
Maalim Seif Sharif Hamad akipeana mkono na aliyekuwa Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume kwa mara ya kwanza baada ya kuafikiana kuachana na siasa za chuki , kusameheana na kusahau yaliopita, Ismail Jussa alikuwa ameandamana na Maalim Seif siku hiyo walipokwenda Ikulu, siku hii siyo siku ya kusahaulika kabisa hasa tukizingatia mambo matatu hayo ambayo yamewafanya watu hawa wakubaliane ni jukumu letu sote kuhakikisha siku hii tunaienzi na kuithamini kwani Maridhiano ndio uhai wa nchi yetu na watu wake
Hali ya mambo Zanzibar hivi sasa inasikitisha,inataka kurejea katika misukosuko ya kisiasa na siasa za chuki,hasama. Malumbano yanayoendelea baina ya Chama cha Mapinduzi(CCM),Chama cha Wananchi(CUF) na viongozi wa dini hayaoneshi mwelekeo mzuri huko tuendako. Hakuna atakayenufaika ikiwa maridhiano yaliyotafutwa kwa gharama kubwa yatavunjika. Tumewasikia wasemaji wa vyama vya CCM na CUF na kwa upande mwengine pia viongozi wetu katika dini. Ingawa kauli hizo za viongozi hao zinaonekana ni za vitisho; lakini wale waliozitamka si watu wapuuzi, au watu wajinga wasioelewa uzito na umuhimu wa kuyaenzi maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa hapa Zanzibar.
Vita ya maneno inayoendelea ni uthibitisho wa baadhi ya Viongozi wenye dhamana katika vyama vya siasa na katika jamii yetu kukosa ustahimilivu kama lengo mojawapo la maridhiano yaliyofikiwa kuona jamii ya Kizanzibari inavumiliana kwenye siasa,dini na hata mambo mengine.Ni dhambi kubwa kuruhusu hali hii itawale fikra zetu. Zanzibar ina matatizo ya kijamii, matatizo ambayo kamwe hayawezi kutatuliwa kwa njia ya ubabe,vitisho au nguvu ya Dola.
Mwanazuoni mmoja kule Marekani, Profesa Robert Alan Dah ambaye amebobea kwenye sayansi ya siasa katika kitabu chake cha Theory and Methods of Political Science, aliwahi kusema kwamba ”Ni wajibu wa dola kuendesha juhudi za kutafuta suluhu za migogoro ya kijamii. Siasa ni hatua za majadiliano endelevu yenye kuhakikisha migogoro inapatiwa ufumbuzi kwa njia za amani”
Matatizo ya kijamii ya Zanzibar hayataweza kusuluhishwa kwa njia nyigine iliyo bora zaidi ya kurejea kwenye maridhiano ya kisiasa,kutatua tatizo la ajira kwa vijana. Pamoja na njia hizi ni lazima viongozi wakakubali dhamana zao na wajibu wao mbele ya jamii,lakini pia lazima wanasiasa waaminiane kwani kwa hali ya sasa hapa Zanzibar kuna sura mbili ambazo haziaminiani jambo linalosababisha kuiweka majaribuni Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Wazanzibari haya yanayozuka sasa katika nchi yetu yanatulazimisha tutangulize busara na hekima nyingi.Hivyo basi, CCM na CUF, kama kweli wana dhamira za dhati za kuiepusha nchi yetu na balaa la kurejea kwenye vurugu na siasa za chuki, hawana budi wakubaliane kiungwana kuheshimu na kutekeleza kwa dhati maridhiano yaliyofikiwa mwaka 2009. Viongozi wa kisiasa waelewe kwamba dunia imebadilika. Leo dunia inafuatilia kwa karibu yanayotokea katika nchi mbalimbali na tunafahamu viongozi wenzenu wa kisiasa wapo mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita dhidi ya makosa ya binadamu kule The Huegue, Uholanzi, nanyi mnaochochea na kunufaika na vurugu, mjiandae ipo siku mtapelekwa The Huegue.
Wazanzibari haya yanayozuka sasa katika nchi yetu yanatulazimisha tutangulize busara na hekima nyingi.Hivyo basi, CCM na CUF, kama kweli wana dhamira za dhati za kuiepusha nchi yetu na balaa la kurejea kwenye vurugu na siasa za chuki, hawana budi wakubaliane kiungwana kuheshimu na kutekeleza kwa dhati maridhiano yaliyofikiwa mwaka 2009. Viongozi wa kisiasa waelewe kwamba dunia imebadilika. Leo dunia inafuatilia kwa karibu yanayotokea katika nchi mbalimbali na tunafahamu viongozi wenzenu wa kisiasa wapo mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita dhidi ya makosa ya binadamu kule The Huegue, Uholanzi, nanyi mnaochochea na kunufaika na vurugu, mjiandae ipo siku mtapelekwa The Huegue.
Vita ya maneno haina mwisho mwema na kwa vyovyote vile viongozi hawataweza kukwepa mzigo mkubwa wa lawama kwa kushindwa kwao kutumia busara na hekima kuepusha shari, kwani ilivyokuwa wenye kutamka kauli hizo ni watu makini wanaolijuwa kila wanalolitamka na kulitenda halitakuwa ni jambo la busara kuzipuuzia kauli zao hizo na hasa tukitazama vitendo vilivyoanza kujitokeza vyenye kuashiria mwelekeo mbaya wa kisiasa Zanzibar na hatma mbaya ya maridhiano ya Wazanzibari.
Kwa wenye macho hawahitaji kuambiwa watazame, Wale wachunguzi wa mambo wanaweza kuona kwamba kauli hizo hazina maana nyingine yoyote isipokuwa kuonesha kuwa hali ya mambo Zanzibar si shwari. Kama hatua za makusudi na za haraka hazitachukuliwa, kuna kila uwezekano Zanzibar ikajikuta inarejea nyuma kwenye zama za siasa za chuki, hasama ambazo hazikumnufaisha yeyote yule zaidi ya hasara tuliyoipata Wazanzibari kwa miaka nenda miaka rudi.
Tukumbuke kuwa Zanzibar ikitumbukia katika machafuko baada ya watu wachache kwa maslahi yao binafsi kuwasha moto na kwa kuwa kawaida ya moto ukishawaka pana taabu ya kuuzima, Basi ni busara ya hali ya juu kwa sasa kukinga kuliko kuponya na kinga ya yote hayo ni kudumisha kwa imani moja tu maridhiano ambayo waasisi wake bado wapo, Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad.
Viongozi hawa walifikiri mbali na pia walimtanguliza Mwenyezi Mungu mbele kwani iwe itakavyokuwa kesho mbele ya haki wana masuala ya kujibu, hivyo kujiweka katika nafasi ya kufaulu mtihani mgumu mbele ya Mola, Dk Karume na Maalim Seif waliamua kwa msimamo thabiti kuepusha shari iliyokuwa ikiinyemelea Zanzibar isitokezee ambapo tulishuhudia hali ya mambo ikirejea katika hali ya kawaida kwa miaka mingi tangu kuanza kwa siasa mwaka 1957.
Rais mstaafu wa awamu ya tano Zanzibar,Dk. Salmin Amour aliwahi kutamka mwaka 2000 kabla ya kustaafu nafasi ya Urais kwa mujibu wa katiba kwamba hataki kuiona Zanzibar ikigeuzwa Rwanda kwa maana ya mauaji yaliyokezea mwaka 1994. Kauli ile ya Dk. Salmini ilikuwa ni ya kizalendo na ya ujasiri mkubwa hususan kuwapinga watu walio nje ya Zazibar wanaotaka kuleta chokochoko na kuifanya Zanzibar kuwa uwanja wa mazoezi kutopata nafasi hiyo. Hapana shaka wenye nia zao watakuwa walichukizwa na ujasiri wa Dk. Salmin siku zile.
Haipendezi wala haijuzu kuongoza mambo, hasa yanayohusu maslahi ya nchi na wananchi kwa kutumia jazba na ushabiki. Uongozi wataka hekima na busara au uadilifu utatoweka! Kiongozi kabla hajanena au kutenda apime matamshi yake na mustakabali wa maneno na vitendo vyake katika taathira ya jamii inayomzunguka. Tukumbuke “Majuto ni mjukuu!”
Kama kweli Wazanzibari na hasa wanasiasa wanania ya kuona Zanzibar ikibakia kwenye utulivu na maelewano ni lazima kila mmoja wetu akawa muumini wa kweli wa maridhiano, awe Serikalini, nje ya Serikali, awe CCM, CUF, Jahazi Asilia, AFP, Viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kutekeleza kwa vitendo maridhiano kwani Zanzibar ni muhimu zaidi kuliko maslahi ya kisiasa.
Karume ni Rais wa sita Zanzibar aliyeanza kutawala kuanzia mwaka 2000 hadi 2010 ameiwacha Zanzibar ikiwa katika hali ya maelewano makubwa. Tusijifanye hamnazo, tunaelewa vema hali ilivyokuwa ambapo misuko suko ya siasa za chuki,hasama na kudumaa kwa maendeleo ilishamiri huku watu kwa wakati ule walitumia muda mwingi kubishana siasa zisizokuwa na tija kwao wala vizazi vyao baadaye.
Zanzibar kwa miongo mingi imekuwa yenye siasa chafu, siasa ambazo zilikuwa ni sehemu ya maisha ya Wazanzibari. Wazungu walijaribu kurekebisha hali hiyo,lakini wakashindwa kwa sababu wenyewe walikuwa sehemu na chanzo cha mivutano ya kisiasa katika Visiwa hivi.
Madhara ya siasa ya chuki ni makubwa sana maana ubaya wake unazidi ule wa chuma kuliwa na kutu maana sumu ya mtu ni chuki. Siasa za kabla ya maridhiano zilikuwa ni zile za kubaguana, kushupaliana huku kila uchaguzi ama ukikaribia au ukifika lazima watu watakufa.Watu walisusiwa harusi, maziko, waumini walifikia hata kususia misikiti,wengine maduka, sokoni walisusiana kununua bidhaa huku wengine wakifikia kutoa talaka au kudai kwa waume zao kwa sababu ya tofauti za vyama vya siasa!
Kilele cha ghasia na hitimisho la siasa za chuki na uhasama kilifikia Januari 26 na 27 pale Chama cha Wananchi (CUF) kilipoitisha maandamano nchi nzima maandamano ambayo yalipigwa marufuku na Dola,lakini CUF hawakusikia na matokeo yake watu wakapoteza maisha akiwemo askari Polisi mmoja kule Pemba kuchinjwa kama kuku!
Baada ya matukio yote hayo, Karume akiwa Rais Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alifungua milango ya mazungumzo na Chama cha CUF yaliyozaa Muafaka II ambao gaukuweza kuwa tiba sahihi kwa matatizo ya Zanzibar.Rais Jakaya Kikwete alihutubia Bunge la Tanzania kwa mara ya kwanza baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, aliweka bayana msimamo wake wa kumaliza mpasuko wa kisiasa Zanzibar. Akaagiza Katibu Mkuu wa Chama chake kwa wakati huo,Yussuf Makaba na yule ya CUF, Maalim Seif Shariff Hamad kukutana kujadili suala hilo.
Maridhiano ya kisiasa yakafikiwa mwaka 2009 na kusababisha katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kufanyiwa mabadiliko yaliyowezesha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Rais Kikwete ni muungwana ambaye ametekeleza ahadi yake ya kuupatia dawa mpasuko wa kisiasa Zanzibar. Katika hali ya sasa tunawaomba watu na hasa wanasiasa kuacha kuwachochea vijana katika misingi ya siasa za chuki na hasama, hasina mwisho mwema.
Mpaka lini Wazanzibari tunaendelea kugawiwa kama samaki nasi tukakubali kugawiwa kwa misingi ya itikadi za kisiasa. Kwa nini viongozi wetu wa kisiasa badala ya kuweka maslahi ya Zanzibar mbele, wao wanaweka mbele maslahi yao au maslahi ya vyama vyao? Inafaa Wazanzibari tukaelewa kuwa huu si wakati muafaka wa kuvuruga maridhiano yetu. Huu si wakati wa kutazama maslahi ya mtu binafsi wala chama! Ni wakati wa kutazama maslahi ya Zanzibar na mustakabali wa Wanzanizbari katika katiba mpya.
No comments:
Post a Comment