Alisema ndiyo maana Serikali imetoa fursa kwa kila Mtanzania kujitokeza na kutaja jina ama majina ya watu wanaotuhumiwa.
Dk. Mgimwa alitoa taarifa hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi kabla ya kuhutubia kwenye mahafari ya kwanza ya wahitimu wa kozi ya Mipango na Maendeleo vijijini ngazi ya cheti katika tawi la kanda ya Ziwa (Mwanza).
“Ni kweli madai hayo yapo, Lakini Serikali hata siku moja haiwezi kukurupuka na kutoa maamuzi ikiwemo kukamata watu hovyo hovyo pasipo kufuata sheria, kanuni pamoja na taratibu za Kamataifa,” alisema Dk Mgimwa ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafari hayo.
Alizitaja baadhi ya taratibu hizo kuwa ni kupatikana kwa majina pamoja na ushahidi wa majina ya watuhumiwa, malalamiko hayo kupitiwa na kitengo cha upelelezi wa kimataifa (Financial Intelligency Unit) na Serikali ya Uswiss kuwa tayari kuthibitisha kwamba ni kweli fedha hizo zimehifadhiwa nchini humo kwa nia ovu.
Dk Mugimwa alisema kwa mujibu wa sheria, siyo kila fedha zinazohifadhiwa nje ya nchi ni fedha haramu.
“Ndiyo maana sasa hivi tuna mpango wa kuanzisha utaratibu wa kutunza fedha nje ya nchi kwa ajili ya akiba ya kigeni kwa kipindi cha miezi minne wakati tunapopata dharura” alisema.
Alikanusha madai ya waandishi wa habari kwamba huenda serikali inaogopa kuwakamata na watuhumiwa ndiyo maana hakuna hatua yoyote iliyokwishachukuliwa.
“ Siyo kwamba tumenyamaza ama tunaogopa kuwakamata watuhumiwa na kuwashukulia hatua za kisheria, hapana. Kwa mfano, hadi sasa tunawasiliana na Uswiss (serikali) ambayo wengi wanasema ndiko ziliko fedha; kinachotakiwa na ambacho ofisi yangu inakifanya sasa hivi ni kufuata taratibu za kimataifa,” alisema na kuongeza kuwa ni mapema mno kuilaumu Serikali ya Tanzania.
Alifafanua kwamba kwa kulitambua hilo, ndiyo maana Serikali imetoa mwanya kwa kila Mtanzania anayedhani kwamba anao ushahidi wa kutosheleza kuwasilisha majina ya watuhumiwa kwa njia ya siri ili yafanyiwe kazi.
Hata hivyo, wakati akihutubia kwenye mahafari hayo, Dk Mgimwa aliwataka wahitimu hao kuwa mfano wa kuigwa kwa kutofanya kazi kinyume na maadili ya kazi .
Aliuahidi uongozi wa chuo hicho kwamba ofisi yake itakuwa bega kwa bega katika kukabiliana na changamoto kadhaa zinazokikabili chuo hicho.
Awali, Mkuu wa chuo hicho, Costantine Lifuliro alimweleza Dk Mgimwa kwamba chuo kinakabiliwa na upungufu wa vitendea kazi.
Alivitaja vitendea kazi hivyo kwamba ni pamoja na vitabu kwenye maabara, upungufu wa kompyuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa chuo kwa vile hadi sasa chuo hicho kinatumia majengo ya kanisa la Africa Inland Church Tanzania(AICT).
Alisema jumla ya wanachuo 323 wamehitimu mafunzo ngazi ya cheti.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment