ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 16, 2012

IJUE DAWA YA MPENZI MSALITI-2


USALITI katika mapenzi unauma sana. Asikuambie mtu, maumivu yake hayana mfano hata kidogo. Ndiyo sababu tunajadili mada hii ili kukupa mwanga wa tatizo hilo kwa undani hasa katika kukabiliana nalo linapotokea na namna ya kukomesha kabisa jambo hilo lisitokee.

Katika utangulizi wangu wiki iliyopita, nilianza kwa kueleza kisa cha msomaji wangu mmoja aliyeomba ushauri. Kwa kuona ukubwa wa tatizo lake, nikaamua kuliweka kwenu kama mfano wa somo letu. Hebu sasa twende tukaone...
TATIZO LIKO WAPI?
Kwanza kabisa nilimwambia huyo dada kuwa anakosea sana kuwa na suluhisho la moja kwa moja, wakati akiomba ushauri. Hana sababu ya kukata tamaa na kuwa na wazo la kuachana na mume wake.
Kubwa zaidi ambalo anatakiwa kuwaza kwasasa ni kwamba, tayari ameshaingia kwenye ndoa, kama inavyojulikana ndoa haina majaribio ni ahadi. Sasa siyo rahisi kuamua kumuacha mumewe.
Hutakiwi kuwa mvivu wa kufikiria kiasi hicho, unatakiwa kuwaza mbali zaidi ya hapo. Unasema umechoka, ni sawa...hakuna anayeweza kuzoea kusalitiwa, lakini ni kweli kwamba umeshindwa kukabiliana na tatizo hilo la mumeo kukusaliti?
Siku zote matatizo hayakimbiwi, hutafutiwa suluhisho ili baadaye uweze kusimama kifua mbele ukifurahia mafanikio yako baada ya wewe mwenyewe kuibuka mshindi!
Mimi nina mtazamo tofauti kidogo kuhusu usaliti, siamini hata kidogo kwamba mwanaume/mwanamke anaweza kumsaliti mwenzi wake kwa ‘makusudi’, lazima kuna kitu fulani nyuma ya pazia. Hebu jiulize, mumeo alikuwa anakusaliti tangu mwanzo wa uhusiano wenu au ni tabia mpya?
Umesema kwamba upo kwenye ndoa kwa miaka 15 sasa na mnao watoto wanne, je, ni kweli kuwa kwa muda wote huo mumeo alikuwa anakusaliti? Naamini jibu litakuwa si kweli.
Niliamua kumshauri hivyo gazetini, nikiamini kwamba kuna wengine ambao wangejifunza kupitia yeye. Ndivyo ilivyokuwa, mara baada ya gazeti kutoka, wasomaji wengine wengi waliwasiliana na mimi, wakieleza matatizo yao lakini wengine wakitoa michango yao ya ushauri.
Hebu tuone baadhi ya maoni hayo, nina hakika kuna kitu utajifunza, kisha tutaendelea na mada yetu.
Msomaji wa kwanza: Rejea makala yako gazetini, hakuna dawa ya kusalitiwa, unatia hasira sana, mume wangu alikuwa anatembea na rafiki yangu kwa muda mrefu sana, una dawa gani hapo? Nina maamuzi, najipanga, nitaachana naye baada ya kuweka mambo yangu sawa. Kuwa mwangalifu na unachokiandika. Maumivu mengine hayana dawa. Usidanganye watu!
TUNAJIFUNZA NINI?
Kwanza nilishtuka sana baada ya kupata hii meseji kutoka kwa msomaji huyo, lakini baada ya kutulia kwa muda nilitabasamu! Unajua kwa nini? Kwa sababu niliona nimefanikiwa kugusa pale nilipokuwa napataka!
Pole sana dada yangu, najua ni kiasi gani unateseka na usaliti, lakini naamini kabisa, mpaka mumeo anafikia hatua ya kutembea na rafiki yako kuna mahali unakosea bila wewe kujua.
Kwa haraka-haraka, kwa kukusaidia wewe na wengine wenye tatizo kama lako, usiruhusu mazoea ya karibu sana kati ya mumeo na shoga yako. Hata wanaume pia, msiruhusu rafiki zenu wawazoee sana wake/wapenzi wenu. Mazoea kupitiliza ni hatari. Yanaweza kuwaingiza mtegoni.
Ikiwezekana hata namba za simu wasibadilishane. Wanataka kuwasiliana kivipi? Kwa ajili ya nini mtu na shemeji yake? Abiria anachunga mzigo wake mwenyewe jamani! Hata hivyo, kuna baadhi ya vitu ukivikosea utasalitiwa tu, hata kama si kwa rafiki yako kuna nyumba ndogo!
Tena kwa mumeo huyo ambaye amefikia hatua anatembea na shoga yako, bila shaka atakuwa na msururu wa wanawake huko nje.
Unajua nini kilitokea? Baada ya kuandika mada hii kwa mara ya pili, msomaji huyo alinipigia simu na kuniambia amebatilisha maneno yake. Kwamba amebadilika na amejifunza kutokana na mada hii. Akili yake imekuwa mpya na ameshayaondoa mawazo ‘mgando’ aliyokuwanayo awali.
Kwangu mimi, naona alifanya maamuzi mazuri, yenye busara na bila shaka sasa anaishi akiwa na mtazamo mpya kabisa. Kwako pia liwe funzo.
Wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!
Chanzo:Global Publishers

No comments: