ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 28, 2012

Sumatra isifanye kazi kwa staili ya zimamoto

MWISHONI mwa wiki tulichapisha picha katika ukurasa wa mbele ikimuonyesha mwanamke mmoja akiwa amebebwa na mwanamume akimwingiza katika basi la daladala kupitia dirishani. Daladala hilo linalofanya safari zake kati ya Ubungo na Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam lilikuwa tayari limejaza abiria kupita kiasi, lakini kutokana na kutokuwapo usimamizi na udhibiti wa mamlaka husika katika vituo vya usafiri, bado abiria walikuwa wakiendelea kuingia katika basi hilo kupitia madirishani.
Hatuoni umuhimu hapa wa kuelezea zaidi hali aliyokuwamo mwanamke huyo aliyeingizwa katika daladala hiyo kupitia dirishani. Hata hivyo, yatosha tu kufahamu kwamba mwanamke huyo alikuwa katika hali ya unyonge na udhalilishwaji mkubwa, kutokana na vyombo vya usafirishaji wa abiria nchi nzima kuachwa kuendesha biashara hiyo kinyume na sheria na kanuni zilizowekwa.

Ni uthibitisho kwamba Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imeshindwa kusimamia taratibu, kanuni na sheria zinazohusu vyombo vya usafirishaji wa abiria na sasa mamlaka hiyo inaonekana kubaki kuwa mtazamaji tu wa matukio hayo ya karaha na aibu. Hicho ndicho kielelezo cha fujo, vurugu na ghasia tunazozishuhudia kila kukicha katika vituo vya mabasi, treni na bandari zetu, kutokana na mamlaka hiyo kushindwa kuweka mifumo endelevu ya kuhakikisha kwamba abiria wanaingia katika vyombo hivyo vya usafirishaji kwa kupanga misururu.

Sumatra sasa inafanya kazi kwa staili ya zimamoto na ndiyo maana hatuoni ikiweka malengo yanayopimwa kwa ufanisi na viwango vya utekelezaji. Matokeo yake ni kukosa ufuatiliaji kutokana na ulevi wa viongozi wengi katika mamlaka hiyo kushinda katika maofisi yenye viyoyozi wakisoma mafaili yaliyojaa ripoti za mikakati na mipango isiyotekelezeka.

Tulishuhudia majuzi Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe akihaha huku na kule katika kujaribu kupunguza makali ya matatizo ya usafiri nchini, huku akiwataka viongozi wa Sumatra kuacha ofisi zao na kuingia barabarani kusukuma juhudi hizo. Lakini Sumatra haionekani kutambua kuwa, lazima ibuni mikakati na mbinu maalumu kukabiliana na matatizo ya usafiri, hasa jijini Dar es Salaam kutokana na ukweli kwamba jiji hilo ndilo kitovu cha uchumi wa nchi yetu.

Ndiyo maana hatuoni mamlaka hiyo ikitumia uwezo wake kisheria kuwatia adabu madereva na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji wa abiria. Pamoja na kutoa taarifa nyingi kupitia magazetini, Sumatra imeshindwa kufuatilia utekelezaji wa mikakati na mbinu mbalimbali inazozitangaza.
Kwa mfano, jana ilitangaza adhabu watakazopewa wasafirishaji wa abiria waendao mikoani watakaopandisha nauli wakati wa Krismasi na Mwaka Mpya kwamba watalipa faini ya Sh250,000 au leseni zao kusimamishwa, huku ikijua kwamba tatizo hilo sasa limekuwa sugu kutokana na mamlaka hiyo kutokuwa na umakini na ufuatiliaji wake kutokuwa endelevu.

Hata hivyo kuna wakati viongozi wa Sumatra wanaonyesha uwezo wa kufikiri. Mfano ni utaratibu wake mpya iliotangaza jana, kwamba itasitisha utoaji wa leseni mpya kwa mmiliki mmoja mmoja katika baadhi ya njia hapa jijini. Kwamba ifikapo katikati ya mwaka ujao wasafirishaji wanaotoa huduma katika njia hizo watatakiwa kujiunga au kuanzisha makampuni au ushirika ili wapewe leseni za kutoa huduma katika njia hizo muhimu.

Bila shaka lengo hapa ni kuhakikisha kwamba utaratibu huo baadaye unahusu njia zote kuu za kutoka na kuingia katikati ya Jiji na kumaliza usafirishaji wa ubabaishaji utokanao na umiliki wa daladala mojamoja.

Sisi tunadhani Sumatra inaweza kupunguza tatizo la usafiri nchi nzima iwapo itaacha kufanya kazi kwa mazoea. Ikumbukwe kuwa, huko nyuma David Mwaibula peke yake aliweza kumaliza fujo na kiburi cha madereva na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji wa abiria jijini Dar es Salaam. Kama mtu mmoja aliweza kufanya jukumu hilo kwa ufanisi, Sumatra yenye mtandao mpana, tena nchi nzima itashindwaje?
Mwananchi

No comments: