ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 16, 2012

JK aitega Nec mpya

  *Ataja sifa za atakaowateua Kamati Kuu
  *Aponda vikali waliotaka kuleta rabsha
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, ameweka wazi kuwa mjumbe yeyote wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ambaye hataweza kutumia muda wake mwingi kuanzia saa hadi mwaka 2015 kwenda mikoani na wilayani kueleza sera na ilani ya chama kwa wananchi ajiondoe mapema.

Rais Kikwete amesema kuwa kazi ya kwanza ya Nec mpya ni kuhakikisha kuwa wajumbe wake wanatumia muda mwingi kufanya kazi za chama.

Kikwete alisema mjumbe yoyote ambaye atakuwa na shughuli nyingine nje ya chama ni bora akafanye shughuli yake badala ya ile ya CCM.



Rais Kikwete aliyasema hayo jana mjini Dodoma katika hafla ya kuwapongeza viongozi wa wapya wa chama hicho waliochaguliwa katika Mkutano Mkuu wa nane uliomalizika Jumanne na Nec juzi.

“Kama una biashara yako basi nenda huko, lakini tunataka wajumbe wa Nec wafanye kazi ya chama muda wote nginja nginja kituo chetu cha kwanza Ikulu mwaka 2015,’’ alisema na kushangiliwa na wanachama.

SIFA ZA WAJUMBE WA CC

Aidha, alisema Kamati Kuu (CC) mpya atakayoiunda itakuwa na wajumbe wenye sifa, taaluma, iliyosheni maarifa, ujuzi na itakoyokuwa na uwezo wa kushauri na kuisimamia serikali.

“Ninajipanga vema kuteua Kamati Kuu ili tupate watu wazuri na kuwa na mchanganyiko, iliyosheheni maarifa na ujuzi na yenye uwezo mkubwa wa kuishauri na kuisimamia serikali,” alisema.

Vile vile, Rais Kikwete alisema wajumbe wa  Nec wataundiwa kamati maalum zinazolingana na idara zilizopo ndani ya chama kwa ajili ya kuleta tija na ufanisi katika idara hizo.

Idara zilizoko ni Fedha na Uchumi, Itikadi na Uenezi, Oganaizesheni, Siasa na Mambo ya Nje. Waliochaguliwa juzi kuziongoza ni Zakia Meghji, Nape Nnauye, Seif Mohammed Khatib na Dk. Asha-Rose Migiro.

Kadhalika, Rais Kikwete alisema wale wote waliokuwa wakitambika ili CCM iharibikiwe wanaota ndoto za mchana zisizokuwa na tija.

“Wale wote waliokuwa wakiota ndoto hizo kwa kukitakia mabaya CCM ni watu ambao hawakijui chama chetu,’’ alisema bila kuwataja.

Alisema CCM ina viongozi makini wanaojua kupambanua jema na baya na kubwa zaidi ni kujua lipi lina maslahi kwa chama na lipi halina maslahi.

“Yale ambayo walitarajia yatokee hayakuweza kutokea na mimi ningeshangaa kama wajumbe wale wangeyafanya yale ambayo yalikuwa yakiombwa na baadhi ya maadui zetu,” alisema na kuongeza:

“Na ndiyo maana mimi sikuwa na wasiwasi manake nilikuwa nasikia maneno haya maneno yale wakati mwingine mtu anakuja anakueleza hivi nikawaambia silikilizeni CCM ninayoijua mimi haya hayatatokea.”

Alisisitiza kuwa hayo yote waliokuwa wakiyafikiria ni ndoto za mchana ambazo wanatumia nguvu kubwa, lakini hazina  nafasi katika chama.

Kikwete alisema kuna baadhi ya watu ambao hawaitakii mema CCM na wamekuwa wakitambika usiku na mchana ili chama hicho kiharibikiwe na hasa wakati wa mkutano wake wa nane.

“Wengi wa watu hao walikuwa wakiomba CCM itoke katika mkutano huo ikiwa kipande kipande, lakini wakatahayari wenyewe kuona tumetoka tukiwa na kasi mpya na umoja tele,” alisema.

 Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa, alisema hotuba ya Kikwete kwa mkoa Dodoma itatumika kama fimbo ya kuwachapia wapinzani wa CCM.

Aidha alimuomba Rais kukubali jina lake kutumika kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

WAPINZANI WAPONDA 

Siku mbili baada CCM kukamilisha chaguzi zake, viongozi wa vyama vya upinzani wamesema hakuna jipya katika safu mpya ya Sekretarieti ya chama hicho na kwamba sasa njia ni nyeupe kwa wapinzani kuingia Ikulu mwaka 2015.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.Willibrod Slaa, alisema hakuna jipya kwa viongozi wa juu wa CCM waliochaguliwa kwa sababu waliopo ni wale wale ambao walikuwepo miaka yote na hawakuweza kusaidia kuleta mabadiliko yeyote ndani ya chama hicho.

“Kuna msemo wa Kiswahili unasema huwezi kuweka mvinyo mpya kwenye chupa ya zamani, hawa waliochaguliwa hawana jipya na baadhi yao wana kashfa kibao ambazo tutaanza kuziweka wazi kwa wananchi ili wawafahamu vizuri,” alisema Dk. Slaa.

Dk. Slaa huku akiwataja kwa majina, alisema baadhi ya waliochaguliwa walishiriki katika kashfa ya wizi wa fedha Malipo ya Madeni ya Nje (Epa) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) takribani Sh. bilioni 133 ambazo zilitumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 kuwezesha  CCM kupata ushindi.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara, Julius Mtatiro, alisema Sekretariati mpya ya CCM haina jipya sana sana wameongeza watu ambao wanafahamika kiutendaji na wamewahi kudumu katika ofisi za umma na kuacha rekodi mbaya.

Mtatiro alidai kuwa mfano, Katibu Mkuu, Abrahaman Kinana, kwa muda mrefu amekuwa kampeni meneja wa CCM za kushinda kwa lazima bila kujali matakwa ya wananchi.

“Kwa sababu CCM ni ileile, Sekretariati hii haitakuwa na jipya, wataendelea kupiga kelele bila mafanikio kama anavyofanya ndugu yangu Nape Nnauye,” alisema Mtatiro.

Mtatiro aliongeza kuwa rushwa, makundi, umimi, uroho kuwatetea matajiri na wawekezaji na kuwapora rasilimali wananchi maskini havitaisha na mfumo huu wa CCM hauwezi kubadili labda CCM iwe imeondoka madarakani.

Alisema Watanzania wana kazi kubwa ya kufanya  kwa kuwa hakuna ajira, hakuna huduma za afya, hakuna miundombinu ya maana hivyo kinahitajika chama mdabala kuja kuwaokoa Watanzania.

Mwenyekiti wa Chama cha APPT Maendeleo, Peter Kuga Mziray, alisema viongozi wa CCM wa juu waliochaguliwa imetoa fursa nzuri kwa vyama vya upinzani kuingia Ikulu.

Mziray alisema walichaguliwa kwa kuanzia na Katibu Mkuu Kinana, asilimia kubwa ni wazee ambao hawataweza kustahimili mikikimiki ya kisiasa ambayo imekuwa na ushindani mkubwa nchini.

“Viongozi wa juu wote waliochaguliwa walikuwepo kipindi cha uongozi wa awamu ya tatu na sasa wamekuwa ni wazee, yaani CCM sasa inaongozwa na vi-babu, nina imani hawataweza kwa sababu hivi sasa ni siasa za vijana,” alisema Mziray.

Alisema kinachotakiwa hivi sasa ni kwa vyama vya upinzani kujipanga na kushirikiana kama vinataka kuiondoa CCM madarakani.

Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema, alisema vyama vya upinzani vinaweza kuishinda CCM iwapo vitaacha siasa za kitoto ambazo zinapelekea vyenyewe kujengeana chuki zisizokuwa na maana.

“Rais Kikwete ni rais wetu wote akifanya jambo zuri lazima tumsifu, lakini inashangaza pale anapojitokeza kiongozi wa chama cha upinzani akimsifu Rais anaanza kutupiwa madongo na kueleza kuwa yeye ni CCM ‘B’,” alisema Mrema na kuwataka wapinzania kujenga umoja ambao utakuwa nguzo kuu ya kushika dola 2015.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: