Chama cha Mapinduzi (CCM) visiwani Zanzibar kimeitaka Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuunda tume maalum kuchunguza viongozi na watendaji wanaotuhumiwa kuhusika na uporaji wa ardhi na mali za serikali wakati wa uongozi wa Rais Mstaafu Amani Abeid Karume.
Tamko hilo limetolewa na Mwenyekiti mpya wa CCM mkoa wa Mjini Magharibi, Burafia Silima, wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja Amani kwa Mabata Kisiwani.
Alisema kuna ufisadi wa kutisha wa ardhi na mali za serikali yakiwamo majengo ulifanyika Zanzibar na wahusika lazima wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Alisema kwa tume itasadia kupata ukweli kuhusu viongozi waliohusika kupora ardhi ikiwamo ya wakulima na kusababisha migogoro.
Alisema kumekuwepo na malalamiko mengi ya wananchi kunyaganywa ardhi na baadhi ya viongozi na watendaji ambayo walipewa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar kwa shughuli za kilimo baada ya mapinduzi ya mwaka 1964.
Kuhusu sekta ya biashara, alisema kwamba kuna biashara chafu ya magendo ya mafuta ya kula na petroli ambayo imekuwa ikifanywa na baadhi ya wafanyabiashara na kuikosesha serikali mapato kila mwaka.
Alisema wakati umefika serikali kuunda tume maalum ya kuchunguza mwenendo wa biashara ya mafuta kutokana na vitendo hivyo kuathiri vyanzo vya mapato ya serikali.
Kuhusu vurugu za Uamsho, Burafia alisema vitendo vinavyofanywa na wafuasi wa kikundi hicho vina baraka za baadhi ya viongozi wa kisiasa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Aliwataka wananchi kuwa makini na kampeni za Uamsho za kutaka Zanzibar kujitenga katika Muungano kutokana na mpango huo kuwa na athari kubwa za kisiasa na kiuchumi pamoja na kuvuruga amani na umoja wa kitaifa.
Mapema Katibu CCM Wilaya ya Dimani Yahya Saleh alisema kwamba wakati umefika kwa serikali kufuta usajili wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara Kislamu Zanzibar (Jumiki) baada ya kuacha kufanya shughuli za kiroho na kufanya kazi za kisiasa kinyume na sheria.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment