Thursday, December 27, 2012

JIANGALIE, SHIDA ZAKO ZITAKUFANYA UACHWE!


NI wiki nyingine tena tunakutana kupitia safu hii ya Mashamsham nikiamini umzima na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku kama kawaida baada ya kusherehekea sikukuu ya Chrismas kwa furaha.
Mimi mzima na niko tayari kabisa kukuletea mada nyingine kali baada ya wiki iliyopita kuzungumzia ishu ya kupendwa na kutamaniwa. Kwa kifupi kwenye mapenzi kuna mambo hayo mawili hivyo unachotakiwa kufanya ni kuwa makini na mtu anayekutokea na kukuambia anakupenda.
Fanya uchunguzi kabla ya kumkubalia kwani huenda kakutamani na baada ya kukumega anaingia mitini na kukuacha unalia.
Baada ya hayo machache kuhusiana na makala hiyo ya wiki iliyopita, sasa tugeukie katika mada yetu ya leo ambapo tunaangalia madhara ya mtu kuwa tegemezi kwa mpenzi wake kwa asilimia mia moja.
Wanawake wana hulka karibu sawa kama nilivyotangulia kusema katika makala zangu zilizopita, kwa upande wa wanaume ni tofauti kidogo. Wanaume wana hulka tofauti kulingana na matakwa na utashi wao, japokuwa kuna baadhi ya vitu huwa wanakaribiana sana hasa katika kutoa uamuzi.
Wanaume wengi hufikiria sana kabla ya kufikia hatua ya kutoa uamuzi, lakini kwa bahati mbaya wanaume wengi baada ya kutoa maamuzi huwa hawarudi nyuma.
Yaani wao ni mbele kwa mbele, tofauti na wanawake ambao huwa na uamuzi wa haraka lakini baada ya kukaa kwa muda na kufikiri sana hujiona wakosaji na kutaka kurekebisha uamuzi wao.
Nimetanguliza hayo kwa makusudi kabisa, unapaswa kufahamu kuwa mume wako au mchumba wako unapomfanyia mambo asiyoyapendelea au unapomuonesha tabia zisizofaa, hukuvumilia kwa muda lakini kumbuka akiona tabia hiyo inakidhiri ni mwepesi sana kukuacha.
Ndugu zangu, ishu ya baadhi ya wanawake kuwa tegemezi hata pale pasipostahili imekuwa kama ‘fashion’ sasa. Baadhi wanapokuwa na wapenzi wao, huona kama wamepata mahali pa’ kutatua shida zao zote bila kujua kuwa dhana hiyo ni mbaya! Nani amekwambia kuwa na mpenzi ndio sehemu ya kumaliza matatizo yako yote?
Bahati mbaya siku hizi wameongeza majina, zaidi ya jina la buzi lililozoeleka huko nyuma, siku hizi huitwa ‘ATM’ yaani wanaume wamefanishwa na mashine ya kutolea fedha ambapo ukizihitaji unachukua wakati wowote.
Wanaume wa sasa hawapo hivyo, wanahitaji mwanamke mwenye malengo ambaye atakuwa na msaada mkubwa katika maisha yake. Hakuna mwanaume ambaye anategemea kuishi na mwanamke asiye na kazi wala mpangilio unaoeleweka wa maisha yake ya baadaye, hakuna mwanaume anayetegemea kuwa na mwanamke ambaye atarudisha nyuma maendeleo yake.
Utakuta mwingine anamtegemea mpenzi wake kwa kila kitu, mara simu yangu haina dola, mara sina pesa ya kula, yaani matatizo chungu nzima.
Sawa haikatazwi kumwambia mpenzi wako shida zako lakini ikizidi sana inakuwa kero, usimtegemee kwa kila kitu, kwani kabla ya kuwa naye ulikuwa unaishi vipi?
Mwanaume anapogundua kuwa wewe ni tegemezi kwake kwa kila kitu, unampa wasiwasi kwamba huna nia ya kuwa naye katika maisha yake yote, badala yake umepanga kumfanya kitega uchumi.
Mapenzi ya siku hizi kusaidiana, siyo kila kitu mpaka mpenzi wako, vitu vingine fanya mwenyewe, au kama mna utaratibu wa kusaidiana katika matatizo mbalimbali, sio kila siku wewe ndio mwenye matatizo!
Shauri yako, kama nilivyokuambia awali, maamuzi ya wanaume hayabadiliki kirahisi sasa jiangalie usije ukampoteza mpenzi wako kwa vitu visivyo na msingi.
Kwa leo niishia hapo, niwatakie heri ya Mwaka Mpya

Chanzo:Global publishers

No comments: