ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 7, 2012

Kanisa lamvaa Prof. Lipumba kuhusu vurugu za kidini


Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba

Kanisa la Kiinjili la Kipentekoste Tanzania limemshukia Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, likimtaka kuacha kuingiza siasa katika suala la vurugu za kidini zilizoanza kujitokeza nchini, kwani kufanya hivyo ni kuleta uchochezi kwa wananchi.

Mchungaji wa kanisa hilo, William Mwamalanga, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, alisema wamepokea kwa hisia tofauti kauli ya Profesa Lipumba kufuatia mvutano kati ya Waislamu na Serikali kwani makanisa yalipochomwa moto chama chake hakikuwahi kutoa tamko kulaani kuhusiana na vitendo hivyo.
Kauli ya kanisa hilo imekuja siku moja baada ya Profesa Lipumba kueleza mambo mengi ikiwemo suala la kukamatwa kwa Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda.

Mwamalanga alisema kauli ya Lipumba kwamba serikali imeshindwa kuchukua hatua kumaliza mvutano huo na kwamba imemuachia Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova kutoa vitisho ni kuleta uchochezi ambao utasababisha waislamu kujenga chuki dhidi ya serikali na Jeshi la Polisi.

Alisema Kamanda Kova anatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria zilizopo kwasababu kama kiongozi wa Jeshi la Polisi asingeweza kuona amani iliyopo nchini inavunjwa na kundi la watu wachache wenye maslahi yao binafsi huku wakikaa pembeni.

Alisema viongozi wa serikali na wananchi wanatakiwa wawe makini na kauli za viongozi wa kisiasa kwani zinalenga zaidi kujitafutia umaarufu wa kisiasa kupitia mvutano uliopo kati ya Waislamu na Serikali kufuatia kukamatwa kwa viongozi kadhaa wa dini hiyo.

Alisema Watanzania wanamfahamu Profesa Lipumba kuwa ni msomi hivyo wanashangaza kuona anazungumzia jambo ambalo tayari lipo mahakamani linashughulikiwa kisheria.

Juzi akizungumza na waandishi wa habari pamoja na mambo mengine, Profesa Lipumba alisema kesi ya Sheikh Ponda ambayo msingi wake ni madai ya kiwanja yanayotakiwa kusuluhishwa na Mahakama ya Ardhi na kwamba Sheikh Ponda ana haki ya kupewa dhamana hata kama kauli zake haziifurahishi serikali.
CHANZO: NIPASHE

No comments: