ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 16, 2012

‘Viongozi wengi sio waadilifu’

MADAI ya ubadhirifu wa fedha na rasilimali za nchi unaofanywa na baadhi ya viongozi wakiwemo wanaoficha fedha nje ya nchi yanatokana na  viongozi hao kushindwa kuzingatia uadilifu na misingi iliyoachwa na hayati baba wa Taifa,Mwalimu Julius Nyerere.

Mhadhili wa Chuo kikuu cha Mtakatifu Augustine na mwanaharakati wa mabadiliko ya katiba,Mwita Nyamaka alitoa kauli hiyo juzi kwenye mdahalo wa elimu ya Katiba, uwajibikaji na utawala bora, jinsia katika nafasi za maamuzi na mabadiliko ya tabia nchi uliofanyika kijiji cha Nyehunge Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.

Mdahalo huo wa elimu ya Katiba unaotolewa katika tarafa saba za Wilaya ya Sengerema na mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali wilayani hapa (SENGONET) umekuja wakati tayari tume ya mabadiliko ya katiba ikiwa imepita kukusanya maoni ya wananchi Septemba 27 hadi 30,mwaka huu.


Alisema kitendo hicho kinatokana na viongozi hao kutozingatia sheria za nchi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inamtaka kiongozi yeyote kuwajibika kwa wananchi.

Mhadhiri huyo alisema badala ya viongozi hao kuwajibika kwa wananchi,wananchi wamekuwa wakiwajibika kwao na hivyo kusababisha wizi wa fedha ambazo zimekuwa zikifichwa nje ya nchi na baadhi ya viongozi waliowekwa madarakani na wananchi ili wawatumikie.

Kauli hiyo imekuja siku chache kufuatia hivi karibuni kuibuka mjadala mkali katika mkutano wa 10 wa bunge baada ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini,Zitto Kabwe(Chadema), kuwatuhumu baadhi ya viongozi wanandamizi wa Serikali kuficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi.

Zitto akitoa kauli hiyo Novemba 8,mwaka huu wakati akiwasilisha hoja yake binafsi,alisema miongoni mwa watu hao ni wale walioshika nyadhifa za uwaziri wa nishati na madini katika kipindi cha 2003 hadi 2010 na wale waliokuwa makatibu wakuu wa wizara hizo katika kipindi hicho.

Kauli ya mhadhiri huyo ilikuja kufuatia swali lililoulizwa na Benjamini Msheleja mkazi wa Nyehunge aliyehoji uhalali wa viongozi wa Serikali hasa waliochaguliwa na wananchi kujilimbikizia mali kinyume na ibara ya 9(j) ni kwamba shughuli za uchumi haziendeshwi  kwa njia zinazoweza kusababisha ulimbikizaji wa mali au njia kuu za uchumi katika mamlaka ya watu wachache.

''Kama ibara hii inakataza viongozi wa Serikali kujilimbikizia mali au njia kuu za uchumi kwa manufaa ya watu wachache, inakuweje hawa watu wanaotuhumiwa kuficha fedha nje hawachukuliwi hatua,licha ya kuvunja sheria za nchi,''alihoji Msheleja.

Akijibu swali hilo Nyamaka, alisema hali hiyo inatokana na baadhi ya viongozi kutofuata misingi iliyoachwa na hayati Mwalimu Nyerere ambaye asingezingatia uzalendo na wajibu wa kuwatumikia wananchi kijiji cha Butiama kingelingana na jiji la Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa ni wakati umefika wa kuwaondoa viongozi wenye tabia ya kujilimbikizia mali kwa kupima sera zao bila kurubuniwa kwa rushwa za Khanga, fulana, fedha na chumvi wakati wa kampeni za uchaguzi ili kuchagua viongozi wenye moyo wa uzalendo wa kuwatumikia wananchi.

Mkurugenzi wa Sengonet, Bethold Byoma, alisema mbali na kutoa elimu hiyo ya katiba  ili kuwasaidia wananchi kufahamu yaliyomo katika katiba pia mtandao huo umesambaza nakala za katiba zaidi ya 200 kwa wakazi wanaohudhuria midahalo juu ya elimu hiyo.     

Mwananchi               

No comments: