SIKU chache bada ya Baraza la Vijana wa Chadema Mkoa wa Mwanza kutamka kuwa hawako tayari kuunga mkono maandamano ya kumpinga Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Wilbrod Slaa,
Bavicha Mkoa wa Singida, wameibuka na kuwaunga mkono wenzao wa Mwanza kwa kusema kuwa watasimama nyuma ya Katibu Mkuu huyo hadi mwisho wa mapambano.
Kupitia taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya habari na Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Singida, Josephat Isango, vijana hao wameeleza kusikitishwa kwao na wenzao wanaompinga Dk Slaa, huku wakidai kuwa wenzao hao wanatumiwa na wanasiasa wa upande wa CCM.
Walidai kuwa huo ni utekelezaji wa propaganda kutoka Idara ya Uenezi ya CCM.
Walidai kuwa huo ni utekelezaji wa propaganda kutoka Idara ya Uenezi ya CCM.
Katika siku za karibuni vyombo vya habari viliripoti hatua iliyoelezwa kuwa ya Bavicha, kumshinikiza Dk Slaa kuachia ngazi kwa madai ya kumiliki kadi ya CCM, madai yaliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.
Isango katika taarifa hiyo ya jana alidai kuwa, baadhi ya vijana waliofukuzwa na Chadema kutokana na utovu wa nidhamu, ndiyo wamekuwa wakiendeleza mapambano hayo ili kukichafua Chadema, kionekane kuwa na migogoro wakati ukweli ni kwamba hakuna hali hiyo.
Alisema kuwa Vijana wa Singida walifanya uchunguzi na wabaini kuwa baadhi ya vijana wenzao ndiyo wanaotumiwa na Nape kwa masilahi ya CCM.
Kutokana na hilo, Isango alimtaka Nape kuachana na kile alichokiita kuwa ni siasa za maji taka, akieleza kuwa siasa hizo zinalenga kuwarubuni na kuwaaminisha Watanzania kuwa CCM peke ndicho chama bora wakati siyo kweli.
“Hata hivyo, vijana waliosimamishwa uongozi ndani ya Chadema ni vyema wakajiunga na CCM wazi ili wakasaidie mafisadi waliosababisha maisha magumu kwa Watanzania. Watanzania wanajua hali yao ya maisha na ndiyo waamuzi sahihi wa Tanzania wanayoitaka, tusiwalishe maneno ya uongo kurutubisha ufisadi nchini,” alisema.
Isango aliongeza: “Ni imani yetu kuwa, kila jambo linalofanywa ndani ya Chadema linakuwa na baraka njema kwa ajili ya ukombozi wa nchi yetu, lakini yako yanayofanywa kwa mashinikizo mabaya kama hili hayana nia njema kwetu.”
Mwenyekiti huyo aliwatuhumu baadhi ya viongozi wa ngazi za juu ndani ya CCM kuwa wamekuwa wakitumika kwa ajili ya kukisambaratisha Chadema kwa mashinikizo yao binafsi na kwamba watu hao wanatamani kuona siku moja Chadema kikisambaratika.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment