KUTOTOLEWA kwa elimu ya uzazi na madhara yatokanayo na wanafunzi kujihusisha na mapenzi katika umri mdogo, kunatajwa kuwa miongoni mwa sababu kubwa zinazochangia wanafunzi hasa wa shule za msingi kupata ujauzito.
Mmoja wa wanafunzi wanaoamini sababu hii ni Happiness Mzalendo, anayeishi kijiji cha Kabirizi, Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera. Msichana huyu ameweka historia ya aina yake nchini baada ya kujifungua siku ya mtihani.
Mzalendo (18) alikuwa mmoja wa watahiniwa wa mtihani wa darasa la saba mwaka huu, lakini akiwa ndani ya chumba cha mtihani, siku ya kwanza ya mtihani huo wa Taifa, alishikwa na uchungu na hatimaye kujifungua mtoto wa kiume.
Anasema uchungu huo ulimfika akiwa anafanya mtihani wa hesabu uliokuwa mtihani wa pili kwa siku hiyo. Aliomba msaada kwa msimamizi na kutolewa nje ya darasa, kitendo kilichoashiria kwisha kwa ndoto zake za kuwa daktari.
Mzalendo tofauti na baadhi ya wasichana wanaoamua kuacha shule wanapojigundua kuwa ni wajawazito, alitumia udhaifu wa kutokuwapo kwa zoezi la kupima wanafunzi wenye ujauzito shuleni kwake, kuficha siri ya mzigo aliokuwa ameubeba tumboni mwake.
Licha ya kujijua kuwa ni mjamzito, aliendelea na shule akitarajia kufanya mtihani wa mwisho ambao kwake ulikuwa daraja la kuelekea katika safari yake ya kuisaka ndoto ya udaktari. Hata hivyo, leo anasikitika kwani safari iligota siku moja kabla ya kulifikia daraja.
Asimulia ilivyokuwa
Mzalendo anasema alihisi uchungu Septemba 19 wakati akifanya mtihani wa Taifa wa kuhitimu darasa la saba. Alimweleza msimamizi wa mtihani amtoe nje ya darasa kutokana na hali yake kuwa mbaya.
Baada ya kutolewa nje alikwenda kujifungua chini ya mgomba ulioko katika shamba la shule. Anasema alipata msaada kutoka kwa mama mpita njia aliyekuwa akitoka shamba kulima.Mtoto aliyemzaa alikuwa na uzito wa kilogramu 2.7 ambaye mpaka sasa hajapewa jina.
Licha ya kupewa ruhusa ya kuendelea kufanya mitihani iliyobaki siku inayofuata na uongozi wa shule, alishindwa kwenda shule kwa kukosa mtu wa kumwachia mtoto wake.
Anasema baada ya tukio hilo alirudi nyumbani anapoishi maisha ya kifukara na bibi yake ambaye kwa kuwa alikuwa akijua hali ya ujauzito wake, hakumgombeza.
“Nilipogundua kuwa nimepata mimba, sikumficha bibi yangu nilimwambia akanizuia kuitoa, lakini shuleni walikuwa hawajui kama nina mimba hadi nilipojifungua nikifanya mtihani.” anasema.
Mzalendo anasema sababu kubwa iliyomsukuma kuingia katika uhusiano wa kimapenzi na hatimaye kubeba ujauzito ni kuishi maisha ya kimasikini, ambapo alikuwa akilazimika kutafuta mahitaji ya kuendesha maisha yake na ya bibi yake ambaye ni ajuza.
Anaongeza kusema: “Baba yangu alinitelekeza siku nyingi, hajui naishije, nakula nini na hata mahitaji ya shule alikuwa hajui nayapata kutoka wapi.Madaftari nilinunua mwenyewe, uniform (sare) nilinunua pia, ningepata wapi pesa wakati mimi ni mwanafunzi?”
Maisha ya ulezi
Wakati Mzalendo akihangaika kulea mtoto wake, huku akiwa hana kipato cha uhakika, kijana alimyempa mimba hiyo, inadaiwa aliondoka kijijini hapo na kuelekea visiwani kwa madai ya kutafuta fedha.
Anasema alipomweleza kijana huyo kuwa ana mimba yake, hakukataa. Alikubali kuwa atamuoa, lakini avumilie kwanza na afanye mtihani.
“Mwenzangu hajaoa, aliniahidi nikimaliza mtihani atanioa, lakini kwa sababu anaishi kwao alisema kwanza atafute pesa ajenge nyumba tupate pa kuishi. Nilimwamini labda kama alikuwa ananiongopea siwezi kujua,”anaeleza Mzalendo.
Bibi yake mlezi aitwaye Felista Nestory anasema asingeweza kumfukuza mjukuu wake, maana alimlea kwa shida tangu alipofiwa na mtoto wake (mama Hapiness) na kumwachia jukumu la kumlea bila kuwa na kipato cha uhakika.
“Ni kweli amekosa, lakini nimfukuze aende wapi, hayo yametokea sasa tunapaswa kukaa na kuangalia tufanye nini, ili mtoto aliyezaliwa aweze kulelewa vizuri.” anasema bibi huyo.
Lawama zake
Unapozungumza naye, pamoja na kujuta kwa yaliyomkuta, Mzalendo anaulalamikia uongozi wa shule yake kwa kutowapa elimu ya uzazi na madhara ya kufanya mapenzi katika umri mdogo.
“ Tangu nimeanza shule hadi najifungua, mimi na wenzangu hatukuwahi kupatiwa mafunzo kuhusu madhara yatokanayo na kufanya mapenzi katika umri mdogo,’’anasema.
Kauli hiyo pia inaungwa mkono na aliyekuwa mwanafunzi mwenzake, Philimina Mussa anayesema: “Tumeanza darasa la kwanza mwaka 2006, sasa tumehitimu lakini hatujawahi kufundishwa madhara ya uhusiano wa kimapenzi katika umri mdogo wala athari za mimba za utotoni wakati ni muhimu sana kwetu.”
Siyo tu elimu ya uzazi ambayo haikuwa ikitolewa shuleni hapo, mhitimu mwingine wa shule hiyo, Elivia Antidius anasema hata wataalamu wa kupima ujauzito kwa wanafunzi, hawakuwahi kuja shuleni kwao, kitendo anachoamini kinachangia baadhi ya wanafunzi kupata mimba.
“Endapo tungekuwa tunapimwa mimba shuleni, ingesaidia kupunguza idadi ya watoto wanaobeba mimba, maana wangeogopa kutambulika na kufukuzwa shule,’’anaeleza mwanafunzi huyo.
Baba mzazi ajitetea
Pamoja na kusikitishwa na kitendo cha mwanawe kubeba ujauzito na kujifungua, baba mzazi wa Hapiness, Justuce Mzalendo anasema licha ya kuishi jirani na binti yake, hakuwahi kujua kama ni mjamzito.
Aidha, anapinga madai kuwa alimtelekeza, kwani alikuwa akimpa mahitaji ya nyumbani na shule.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment