ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 19, 2012

Upe uhuru moyo wako ufurahie mapenzi

KAMA ada tumekutana kwenye kona yetu, nimeendelea kupata pongezi na maswali mengi kulingana na mada za kila siku ninazozitoa baada ya kuwagusa watu, kwa kifupi nasema asanteni.

Leo nazungumzia uhuru wa moyo katika mapenzi.Kwanza nifafanue kuwa, Uhuru wa moyo ni kufuta dhana potofu za kufikiria mpenzi wako akiwa mbali nawe lazima atakuwa anakusaliti au kwa maana nyingine ni ile hali ya kuweka suala moyoni kwa muda mrefu, japo mlimalizana, lakini mkikosana lazima kosa la awali uliseme na kuwa kama wimbo wa taifa.

Kuamini mwenzako kila kosa analofanya huwa amedhamiria na kuwa hana bahati mbaya. Kuwa mbinafsi kwa kuamini katika mapenzi yenu, wewe ndiye unayeumizwa sana na kuona mwenzako huwa hapati maumivu ya moyo, makosa yako bahati mbaya ya mwenzako makusudi.
Nina imani nimeeleweka vizuri, lakini ili uweze kufahamu kinagaubaga, twende pamoja:
Dhana potofu:
Watu wa aina hii huamini kabisa mwenzake hana lolote analowaza juu ya maisha au kimaendeleo zaidi ya kuwaza usaliti. Binadamu hawa nimewaelezea sana kwenye mada ya wiki iliyopita.
Watapataje uhuru wa moyo wao? Jibu ni rahisi tu, kwa kuwaamini wapenzi wao.
Unapaswa uelewe kuwa, upo ndani ya penzi kwa sababu kabla hujaingia ulichunguza tabia ya mwenzako na kuamini ni sahihi kwako, siku zote penzi usiloliamini usiingie.
Hajawahi kukufanyia kosa lolote lakini kwa vile ni mzuri au mtanashati unaamini lazima atakuwa na mtu mwingine zaidi yako. Hivyo si sahihi kabisa.
Hizo ni hisia potofu, siku zote uaminifu wa mtu hauji kwa kumlinda kama polisi na kibaka, bali huja kwa kuaminiana huku kila mmoja akijiaminisha kwa mwenzake kwa kuwa hakuna kiumbe kinachowaza ujinga kila wakati.
Kuweka jambo moyoni kwa muda mrefu:
Watu wa aina hii huamini wao siku zote wapo sahihi ila wenzao hawako sahihi, makosa yao huwa bahati mbaya lakini kwa wenzao huona wamedhamiria, hupenda kusamehewa kuliko kusamehe.
Linapotokea tatizo ambalo lilimuumiza au hata kumuudhi, basi huwa halitoki moyoni japo huwa anasema amekusamehe lakini moyoni huwa na donge zito ambalo humtesa na kuufanya moyo wake ukose uhuru, kila anapolikumbuka kosa la zamani, maumivu huanza upya.
Ili kuupa uhuru moyo wako, amini kabisa mwanadamu ameumbwa kwa udhaifu, pia makosa ni sehemu ya mchezo wa maisha. Mtu anapokosa na kukuomba msamaha na ukakubali kumsamehe, basi hakikisha msamaha wako unatoka moyoni na si mdomoni ili kuufanya moyo wako uwaze kitu kipya na kuwa huru.
Ubinafsi:
Watu wa aina hii huamini kabisa wao ndiyo wenye haki ya kutenda kosa na kusamehewa lakini huwa hawaangalii upande wa pili nao unahitaji faraja kama wanavyohitaji wao.
Hawapendi kulaumiwa wanapofanya kosa lakini inapotokea hivyo kwa wenzi wao hushadadia jambo hata lisilo na maana kwa vile huamini wapo sawa, pia watu wa aina hii hupelekwa na hisia zao ambazo huwa tofauti na ukweli.
Ili kuupa moyo wako furaha, amini maumivu unayoyapata wewe hata mwenzako naye huyapata hivyohivyo.
Usiwe na uamuzi wa haraka, mpe nafasi mwenzako hata kama kafanya kosa msikilize kisha toa uamuzi. Kubali kukosolewa ili kurudi kwenye mstari kwa vile kioo chako ni mwenzako, si wewe mwenyewe.
Ukitambua yote haya, nina imani moyo wako utakuwa na uhuru na kukufanya ufurahie penzi lako.
Kwa haya machache tukutane wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

No comments: