ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 25, 2012

USIKUMBUKE MAZURI YAKE, USISONONEKE, MWACHE AENDE ZAKE

WALIO katika mapenzi matamu watakubaliana na mimi kuwa, uhusiano wenye amani na kusikilizana ndiyo kitu ambacho kila mmoja wetu anakihitaji na ikiwa hivyo unaweza ukajikuta unanawiri tu!
Wakati mwingine unaweza hata kujikuta hujala chochote lakini ukajihisi umeshiba eti kwa sababu tu umemuona mpenzi wako au kuwa naye karibu tu, yaani yeye kwako ndiyo mambo yote, yeye ndiyo kila kitu kwenye maisha yako. Huo ndiyo utamu wa maisha.
Naamini kabisa wapo ambao wako katika aina hiyo ya mapenzi. Hao wanatakiwa kumshukuru Mungu kwa kuwaweka katika mazingira hayo.

Lakini sasa wakati wengine wakiishi kwa raha katika maisha yao ya kimapenzi, wapo wengine wanaoishi na wapenzi wao huku mioyo yao ikiwa imesinyaa, yaani hawana furaha kabisa!
Kwao kila siku ni karaha na vituko vya makusudi kutoka kwa wapenzi wao licha ya kwamba wanawapenda sana na kuonesha mapenzi yao yote.
Kila siku kwao ni ya maumivu na simanzi ya moyo isiyojulikana mwisho wake. Hii inauma sana na kwa kweli walio katika sampuli hii ya mapenzi, wanajuta kukutana na wapenzi walionao.
Cha ajabu sasa, licha ya baadhi ya watu kutokuwa na furaha kabisa katika maisha yao ya kimapenzi eti wanahisi njia sahihi ni kuvumilia huku wakiamini siku moja mambo yatabadilika.
Jamani, huenda nikawa na msimamo tofauti kidogo kwani mimi naamini mapenzi ya kweli ni pamoja na kumsikiliza mwenzio na kuheshimu hisia zake, hasa katika mambo yanayofaa.
Tofauti na hapo, tabia ya kutokuwa msikivu, kutojali na kutokuwa mwepesi kubadilika ni dalili tosha ya kutokuwepo kwa upendo wa dhati. Mapenzi, nijuavyo mimi ni kupenda, kupendwa, kusikilizana, kupatilizwa na kuheshimiana na si kinyume!
Wakati mwingine unaweza kujikuta katika wakati mgumu wa kuamua hatima ya uhusiano wako na mpenzio kwa kuwa unahisi unampenda sana na kwamba hauko tayari kumkosa.
Ukweli ni kwamba, hata kama huyo uliyenaye unampenda vipi, lakini kama anaonesha kubadilika na kutokupa ile furaha uliyoitarajia, huna sababu ya kumng’ang’ania. Mwache aende zake kwani huenda kuendelea kuwa naye ndiyo kuyafupisha maisha yako.
Inawezekana kuna mambo mazuri ambayo amekuwa akikufanyia huko nyuma kiasi kwamba ukikumbuka unasita kufanya uamuzi wa kumtosa. Sikiliza nikuambie kitu, unapokutana na hali hiyo, elewa ni shetani ambaye anataka kukufanya uendelee kuwa kwenye utumwa wa mapenzi.
Pata ujasiri, yaliyopita katika uhusiano wako, yafanye kuwa historia kisha fanya uamuzi sahihi.
Amini ulifanya uamuzi usio sahihi wa kuingia kwenye uhusiano na mtu huyo anayekufanya ulie kila siku na kujiona kama vile uko ‘singo’ kisha fanya uamuzi sahihi wa kumweka pembeni.
Hiyo itatoa nafasi kwa yule mwenye mapenzi ya kweli na wewe, mwenye kila kigezo unachokitaka kupiga hodi kwenye moyo wako na hatimaye kujikuta unayafurahia maisha yako.

Ni hayo tu kwa leo.

www.globalpublishers.info

No comments: