ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 7, 2012

Upinzani kumshtaki Rais bungeni

Julius Magodi, Dodoma
SUALA la kuwapo kwa majaji wasiokuwa na sifa nchini limeingia katika sura mpya baada ya Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu kusema atawasilisha hoja ya kumshtaki Rais Jakaya Kikwete kama atashindwa kuwaondoa kazini ifikapo Kikao cha Bunge lijalo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Bunge jana, Lissu alisema amechukua uamuzi huo baada ya kuona Bunge limeikalia ripoti ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iliyomhoji kuhusu kauli yake ya kuwatuhumu majaji kuwa baadhi yao hawana sifa.
Alisema ameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuona Rais Kikwete ambaye ana mamlaka ya kuteua majaji, ameshindwa kuwaondoa kazini majaji hao wasiokuwa na sifa.

Lissu alisema atawasilisha hoja yake hiyo kwa kutumia Kanuni ya Bunge sehemu ya 11, Ibara ya 121, 122, 123, 124, 125 na 126 na pia kwa kutumia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 146 A.
Sehemu ya 11 ya Kanuni ya Bunge, Ibara ya 121 inaeleza kuwa mbunge yeyote anaweza kuwasilisha kwa Spika taarifa ya hoja ya kumshtaki Rais kwa madhumuni ya kumwondoa Rais madarakani kupitia azimio la Bunge kwa mujibu wa Ibara ya 46 A ya Katiba ikiwa inadaiwa kwamba Rais; ametenda vitendo ambavyo kwa jumla vinavunja katiba au sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Lissu alisema atakusanya saini za wabunge kuunga mkono hoja yake ambayo ni asilimia 20 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge. Wabunge wote kikatiba ni 357.
Julai 13, mwaka huu wakati akitoa maoni ya Kambi ya Upinzani katika Wizara ya Katiba na Sheria bungeni, Lissu alisema uteuzi wa majaji umegubikwa na ukiukwaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Alisema baadhi ya majaji walioteuliwa hawana sifa, uwezo na kwamba hawakufaa kufanya kazi hiyo.
Kauli hiyo ilisababisha Bunge kuiagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo (CCM), Hassan Ngwilizi kumhoji ili athibitishe kauli yake.
Alisema wakati akihojiwa na kamati hiyo, pamoja na nyaraka nyingine, aliwasilisha nakala ya ripoti ya kikosi kazi kilichoundwa mwaka 2008 na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo kuchunguza uteuzi wa majaji nchini.
Alisema ripoti ya kikosi kazi hicho kilibaini kuwapo majaji ambao hawana sifa ya kufanya kazi hiyo, lakini Rais Kikwete ameshindwa kuwaondoa kazini.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema alisema hali ya mahakama ni mbaya, kwani kuna majaji wawili ambao waliwahi kukamatwa kwa rushwa wakiwa mawakili, lakini wakateuliwa kufanya kazi hiyo.
Alisema baadhi ya majaji hawana uwezo hata wa kuandika hukumu kutokana na kutojua vyema lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo inayotumika katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.
Mbunge huyo alimtaja Jaji mmoja wa Mahakama ya Rufani ambaye ameteuliwa akisema hana hata shahada ya kwanza ya sheria kinyume cha taratibu.
“Kwa mfano, yupo Jaji wa Mahakama ya Rufani (jina tunalo), ambaye hana hata shahada ya sheria anaweza vipi kuwa jaji?,” alihoji Lissu.
Alisema jaji huyo hivi sasa anasoma shahada ya sheria katika chuo kikuu kimoja hapa nchini.
Lissu alisema ili mtu aweze kuchaguliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu lazima awe na elimu ya shahada ya kwanza ya sheria, awe ametumikia miaka 10 mahakamani na anayechaguliwa kuwa jaji wa Mahakama ya Rufani lazima awe ametumikia miaka 15 mahakamani.
Mbali ya kueleza hayo, Lissu alisema kwamba alitoa pia katika kamati hiyo, ushahidi unaoonyesha kuwa kuna jaji mmoja wa Mahakama Kuu ambaye hawezi hata kuandika sentensi moja ya Kiingereza iliyonyooka... “Kama jaji hawezi kuandika hata sentensi moja ya Kiingereza iliyonyooka, tunaweza vipi kuwa na mahakama inayotenda haki?”
Alisema kuna jaji mwingine ambaye ameongezewa mkataba wa kufanya kazi mara ya tatu kitu ambacho ni kinyume cha sheria. Alisema kwa mujibu wa Tume ya Mahakama, hakuna jaji ambaye anaweza kufanya kazi kwa mkataba kwa vipindi vitatu.
Mbunge huyo alisema mbali ya madudu hayo katika sekta ya mahakama, hivi sasa kuna jaji maarufu ambaye ameghushi umri wa kuzaliwa ili aweze kuendelea kufanya kazi hiyo.
Alisema jaji huyo amezaliwa Septemba 4, 1949 lakini amebadilisha umri wake kuwa amezaliwa Septemba 4, 1952 ili aweze kufanya kazi hiyo hadi mwaka 2017.
Mbunge huyo alisema kazi hiyo ya kughushi umri wa jaji huyo imefanywa kwa kunyofoa nyaraka za kumbukumbu zake Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alimtaka jaji huyo kuzirejesha mara moja nyaraka hizo vinginevyo katika Bunge lijalo atamtaja kwa jina hadharani.
Alipotakiwa kueleza kwa nini asimtaje sasa alisema akifanya hivyo anaweza kutingisha nchi.
Kama Lissu atachukua hatua hiyo, itakuwa ni mara ya pili kwa mbunge kuwasilisha bungeni hoja ya kutaka kumwajibisha kiongozi wa juu serikalini.
Mara ya kwanza alikuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe katika Bunge lililopita alipokusanya saini za wabunge kutaka kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akitaka awajibishe baadhi ya mawaziri waliokuwa wametajwa kuhusika katika matumizi mabaya ya madaraka katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Hata hivyo, Rais Kikwete alifanya mabadiliko makubwa katika Baraza lake la Mawaziri hivyo kuzima hoja hiyo ya Zitto.

Mwananchi

No comments: