ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 7, 2012

Viongozi wa Uamsho wapewa masharti magumu ya dhamana

Sheikh Farid Hadi Ahmed na wenzake saba leo wamerejeshwa tena rumande baada ya kupewa masharti magumu ya dhamana katika Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe, Sheikh Farid wakati akiondoka alisema “Haki Haifichi lazima ipo siku itakuja juu”

Salma Said, Zanzibar Novemba 07-2012
SHEIKH Farid Hadi Ahmed na viongozi wenzake saba wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar wanaokabiliwa na kosa uchochezi jana wamepewa masharti magumu ya dhamana na Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe Mjini Unguja.
Mahakama hiyo, Ame Msaraka Pinja ni Hakimu alisema kuwa baada ya mahakama kupitia maelezo ya pande zote mbili imeamuwa kutoa masharti magumu kwa watuhumiwa hao wakitakiwa kuwasilisha kiasi cha shilingi 1,000,000 taslim kila mshitakiwa, pamoja na kudhaminiwa na wadhamini watatu kila mmoja wadhamini ambao kila mmoja ametakiwa kuwasilisha kiwango kama hicho cha fedha taslimu.

Sambamba na masharti hayo, wadhamini hao pamoja na washitakiwa wenyewe wametakiwa kuwasilisha vivuli vya hati zao za kusafiria (pass port) au vitambulisho vya Mzanzibar Mkaazi.
Kwa mujibu wa mahakama, wadhamini hao lazima wawe ni wafanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) wawe na vitambulisho vya kazi pamoja na barua za Sheha wa Shehia wanazoishi.
Washitakiwa wote wamerejeshwa rumande chini ya ulinzi mkali wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuwa hata kama wangeweza kukamilisha masharti hayo ya dhamana, bado wangeendelea kuwepo rumande, kutokana na kukabiliwa na kesi nyengine katika mahakama ya Mrajis wa Mahakama Kuu Vuga, ambayo dhamana zao zimefungwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Ibrahim Mzee Ibrahim.
Kesi ya Sheikh Farid na wenzake saba ilianza kutajwa Oktoba 19 mwaka huu, ambapo
jana ilikuwa ni siku ya kutoa mamuzi juu ya dhamana za watuhumiwa hao ambao wanadaiwa kutenda kosa hilo Agasti 17 mwaka huu, huko katika maeneo ya Magogoni Msumbiji wilaya ya Magharibi Unguja.
Watuhumiwa wengine wanaokabiliwa na shitaka hilo ni Sheikh Farid Hadi Ahmed (41) Mkaazi wa Mbuyuni, Msellem Ali Msellem (52) Kwamtipura, Mussa Juma Issa (37) Makadara, Azzan Khalid Hamdan (43) Mfenesini, Suleiman Juma Suleiman (66), Makadara, Khamis Ali Suleiman (59) Mwanakwerekwe na Hassan Bakari Suleiman (39) Tomondo. Watuhumiwa hao wote kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 45 (1)(a) na (b) sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria ya Zanzibar.
Imeelezwa mahakamani hapo kuwa, Agosti 17 mwaka huu, majira ya saa 11:00 za jioni huko Magogoni Msumbiji wilaya ya Magharibi Unguja, wakiwa ni wahadhiri toka Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu, walitoa matamko ya uchochezi yanayoashiria uvunjifu wa amani na kusababisha fujo, maafa mbali mbali na mtafaruku kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mwendesha Mashtaka kutoka Serikalini alidai mahakamani hapo kuwa upelelezi wa shitaka hilo bado haujakamilika na kuiomba mahakama ipange tarehe nyengine kwa kutajwa kutajwa tena kesi hiyo.
Kwa upande wao Mawakili wa upande wa watuhumiwa Salum Tawfik na Abdalla Juma na waliiomba mahakama kutoa agizo la kupatiwa haki zinazostahiki kwa wateja wao, ikiwemo askari wa Vyuo vya Mafunzo kuruhusu kuonekana na familia zao, kupatiwa chakula, pamoja na kuweka katika vyumba vya pamoja na sio kama walivyo sasa ambapo baadhi yao wamo katika vyumba vya mtu mmoja mmoja na waruhusiwe kufanya ibada ya kusoma kuraan pamoja na kuweza kuletewa nguo.
“Kwa kweli hii sio haki na askari wa vyuo vya mafunzo wanaonekana kupindisha sheria kwa kutowatendea haki wateja wetu, inafika wakati wateja wetu wanafungiwa ndani masaa 24 na hata sisi mawakili wao haturuhusiwi kuwaona hii Mheshimiwa Hakimu haijawahi kutokea duniani kote”, alisema Tawfik.
Hivyo waliiomba mahakama kutoa agizo kwa maafisa wa Vyuo hivyo vya Mafunzo kuwatendea haki wateja wao hao, kama sheria na katiba ya nchini zinavyoelekea juu ya usawa wa watu wote mbele ya sheria na kulinda na kupata haki sawa kwa mtu ndani ya sheria.
Mwendesha Mashitaka wa mahakama hiyo Khamis Jaffar Mfaume, Mwanasheria wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) akitetea hoja hizo za upande wa utetezi alifahamisha kuwa, kwa upande wao hawana taarifa na suala hilo.
Hata hivyo alisema kuwa, kwa upande wao hawana pingamizi za aina yoyote kwa washitakiwa hao katika suala zima la kutendewa haki kama walivyo mahabusu wengine kutokana na hilo ni haki yao kwa mujibu wa sheria.
Baada ya hoja za pande hizo mbili, hakimu Ame Msaraka Pinja ameviagiza vyombo vya sheria kuzingatia wajibu wao wa kusimamia sheria, na kila chombo kinapaswa kufuata sheria kama zilivyowekwa.
“Mahakama haitakua na uamuzi kwani tumesikia kilichoelezwa, ila inasema kuwa vyombo vyote vya dola vina wajibu mkubwa wa kusimamia na kutekeleza sheria kama zilivyowekwa”, alisema Pinja.
Baada ya maamuzi hayo, Mwanasheria huyo wa serikali aliiomba mahakama hiyo kuiahirisha kesi hiyo na kuipangia tarehe nyengine kwa ajili ya kutajwa, kwa madai upelelezi wake bado haujakamilika.
Hakimu Ame Msaraka Pinja, alikubaliana na hoja hizo na kuiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 21 mwaka huu kwa kutajwa, na kuamuru washitakiwa hao wabakie rumande.
Kwa upande wa jana hali ya amani na utulivu ilitawala kwa kiasi kikubwa kutokana na kutokuwepo kwa msongamano wa watu, licha ya askari polisi wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU), wakiwa wamevalia mavazi maalumu huku wakiwa wameshikilia silaha mikononi, na wengine wakiwa na mikanda iliyohifadhiwa mabomu ya machozi, wakiwa wamelizingira aneo zima la mahakama hiyo kwa ajili ya kuimarisha usalama.
Washitakiwa waliwasili katika viunga vya mahakama hiyo majira ya saa 3:47 asubuhi, wakitokea rumande ya Chuo cha Mafunzo Kilimani wakiwa katika msafara wa magari manne yaliyosheheni askari wa FFU.
Hata hivyo akijibu hoja hiyo, Hakimu Pinja alisema kwamba amesikia maelezo yaliotolewa na Mawakilishi na hivyo maamuzi zaidi yatayolewa katika tarehe nyengine ya kutajwa kesi hiyo mahakamani hapo. Kesi ya watuhumiwa hao imeahirishwa na inatarajiwa kutajwa tena mahakamani hapo Novemba 21 mwaka huu.

No comments: