ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, November 17, 2012

Dk. Bilal: Wenye ‘vijisenti’ ng’ambo watashughulikiwa bila kujali vyeo vyao


Makamu wa Rais Dk. Mohamed  Bilal, amesema watuhumiwa  walioficha fedha nje kinyume cha sheria  watachukuliwa hatua  bila kujali nafasi wala nyadhifa  zao na kwamba suala hilo litawekwa wazi.

Kadhalika amejitetea kuwa yeye si mmoja wa  viongozi walioficha fedha ng’ambo.

Dk. Bilal alilazimika kusema hayo, kufuatia swali lililoulizwa na mmoja wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA),  katika Mhadhara wa 13 wa Kumbukumbu  ya Waziri Mkuu wa zamani, hayati Edward Moringe Sokoine uliofanyika katika kampasi ya Solomoni Mahlangu mjini hapa.


Katika swali lake mwanachuo John Robart alitaka kujua ni hatua gani serikali imewachukulia viongozi waliotajwa kuficha fedha nje  ikiwa ni sehemu ya kumuenzi hayati Sokoine.

Alisema Sokoine  alikuwa mwadilifu na aliyekemea rushwa katika ngazi zote ili kuleta usawa baina ya maskini na matajiri.

Akijibu swali hilo, Dk. Bilal alisema pamoja na kwamba yeye si miongoni mwa walioficha fedha nje, lakini kama wapo Watanzania  na wakithibitika kuwa wameficha fedha kwenye benki za ng’ambo sheria na taratibu zitaongoza jinsi ya kuwashughulikia.

Alisema iwapo taarifa sahihi za watu hao walioficha fedha nje zitapatikana ,serikali itawachukulia hatua  bila kujali nafasi zao na kwamba suala hilo litawekwa wazi bila kificho.

Watanzania zaidi ya 300 wanadaiwa kuficha mabilioni ya Dola za Marekani katika benki za kigeni ikiwemo Benki ya Uswisi ambapo hivi karibuni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema)  Zitto Kabwe, aliwasilisha hoja binafsi bungeni kutaka uchunguzi wa kina ufanyike na wahusika washughulikiwe kisheria.

Taarifa hizo alizozitoa zilihusisha madai kuwa baadhi ya Watanzania wameficha Dola milioni 300 kwenye benki za Uswisi ikiwa ni rushwa walizopewa kwenye miradi ya utafiti wa  gesi na mafuta inayofanywa na makampuni ya kigeni.
CHANZO: NIPASHE

No comments: