ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, December 1, 2012

HATARI Asbetos: Watanzania wafa kimyakimya

Licha ya mabati ya asbestos kupigwa marufuku duniani kutokana na kusababisha saratani na kuathari mazingira, nyumba za serikali zimeendelea kubakia na mabati hayo hali inayotishia afya za familia zinazoishi kwenye nyumba hizo.

Mabati haya nchini yalitumika kwenye ujenzi na pia ilichanganywa na malighafi nyingine kuzalisha bidhaa mbalimbali za viwandani.

Hata hivyo licha ya kukataza matumizi ya bidhaa hizo miaka ya 1990, maelfu ya familia nchini zinaishi kwenye nyumba zilizoezekwa na asbestos bila hatua za kubadilishwa mabati hayo kuchukuliwa.



Gazeti hili lilithibitisha kuwa licha ya kupiga marufuku matumizi ya asbestos hakuna sheria iliyoamuru ziondolewe na kuharibiwa. Nyumba za serikali na za watu binafsi zimeendelea kubaki na mabati hayo  licha ya kuhatarisha afya kwa wakazi.

Wafanyakazi wa Shirika la Umeme (Tanesco)  wanaoishi Ubungo jijini Dar es Salaam kwa karibu miaka 40 wameendelea kuvuta  sumu ya asbestos pia wakinywa maji ya mvua yanayokingwa kwenye mabati hayo.

Katika mahojiano na wafanyakazi hao wa Tanesco, NIPASHE ilibaini kuwa hawaelewi kuwa wanaishi kwenye sumu na baadhi ya maofisa wa idara ya miliki walipoulizwa iwapo wameliomba shirika hilo  kubadilisha mabati walisema hawajafanya hivyo.

Makazi mengine ambayo mabati ya asbestos yanaendelea kutumiwa ni kwenye nyumba za polisi mfano kwenye kituo cha polisi cha Oysterbay jijini Dar es Salaam, nyumba za askari hao zimeezekwa kwa asbestos kadhalika ofisi wanazotumia.

Familia za askari hao zinachota maji ya mvua yenye vumbi na vipande vya asbestos bila kujua kuwa wanahatarisha afya zao.

Makazi mengi ya polisi na majeshi yana nyumba za asbestos na hakuna jitihada zinazochukuliwa kuondoa mabati hayo ili kulinda afya zao wakati wakisubiri ujenzi wa nyumba mpya.

Hospitali ya Mwananyamala licha ya kujenga majengo mapya inaendelea kutoa huduma kwenye sehemu zilizoezekwa na asbestos mfano wa  wodi ya wanawake na watoto.

Makanisa yana majengo yaliyoezekwa na asbestos mfano Kanisa la Kipentekoste lililoko Kinondoni Biafra  na Kanisa Katoliki Mbezi Louis ni miongoni mwa mengi ambayo wakazi wake wameendeelea kudhurika na  athari za mabati hayo.

KITAALAM ASBETOS NINI 
Nyuzinyuzi za asbestos kitaalamu ni imara haziungui kwa urahisi na mara nyingi zimetumiwa kwenye kutengeneza vifaa vya ujenzi na vya umeme.

Baadhi ya bidhaa hizo  ni pamoja na  dari, vigae, mabati, vifaa vya umeme, wakati mwingine breki na klachi za magari.

ATHARI 
Kwa mujibu wa Idara ya Afya na Huduma za Watu ya Marekani bidhaa hii ni chanzo cha maradhi ya saratani ya ngozi,  tumbo, koo na  mapafu. Kinacholeta maradhi haya ni kuvuta vumbi ama kula chembechembe zake hasa kutokana na mabati haya kuchakaa kutokana na kukaa muda mrefu.

Baadhi ya mafundi wa ujenzi na umeme huvaa glovu zilizotengenezwa na asbestos ambazo pia ni sumu kwa vile kemikali zake hubakia mikononi.

Kwa kuvuta vumbi ama kunywa maji yenye nyuzinyuzi za  asbestos, mabaki yake yanajikusanya kwenye mapafu ama tumboni na baadaye huleta madhara.

Tafiti za kiafya zinaonyesha kuwa asbestos zinasababisha saratani ya utumbo mkubwa na njia ya haja kubwa na imethibitika kuwa ni chanzo cha saratani ya vifuko vya mayai  kwa wanawake.

Idara hiyo ya afya ya Marekani katika taarifa zake za mtandao inaeleza kuwa asbestos ni chanzo cha saratani na madhara makubwa yapo kwa wanaoishi kwenye nyumba zenye bidhaa zinazotokana na asbestos (dari au mabati) kwa muda mrefu.

“Madhara ya asbestos yanaanza kuonekana  kuanzia  miaka 10 hadi  30,” iIisema ripoti ya Idara ya Afya na Huduma za Watu ya Marekani.

MOYO
Kuna ushahidi kuwa kuvuta hewa ya  asbestos kunaongeza saratani za tumbo, koo, kongosho na figo lakini pia hudhuru moyo.

“Inaleta makovu kwenye mapafu yanayosababisha shida ya kupumua na kupunguza kiwango cha damu kwenye mapafu hali inayobana mishipa ya moyo na kuusababisha kuwa mkubwa.”  Ilisema na kuongeza kuwa athari zake ni vifo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: