Mwenyekiti wa Kampuni ya Biashara za Nje ya Mjini Dar es salaam { ETG } Bwana Mahesh Patel akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Nyumbani kwake Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwa katika dua ya pamoja ya kumuombea shufaa Marehemu Mzee Othman Ali Bakari Mwenyekiti wa Mwanzo wa Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar aliyefariki dunia tarehe 15/11/2012 Mjini Dar es salaam na kuzikwa hapa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Kushoto yake Mwakilishi wa Jimbo la Kikwajuni Mh. Mahmoud Mohamme Muusa na kulia kwake ni Mzee Mwinyiwesa Idarous wakisoma Dua kumuombea Marehemu Mzee Othman Ali Bakari aliyefariki dunia Juzi Mjini Dar es salaam na kuzikwa hapa Zanzibar.
Kampuni inayojishughulisha na Biashara za nje yenye Makao Makuu yake Mjini Dar es salaam { Export Trading Group } ina mpango wa kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwajengea uwezo wakulima kumudu kuzalisha Kitaalamu ili kufikia kiwango cha uwezo wa kuuza mazao yao nje ya Nchi.
Mwenyekiti wa Kampuni hiyo Bwana Mahesh Patel alieleza hayo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi yaliyofanyika nyumbani kwa Balozi Seif Mazizini Nje Kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mwenyekiti huyo wa Export Trading Group Bwana Mahesh Patel alisema Kampuni yake imeshajipangia utaratibu wa namna ya kusaidia wakulima katika kuwapatia taaluma ya kisasa ya uzalishaji wa mazao yao.
Alisema utaratibu huo tayari unaendelea kutolewa na Kampuni yake katika Mataifa mbali mbali Barani Afrika na hivi sasa wameona ipo haja kwa Uongozi wa kampuni hiyo kutoa upendeleo pia kwa wakulima wa Zanzibar.
“ Tumekuwa tukiunga mkono juhudi za wakulima katika kuwapatia Taaluma bora za kisasa ambazo tayari zinafanya kazi katika Nchi kadhaa zikiwemo Malawi, Zambia, Zimbabwe,Burundi na Rwanda”. Alisisitiza Bwana Patel.
“ Taaluma hiyo ilienga zaidi katika mazao ya Ufuta, Mahindi zikiwemo pia mashine za kisasa za kubambulia Korosho katika Mkoa wa Tanga”. Aliendelea kufafanua Mwenyekiti huyo wa ETG.
Bwana Mahesh Patel alieleza kwamba katika kusaidia wakulima wa Zanzibar kimapato ili kumudu vyema kuendesha Maisha yao ameiomba Serikali kufikiria namna ya kuipatia Kampuni yake uwezekano wa kuzalisha Bidhaa ya Sukari hapa Nchini.
Alisema kuendelezwa kwa sekta hiyo Nchini upo uwezekano mkubwa wa kuongeza ajira kwa wakulima walaio wengi kumudu kuendesha Ukulima wa Miwa na hatimae kuiuza kiwandani baada ya kupatiwa Taaluma sahihi.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Kampuni hiyo inayojishughulisha na Biashara za Nje { ETG } kwa uamuzi wake wa kusaidia nguvu za wakulima Kitaalamu katika uzalishaji mali.
Balozi Seif alisema Kilimo bado kinaendelea kuwa uti wa Mgongo wa Taifa hili lakini kinachokosekana zaidi hivi sasa kwa wakulima walio wengi ni ufinyu wa Taaluma ya kuendesha kilimo hicho.
“ Tumekuwa tukishuhudia mfano wa wakulima wetu wengi wa mpunga wamekuwa wakilima zao hilo muhimu katika eneo kubwa lakini kipato chake hakilingani na nguvu na uwezo waliotumia katika uzalishaji”. Alifafanua Balozi Seif.
Alisema upo uwezekano wa wakulima wengi kufaidika na kilimo cha miwa na baadaye kuiuza kiwandani ambacho utafiti unaonyesha kwamba mapato yake ni makubwa ikilinganishwa na kilimo cha Mpunga kilichozoeleka kwa wakulima hao.
Kampuni ya Biashara za Nje { ETG} inaendelea kutoa huduma kwa Mataifa kumi na nane Barani Afrika Pamoja na India, China na Kusini Mashariki mwa Bara la Asia tokea kuundwa kwake Mwaka 1967.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifika Mtaa wa Kwaala Msha kuifariji Familia ya Mwenyekiti wa mwanzo wa Chama cha Wafanyabiashara wenye viwanda na wakulima Zanzibar Bwana Othman Ali Bakari aliyefariki dunia Tarehe 15/11/2012 Mjini Dar es salaam ma kuzikwa hapa Zanzibar.
Bwana Othman ambae pia aliwahi kuwa Meneja wa Kampuni ya Uchongaji ya Jemille General Trader ya Kijangwani hadi kufariki kwake alizaliwa tarehe 11/4/1930 na kupata elimu ya msingi mwaka 1936 na kuendelea sekondari hadi mwaka 1950.
Akiwafariji wafiwa hao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali kwa aupande wake pia aimepata pigo kutokana na kifo cha Bwana Othman kufuatia mchango wake mkubwa wakati alipokuwa mtumishi katika ngazi tofauti Serikalini.
Akitoa Shukrani kwa niaba ya Familia ya Marehemu Mzee Othman Ali Bakari Mzee Mwinyiwesa Idarous aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutokana na Viongozi wake wa ngazi za juu kuwa karibu na jamii hasa pale Jamii hizo zinapopatwa na misiba au maafa.
Mzee Othman Ali Bakari katika uhai wake aliwahi kuwa mfanyakazi wa Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar katika kitengo cha useremala na baadae Meneja wa Ujenzi wa Shirika hilo.
Pia aliwahi kuwa Naibu Katibu wa Shirika la ZSTC sambamba na Mkurugenzi wa Kikundi cha Utamaduni katika masuala ya Jamii Mitaani cha Kwaala Msha { Aalamsha Social Club }
Marehemu Mzee Othman Ali Bakari ameacha Vizuka wawili, Watoto kumi na sita na Wajukuu ishirini na Mbili.
Mwenyezi muungu ailaze roho ya Marehemu Mzee Othman Ali Bakari mahali pema peponi amin.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
17/11/2012.
No comments:
Post a Comment