ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 26, 2012

Tas Mwanza yalaani albino kuzikwa ndani ya duka


Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi (Tas) mkoani Mwanza, kimelaani vikali kitendo cha familia moja wilayani Magu kumzika ndani ya chumba cha biashara mtoto wao mwenye ulemavu wa ngozi (albino).

Mtoto huyo aliaga dunia Desemba 15, mwaka huu nyumbani kwao mjini Magu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Mwenyekiti wa Tas Mkoa wa Mwanza, Alfred Kapole, alisema kimsingi chama chake hakikubaliani na kitendo hicho ambacho kilifanyika usiku wa manane bila kuishirikisha jamii ya eneo husika.

Kapole, ambaye alikuwa ameongozana na viongozi wenzake wa chama hicho mkoani Mwanza na taifa, alisema hatua yao ya kulaani kitendo hicho inatokana na ukweli kuwa inaweza kuchochea mauaji dhidi ya albino.
Alifafanua kuwa wiki iliyopita, alipokea taarifa kutoka wilayani Magu kuwa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Witness Edward Omari, mwenye umri wa miaka miwili na miezi saba, mkazi wa mtaa wa Isandula mjini Magu, amefariki dunia na mwili wake kuzikwa ndani ya chumba cha biashara kinachomilikiwa na baba yake.

Aidha, alisema taarifa hizo zilieleza kuwa siyo tu kwamba mtoto huyo alizikwa ndani ya chumba cha duka, bali pia kitendo hicho kilifanywa usiku wa manane bila jamii ya eneo husika kushirikishwa.

“Nilipigiwa simu na mwenzetu mmoja kutoka Magu akaniambia kwamba baada ya Witness kufariki dunia, alizikwa ndani ya chumba cha duka, na kweli tulipokwenda kuitembelea familia yake, tuliingizwa ndani ya chumba hicho kuonyeshwa kaburi lake,”alisema Kapole.

Aliongeza kwamba taarifa zaidi walizozipata zinasema kuwa mwili wa mtoto huyo ulichukuliwa na wazazi wake kutoka chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Wilaya ya Magu Desemba 16, mwaka huu majira ya usiku kwa ajili ya kwenda kuuzika.

Ofisa Uhusiano wa Tas taifa, Josephat Toner, alisema wao kama jamii ya albino, hawakubaliani na kitendo hicho kwa sababu kinakiuka misingi ya ubinadamu na pia kinaweza kuchochea mauaji dhidi yao.
Alisema katika jamii nyingi za Watanzania, wanaamini kuwa albino hawafi kifo cha kawaida bali hupotea, hali ambayo imekuwa ikichochea mauaji dhidi yao kwa baadhi ya watu kudhani kuwa viungo vyao si vya kawaida na vinaweza kusababisha utajiri.

Kwa msingi huo, alisema kitendo cha familia ya Witness kumzika mtoto wao ndani ya chumba cha biashara tena usiku wa manane pasipo kuishirikisha jamii, kinaweza kuchochea imani hiyo potofu kwamba albino hawafi bali hupotea.

“Albino ni binadamu kama binadamu wengine, tunazaliwa na kufa, hivyo mazishi yetu yanapaswa kufanyika hadharani kama vile mazishi ya watu wengine yanavyofanyika, lazima `wananzengo' (wanajamii) washiriki kwa taratibu zilizozoeleka ili kuondoa kabisa dhana potofu kwamba hatufi bali tunapotea,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu wa Tas Mkoa wa Mwanza, Mashaka Tuju, alisema kitendo kilichofanywa na familia ya Witness, kimewatia simanzi kiasi cha kuwafanya wawe na hisia mbaya dhidi ya familia hiyo.

Alifafanua kwamba ingawa Witness alikufa kifo cha kawaida baada ya kuugua kwa muda mfupi, lakini namna ambavyo mwili wake umezikwa ndiko kunakowatia shaka na kuhisi kuwa huenda kuna jambo limejificha.

Alisema kama lengo la familia hiyo lilikuwa kuepusha uwezekano wa watu wenye imani potofu kufukua kaburi la mtoto wao, ni bora wangemzika katika makaburi ya jamii na kujengea zege lakini sio kumzika ndani ya chumba cha biashara tena kwa siri.

“Kutokana na mazingira ya tukio lenyewe, kama chama tumeamua kufungua jalada la shaka na kuiomba mahakama itoe kibali kwa Jeshi la Polisi kufukua kaburi la Witness ili tujiridhishe iwapo kweli mwili wake una viungo kamili kwa sababu hata mahali penyewe tulipoonyeshwa kuwa ndipo alipozikwa, hapaonyeshi dalili hizo,” alisema.

Alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu, alisema hajapata taarifa.

Hata hivyo, alisema kama tukio hilo lipo ni vema viongozi wa Tas wakamuona Mkuu wa Polisi Wilaya ya Magu ili alishughulikie.

“Mimi sina taarifa pengine Tas walikuja ofisini wakati nimetoka, lakini nitafuatilia kujua kama walizungumza na wasaidizi wangu ili tumwelekeze OCD alishughulikie ingawa suala la kufukua kaburi linahitaji kwanza kibali cha mahakama,” alisema Kamanda Mangu.

CHANZO: NIPASHE

No comments: