ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, November 17, 2012

TAZARA kwawaka moto mishahara yaota mbawa

Baadhi ya abiria waliofika katika stesheni ya Tazara jana, wakiwa kwenye misururu wakisubiri kurudishiwa nauli ,baada ya mgomo wa wafanyakazi kuendelea na mgomo. Picha kushoto, mama aliyefikia 
Pamoja na serikali kuahidi kuwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) wangelipwa mishahara yao kuanzia jana, ahadi hiyo imeota mbawa.
Wakati wafanyakazi hao wakiwa katika hali ya kukata tamaa kutokana na kukosa mishahara ya miezi minne,  abiria waliokuwa wasafiri  tangu Ijumaa  iliyopita kwenda Zambia wameendelea kurejeshewa nauli zao.


Katika ofisi ya Tazara jijini Dar es Salaam  wasafiri hao waliendelea kujipanga misururu mirefu kurejeshewa  nauli zao. Safari  ya wiki iliyopita ilikwama  kutokana na mgomo  wa wafanyakazi wanaodai  mishahara ya miezi minne kuanzia Juni hadi Oktoba mwaka huu.

Akizungumza na wafanyakazi hao jana jioni, Naibu Waziri wa Uchukuzi Dk. Charles Tizeba, aliahidi kuwa wafanyakazi hao wangeanza kulipwa mshahara wa Septemba jana mingine  ya Oktoba, Juni na Julai ingelipwa baada ya Wizara  ya Uchukuzi kukutana na menejimenti.

Akizungumzia kadhia  hiyo, Naibu Waziri alisema treni ya kwenda Zambia ilikuwa iondoke jana lakini ilishindikana baada ya abiria wachache kujitokeza .

“Tusingeweza kupeleka treni kwa hasara maana abiria walikuwa wachache kwa vile  wengi walisharudishiwa nauli zao. Uhakika wa usafiri utakuwa Jumanne wiki ijayo,” alisema.

Abiria hao wakiwa na mizigo, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, walifurika kwenye stesheni ya Tazara Dar es Salaam wakiwa na matumaini ya kusafiri, lakini badala yake walikuta tangazo likieleza kuahirishwa kwa safari hiyo hadi Jumanne bila ya kutolewa ufafanuzi zaidi.

Naibu Waziri alisema ilishindikana kutoa taarifa mapema kwa abiria kutokana na muafaka kati ya wizara na wafanyakazi wa Tazara kufikiwa usiku.

Baadhi ya wafanyakazi ambao walikataa kutaja majina yao, walisema matatizo hayo yamesababishwa na serikali kutosimamia ipasavyo uendeshwaji wa mamlaka hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wafanyakazi hao walidai kuwa Tazara inaendeshwa kisiasa zaidi tofauti na Zambia ambako shughuli za usafirishaji abiria na mizigo zinaendelea kama kawaida hadi mpakani na Tanzania.

Mgomo huo wa wafanyakazi wa Tazara uliathiri pia safari za treni ya abiria za ndandi ya  Dar es Salaam.

Jitihada za kuupata uongozi wa Tazara akiwemo Mkuu wa Stesheni ya Tazara, ilishindikana baada ya ofisi zao kufungwa.

CHANZO: NIPASHE

No comments: