ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 19, 2012

Serikali yatangaza baa la njaa


Venance George, Morogoro                    
SERIKALI imesema kuwa hali ya upatikanaji wa chakula nchini kwa sasa ni mbaya kutokana na maeneo mengi ya nchi kukabiliwa na ukame na upungufu mkubwa wa chakula uliosababisha kupanda ghafla kwa bei ya mazao mbalimbali ya nafaka likiwemo zao la mahindi.

Akizungumza na wajumbe wa bodi ya tumbaku nchini (TTB) juzi usiku mjini hapa akiwa njiani akitokea katika mikoa ya Njombe, Mbeya na Iringa kukagua hali ya chakula katika mikoa hiyo, Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adamu Malima, alisema hali ya chakula ni mbaya sana na Hifadhi ya Taifa ya Chakula haina chakula cha kutosha kwa sasa.

Malima alisema kuwa mbali ya kwenda kutathimini hali ya upatikanaji wa chakula katika mikoa hiyo ambayo ni miongoni mwa mikoa minane nchini inayozalisha chakula kwa wingi nchini, ziara yake hiyo pia ilikuwa ni kuweka uratatibu wa Serikali kununua chakula kwa ajili ya hifadhi ya taifa.

Naibu waziri huyo alisema kuwa mwaka jana mpaka kufikia mwezi Oktoba chakula kilichozalishwa katika mikoa hiyo kilifikia wastani wa tani 25 milioni wakati uwezo wa kuzalisha mahindi katika mikoa hiyo ni tani 22 milioni hata hivyo uzalishaji wa mwaka huu umekuwa chini ya matarajio.

Malima alisisitiza kuwa bei ya mahindi kwa kipindi cha mwaka jana ilikuwa ni Sh350 kwa kilo moja na Serikali ilinunua mahindi kwa bei hiyo kwa ajili ya hifadhi ya taifa, lakini bei ya mwaka huu imepanda zaidi kutokana na kiwango cha mahindi kuwa kidogo huku mahitaji yakizidi kuongezeka.
                                                                                                                                                                                                                       “Leo (juzi) nimetangaza bei mpya ya ununuzi wa mahindi katika hifadhi ya taifa ya chakula mpaka kufikia Sh500 kwa kilo moja, kupanda kwa bei hiyo kumetokana na walanguzi kununua mahindi ya wakulima kwa bei ya Sh380 wakati huo Serikali ikinunua kwa Sh350, hivyo kuifanya Serikali kukosa mahindi ya kununua kwa ajili ya hifadhi ya taifa,” alisema naibu waziri huyo.


Malima alisema kuwa pamoja na Serikali kuongeza bei ya kununulia mazao hayo, upatikanaji wa mahindi umekuwa ni mdogo kufuatia wakulima wengi kutokuwa na bidhaa hiyo kwa sasa.

Alisema kuwa mwaka huu kuna hatari taifa kukabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula kutokana na hali hiyo hivyo kushauri wakulima kuhifadhi chakula kidogo kilichopo na kukitumia kwa uangaliwa kukwepa kukabiliwa na njaa.

Kuhusu zao la tumbaku, Malima alisema kuwa zao la tumbaku limeendelea kuwa zao la kutegemewa katika mapato ya Serikali kwa mazao kilimo baada ya mazao ya mbogamboga na maua ambayo yamekuwa yakiingiza pato kubwa zaidi.

Malima aliishauri bodi ya tumbaku kuongeza jitihada katika kukidhi matarajio ya kuhakikisha inainua ubora wa zao hilo nchini na kuanzisha mfuko wa bodi utakaosaidia kukabiliana na changamoto nyingi zinazoikabili bodi hiyo.

Alisema kuwa ikiwa bodi itafanikiwa kunzisha mfuko huo na ukawa na usimamizi madhubuti utawezesha kumaliza changamoto nyingi zinazoikabili bodi ikiwa ni pamoja na ufinyu wa bajeti inayotolewa na Serikali kuiwezesha bodi hiyo.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa bodi hiyo, Wilfred Mushi alitoa maelezo mbele ya naibu waziri huyo juu ya utendaji kazi wa bodi na changamoto zinazoikabili, alisema kuwa kwa sasa bodi imeweka mikakati ya miaka mitano ambapo mikakati hiyo ikitekelezwa kikamilifu uzalishaji na tija ya zao hilo itaongezeka.

Mushi alidai kuwa ikiwa Serikali katika masuala iliyoombwa kuiwezesha bodi yatatekezwa kutaliwezesha zao hilo kuiingizia serikali wastani wa dola178 milioni za Marekeni kutoka Dola109 milioni zinazokusanywa kwa sasa kama kodi ya Serikali.
Hata hivyo, bodi hiyo imetakiwa kufanyia kazi malalamiko ya chinichini inayotolewa na baadhi ya wananchi na wadau wakidai kuwa bodi imeegemea upande wa wakulima wakubwa na wafanyabishara na kusahau makundi mengine kwa kuitisha mikutano ya makundi yote, bodi, wafanyabishara, wakulima na wadau wengine.

No comments: