BADO siku chache tusherehekee Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya. Tumuombe Mungu atujalie afya njema ili tuweze kujumuika na wenzetu katika siku hizi muhimu kwetu.
Ndugu zangu, leo nataka kuzungumzia mambo mawili katika uwanja wa mapenzi. Hivi unajua kwamba kuna kupenda na kutamani katika mapenzi? Hivi unatambua kwamba wanaume wengi siku hizi siyo kwamba wanawapenda kwa dhati wale walionao bali wamewatamani tu kutokana na mvuto walionao?
Huenda ukawa hujui na yawezekana kabisa wewe mwanamke unayesoma hapa uko kwenye uhusiano na mwanaume ambaye amekutamani na wala hana mapenzi ya dhati na wewe na ndiyo maana unaona migogoro haiishi.
Wapo wanaume wengi huwatokea wanawake kwa maelezo kwamba wamewapenda lakini mioyo yao inaweka wazi kwamba wamewatamani tu. Huo ndiyo ukweli wenyewe, nasema hivyo baada ya kufanya utafiti kuhusu hilo.
Unakuta mvulana anakutana na msichana mrembo kisha kumtamkia wazi kwamba eti kampenda. Hivi hujawahi kumsikia mtu anamtongoza msichana kwa kumwambia; ‘Yaani nimetokea kukupenda ghafla, naomba uwe mpenzi wangu.”
Ni sawa unaweza kutokea kuvutiwa na mtu fulani baada ya kukutana naye kwa mara ya kwanza lakini utafiti unaonesha kwamba, wengi wetu tumekuwa tukiwatamani tu baadhi ya watu na siyo kwamba tunakuwa na mapenzi ya dhati dhidi yao.
Ukifuatilia sana utabaini kuwa kwa sasa baadhi ya wanaume wanapokutana na wanawake wenye makalio makubwa, kifua chenye mvuto, macho yaliyolegea, uvumilivu huwashinda.
Yaani ni wachache sana ambao watavumilia kupishana nao bila ya kuwaangalia kwa zaidi ya mara moja. Mbaya zaidi wengine hawaishii kuangalia tu bali hudiriki kuwatamtamkia kwamba wamewazimikia.
Kuthibitisha si kwamba wamewapenda kwa dhati utakuta watakapokubaliwa na kupewa penzi mara moja ama mbili huingia mitini.
Hii inaonesha dhahiri siyo kwamba wamewapenda bali wamewatamani kimapenzi na ndiyo maana wakifanikiwa kukiona wazi kile kilichowavutia wanakinahi na kupotea.
Kimsingi wapo wanawake wazuri tu ambao wameingia katika mapenzi ya kuumiza kutokana na kutamaniwa.
Utakuta mapenzi yao hayana muda mrefu lakini migongano ya hapa na pale haiishi ikiwa ni pamoja na kusalitiana.
Kwa maana hiyo kuna kila sababu ya wanawake kuwa makini sana na hawa wanaume wanaojifanya wametokea kuwazimikia ghafla. Wajue kwamba wakikubali kuingia kwenye uhusiano na wanaume waliowatamani watakuwa wamejiingiza kwenye matatizo.
Kinachotakiwa kufanyika ni kumsoma mtu kabla ya kumpa nafasi kwenye moyo wako. Hili linawahusu sana wale ambao wanajijua kwamba wanawadatisha wanaume kwa muonekano wao.
Usikurupuke kumpa nafasi mwanaume bila kujiridhaisha kama kweli ni mkweli na kwamba kile anachokisema kinatokana moyoni mwake.
Upe moyo wako kazi ya kufanya tathmini,ukiridhika uliyempata ni sahihi na hakuna usanii ndani ya maneno yake kwamba anakupenda, kubaliana naye kisha mtangulize Mungu.
Endapo utakubali kuingia kwenye uhusiano na mtu aliyekutamani itakuwa imekula kwako.
Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo na niwatakie heri ya Krismasi na Mwaka Mpya.
Chanzo:Globalpublishers
No comments:
Post a Comment