaa wako, ondoa hiyo dhana haraka sana kichwani mwake.
Jambo hili litawezekana kwa wewe kuonyesha penzi lako la dhati kwa ujumla wake. Hapa siwezi kufafanua zaidi, lakini fahamu kwamba unatakiwa kumfanya aone kwamba kweli unampenda na huna mpango wa kuachana naye.
ELEZA MAZINGIRA YAKO YA KAZI
Wakati mwingine mazingira ya kazi yako yanaweza kukuweka karibu na watu wenye jinsia tofauti na yako, mathalani wewe ni mcheza shoo, mwanamuziki, mwigizaji n.k, mweleze mpenzi wako wazi kuhusu ukaribu huo wa kikazi na afahamu kabisa kwamba ukaribu huo ni wa kikazi tu!
Ukifanya hivyo, atakuwa huru na wewe. Atazidi kukupenda hasa kutokana na ukweli kwamba, umekuwa mkweli kwake.
MPE NAFASI
Ili aone penzi lako ni la dhati, unatakiwa kumpa nafasi ya kuonesha mapenzi yake. Hata kama ni kwenye matembezi au kwenye halaiki ya watu. Mpe uhuru na wewe.
Hata katika mambo binafsi na yale yanayohusu maisha, mpe nafasi akushauri, acha akupangie mavazi na hata namna ya ufanyaji wako kazi. Ukimpa nafasi atakuwa na amani zaidi na atazidisha penzi lake maradufu.
WEKA USTAA WAKO PEMBENI
Hata kama unajulikana na dunia nzima, katika mapenzi hakuna ustaa. Mnyenyekee mpenzi wako, mpe nafasi ya kwanza, mfanye azidi kukuamini. Msikilize kwa kila jambo, kama unaona anakosea, mweleweshe kwa upole, usitumie lugha ya ukali.
Kuuweka ustaa wako pembeni na kuwa ‘busy’ kuhakikisha penzi lako linakuwa la kudumu kutazidi kutakupa nafasi nzuri zaidi katika moyo wa mwenzi wako. Hapo sasa utaona ladha ya penzi la dhati.
Haki ya kupenda ni ya kila mtu, itumie haki hiyo vizuri huku ukihakikisha maisha yako yanakuwa ya furaha siku zote na mwenzi wako akifurahia kuwepo kwa penzi lenu. Wengi wanaamini mastaa hawawezi kudumu kwenye uhusiano, lakini sasa naamini utakwenda kubadilisha mtazamo huu kwa wewe mwenyewe kuwa mfano.
Naamini nimeeleweka vyema. Ahsante sana kwa kunisoma. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine kali, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers, ameandika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.
No comments:
Post a Comment